Habari za Punde

Msaidizi wa Mganga Huwa Hafukuzwi.

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Tangu awali eneo lote la Ulanga, Malinyi na Kilombero lilikuwa chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Aprili 21, 1964 ndipo Vatikani ilitangaza eneo hilo kuwa Jimbo Katoliki la Mahenge linalosimamiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Jimbo hilo likipewa Askofu wake wa kwanza Baba Askofu Elias Mchonde, baada ya eneo hilo kuwa jimbo na mipaka yake ikawa kwa Magharibi wakipakana na Dayosisi ya Iringa, Kusini Mashariki wakipakana na Dayosisi ya Songea na Njombe, Kaskazini Dayosisi ya ya Morogoro na Mashariki Dayosisi ya Lindi na Tunduru- Masasi. Kumbuka msomaji hiyo ni mipaka ya majimbo ya Kanisa Katoliki la Roma, siyo mipaka ya kisiasa.

Dayosisi ya Mahenge eneo lake lina milima na mabonde. Eneo kubwa la bonde lipo Kilombero na eneo kubwa na milima lipo Ulanga na Malinyi.

Kabla ya mwaka 1964 Wakatoliki wa Mahenge walikuwa jirani mno na Wakatoliki wa Mzizima (Dar es Salaam) Askofu wao alikuwa mmoja mwahashamu Baba Askofu Kadinali Lauriane Rugambwa. Hata leo hii Jimbo Katoliki la Mahenge linaitika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Miongoni mwa Parokia za Jimbo Kuu la Dar es Salaam kabla ya Aprili 21, 1964 ilikuwa ni Luhombero iliyoanzishwa mwaka 1936. Parokia hii tangu enzi ikitoa huduma za kiroho kwa wanavijiji vya Ikangao na maeneo jirani.

Eneo hilo la Luhombero linatokana na jina la Mto Luhombero ambao unajaa maji mwaka mzima, huku kukiwa na viboko na mamba wengi. Maji yake yanakusanywa kutoka mito mbalimbali ikiwamo Mto Ikangao na Mto Mrundu.

Mto Mrundu unayakusanya maji yake na kuyapeleka Mto Ikangao nao Ikingao unayapelekea Mto Luhombero. Majina haya yote ya mito ndiyo yakawa majina ya vitongoji na vijiji jirani na mito yote.

Parokia hiyo ya Luhombero yenye miaka 86 sasa ikitanguliwa parokia mbili kongwe ikiwamo parokia ya Kwiro iliyoanzishwa mwaka 1902 sasa ina miaka 120.

Wakati parokia hii inaanza baba wa babu zangu walikuwa wakulima wa mpunga jirani na eneo hilo lenye rutuba sana, watoto wao (babu zangu) wakabahatika kupata elimu katika shule zilizopo jirani na eneo hili na baadaye hadi Kwiro.

Ndiyo kusema Ukristo ulifika mapema na kujengwa kwa parokia hiimaana yake kulikuwa na wauumini wa kutosha katika eneo hilo. Hawa wazee waliopata kusoma kidogo walipata kazi za ualimu na kazi zingine ndogo ndogo. ukishapata kazi lazima uwe na mke, siyo kuishi kihuni.Kwa hiyo walirudi nyumbani kwao na kutafuta wake na kwa mila wa Wapogoro mahari inalipa na baba, hauwezi kuoa hadi baba akubaliane na maombi yako.

Babu yangu akarudi kwao akao binti mmoja wa Liheta kwa imani ya Kanisa Katoliki , ndoa ilipokamilika akaondoka na mkewe nakurudi kazini kwake, maisha yakaendelea wakajaliwa kupata watoto kadhaa.

Utaratibu wa maisha ya watumishi ni kama wa sasa, likizo ikifika unabeba familia unarudi kwenu kusalimia ndugu zako na rafiki zako wa zamani.

Siku moja babu yangu akiwa likizo kwao alifunga safari kwa rafiki yake mmoja ambaye alikuwa binti ambaye walisoma naye hadi ualimu na safari hiyo aliambatana mwanae mdogo wa kiume (baba yangu).

Walipofika hapo walizungumza vizuri na kukumbushana maisha yao ya shule na ya chuoni wakati wakisoma ualimu, mwisho babu yangu alimtambulisha mtoto wake wa kiume kwa rafiki yake huyu kike.

Unapokwenda kwa rafiki lazima apike chakula, basi ulipikwa wali na samaki, ulipoiva wakala vizuri, walimaliza mazungumzo yao na baada ya muda wakaanza safari ya kurudi kwao Mrundu huku jua likizama.

