Habari za Punde

Utamaduni Unalinda Utambulisho wa Taifa - Mhe.Mchengerwa.

 

Na.Adeladius Makwega  – MWANZA.

Serikali imesema kuwa ipo faida kubwa sana katika kutunza na kuhifadhi utamaduni wetu kwa kuwa utamaduni ni silaha ya kujenga msingi imara kwa taifa kwa kuepuka kuwa watumwa wa tamaduni za mataifa mengine kwani kwayo ndio utambulisho wa taifa letu.

Kauli hiyo ya  imetolewa  na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo  nchini Mohammed Mchengerwa Juni 19, 2022 katika tamasha la utamaduni la Usukuma Bulabo linalofanyika mkoani Mwanza  ambalo limezinduliwa na litadumu kwa siku saba.

“Changamoto zilizowasilishwa kupitia risala yenu, wizara imeyapokea na mengine yameshaanza kufanyiwa kazi na tunaendelea kuyatatua kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika aidha changamoto nyingine bado tutaendelea kuzifanyia kazi kwani kama mnavyofahamu serikali ya awamu ya sita chini Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu. 

Mheshimiwa Waziri Mchengerwa akiwakilishwa katika tukio hilo la na Dkt. Resani Mnata, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia lugha wa wizara hiyo aliwahimiza wananchi wote na Watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakalofanyika Agosti 23, 2022.

“Zoezi hili lina faida kubwa kadhaa ikiwemo kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya, hali ya ajira, miundo mbinu na barabara, nishati na maji safi. Niwaombe muwape ushirikiano watumishi watakaohusika katika zoezi hii muhimu.”

Awali wakisoma risala yao Umoja wa Watemi wa Usukuma kwa kauli moja  wameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana nao katika kulinda utamaduni wa makabila mbalimbali nchini Tanzania.

“Tunaomba sana wizara yako ikishirikiana na wizara zingine kuendelea kutuunga mkono katika kutangaza amali njema za utamaduni ili kuondoa dhana potovu iliyojengwa katika jamii kuwa mila na tamaduni zetu ni uchawi, ushirikina, upagani na ni ushamba uliopitwa na wakati. Wanasahau kuwa taifa bila utamaduni imara limekufa na mtu asiye na utamaduni ni Mtumwa.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Magu mheshimiwa  Salum Kali amesema kuwa  anayo furaha kubwa kwa kuwa Makumbusho ya Bujora yako katika wilaya yake, hii ni nafasi kubwa ya Wasukuma walio mbali kufika hapa kujifunza utamaduni wao.

“Makumbusho haya ni ushahidi kuwa Waafrika walikuwa na maendeleo makubwa katika maisha yao, Makumbusho ya Bujora ni chachu ya kila kabila kuwa na makumbusha yake.”

Tamasha la hilo  linawakusanya Wasukuma kutoka maeneo mbalimbali huku likihusisha Kanisa Katoliki ambao ndiyo waliohifadhi  kumbukumbu kadhaa za Wasukuma hapa Bujora.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.