Habari za Punde

SHIRIKIANENI KUWALINDA WATOTO WA KIKE NA WA KIUME-MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wazazi na walezi washirikiane na walimu katika kuwalinda watoto wa kike na wa kiume ili waweze kutimiza ndoto zao kielimu.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watoto hao wasikubali kudanganywa na watu wasiopenda maendeleo yao na badala yake wasome kwa bidii na wahakikishe malengo yao kielimu yanatimia.

 

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 3, 2022) alipozungumza na wanafunzi, wazazi na walimu katika shule ya Sekondari Mandarawe wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.

 

“Kwa sasa kielimu wilaya yetu imepiga hatua kubwa, wanafunzi someni  kwa bidii na Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inawawezesha  kutimiza malengo mliyojiwekea.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Kata zote za Wilaya hiyo zina shule za sekondari na tayari wameanza ujenzi wa mabweni, lengo likiwa ni kuwapunguzia wanafunzi adha ya umbali mrefu kwenda shuleni.

 

“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apelekwe shule na elimu msingi inatolewa bila ada nchini kote.”

 

“Kwenye suala la elimu tumejipanga vizuri na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuunga mkono kwa kutupa sh. milioni 700 za ujenzi wa shule ya sekondari wasichana ya mchepuo wa Sayansi.”

 

Pia, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Namichiga na ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi wasimamie vizuri mradi huo na wahakikishe fedha zinatumika vizuri.

 

Mbali na kukagua ujenzi wa kituo hicho, pia Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo vya Afya cha Kata ya Narungombe pamoja na maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Nangurugai.

 

Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wananchi wahakikishe wanatunza mazingira na kuacha kukata miti hovyo. “Tutunze  mazingira na tusilime katika vyanzo vya maji.”

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, JUNI 03, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.