Walipofika nyumbani walikuta chakula kipo tayari, babu yangu alikula vizuri kuondoa maswali kwa mkewe mithili ya mtu ambaye alishinda na njaa lakini baba yangu hakula kabisa kwani alikuwa ameshida wali na samaki aliyokula kwa rafiki aliyesoma na baba yake. Kila mmoja akaenda kulala, ilipofika saa nne ya usiku wa siku hiyo hoyo baba yangu akaanza kulalamika tumbo linamuuma sana.

Wakaamua kumbeba mtoto huyo mdogo mwenye umri wa miaka mine (72) hadi kwa mganga(mbui) palikuwa na mwendo lakini walifika huko, walipokelewa usiku huo huo na mganga kuwaeleza wasaidizi wake wampatie dawa za kienyeji ya kumtapisha, akapewa dawa hiyo akaanza kutapika mno vitu vingi vyenye rangi nyeusi, wakakesha hapo hapo hadi asubuhi huku baba yangu huyu akiendelea kupata tahafifu. Kulipokucha mgonjwa akapatiwa uji huku nguvu zikirejea.

Msaidizi wa mganga akatoa mashati ya kwa mtoto mgonjwa kutokula baadhi ya samaki ikiwamo samaki aliyeliwa siku hiyo walipoenda kumtembelea yule mwalimu. Babu yangu akaambiwa na msaidizi wa mganga haya matapishi yanaonesha mtoto amelishwa kitu cha kufisha, kwani mlikula nini?

Babu yangu alieleza safari ile ya kwa mwalimu mwezake. Msaidizi wa mganga akauliza si yule mwalimu, babu alijibu ndiyo. Msaidizi akauliza haukutoa ahadi ya kumuoa? Maana wewe umekwenda kuoa mbali.

“Ndiyo nilioa mbali na yeye kumuacha kwa kuwa sisi ni wakristo hatuwezi kuwa na wanawake wawili, kule Misheni(Parokiani) Luhombero nikifanya hivyo nitaonekana mtoto wa Kazimbaya anaishi maisha ya kipagani.” Babu yangu alijibu.

“Mwanakwetu hadaa haramu binti za watu kama unafuata dini ya misheni(Ukristo).”

Alisema msaidizi wa mganga, wengine wana hasira lakini nakuomba msamehe msilipeleke shauri hili Mwaya (serikalini).

Baada ya baba yangu kupona babu yangu alichukua familia yake na kurudi zake Dar es Salaam.

Naye mganga aliendelea kutibu watu kutoka maeneo mbalimbali, lakini baada ya muda kuliibuka kutokueleana baina ya mganga na msaidizi wake, hivyo mganga kuamua kumuondoa msaidizi huyu.

Kwa kuwa msaidizi alikuwa mgeni wa eneo hilo akitokea huko Ugindoni, alifika kwa kina Makwega kuwaeleza kilichotokea. Ndugu zangu hawa kwa kuwa kwanza walikuwa wakimuogopa mganga walimchukua ndugu huyo hadi kwa padri ndugu huyu alibatizwa akawa anaishi jirani nao, akapatiwa mke mpaka leo hii uzao wake upo.

Mwanakwetu ndugu zangu hawa wanasema kuwa huyu msaidizi wa mganga alipokuwa kwa mganga alikuwa na mbuzi kuku wake aliopewa zawadi na wateja walikwenda kutibiwa hapo lakini mganga alimkataza kuondoka navyo.

Alipofika katika mji wa akina Makwega hakuwa na chochote mikononi zaidi ya nguo zake .Kwa kuwa akina Makwega walikuwa ni walimu wa dini walimpokea nakubaini ndugu huyu alikuwa na vitu vikubwa viwili visivyoweza kushikika; cha kwanza ni elimu ya aina za dawa zilizokuwa zinatolewa kwa mganga huyo na pia siri za wagonjwa ambao walikuwa wakienda kwa mganga kutibiwa. Kwa hiyo wale misheni wakawa na mtaji mkubwa wa mambo yote yanayofanyika kwa mganga.

“Mganga huwa halimi, kama analima basi kwa maelekezo tu, pumzi ya kulishika jembe na kulima miraba hana afadhali ya misheni wanalima kwa kutumia vifaa bora na hata mikono yao.” Siri za mganga zilitoka nje.

Mwanakwetu, mganga alipoteza umaarufu wake na watu walikacha kwenda kutibiwa na hata kila alipotafuta msaidizi katika jamii hii hali ilikuwa tete, watu walikumbuka kisa cha awali cha msaidizi wa mganga na yaliyomkuta.

“Basi huo uganga wake ajitibie yeye mwenyewe aone kama atapata kuku na mbuzi wanaoletwa kila siku.” Mganga alinagwa.

Hali ilikuwa mbaya mganga huyu alifugasha virago na kurudi kwao Ugindoni ama kweli msaidizi wa mganga huwa hafukuzwi.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.