Habari za Punde

Watu Wenye Ulemavu Iringa Waomba Kuboreshwa Miundombinu ya Elimu.

Baadhi ya viongozi wa chama cha watu wenye ulemavu mkoa wa Iringa na wadau wa watu wenye ulemavu wakiwa kwenye mafunzo maalamu ya elimu jumuishi.

Na Fredy Mgunda,Iringa.


CHAMA cha walemavu mkoa wa Iringa kimeiomba Serikali kutatua changamoto ya kukosekana kwa miundombini bora ya wanafunzi wenye ulemavu ili nao waweze kupata elimu kama wanafunzi wengine wasio na ulemavu.

 

Akizungumza wakati mkutano Makamu mwenyekiti chama cha walemavu Tanzania(CHAWATA),Iringa Rukia Makweta alisema kuwa mfumo wa elimu maalaumu unachangamoto nyingi ndiyo maana jamii imetakiwa kufahamu umuhimu wa mfumo wa elimu jumuishi pamoja na kwamba miundombinu ni changamoto kwao.

 

Makweta alisema kuwa watoto wenye mahitaji maalumu kuchanganyikana na wengine inatengeneza umoja na kuondoa unyanyapaa kwa kuwa tayari wamezoeana na kupendana pamoja na kupewa ushirikiano kutoka kwa wenzao.

 

“Nafikiria itakuwaje mwanangu atakapoanza masomo? Mazingira hasa ya vyoo kwenye shule nyingi hasa hapa kijijini hayaruhusu mlemavu kusoma, ni bora nibaki nae nyumbani,” Alisema

 

Makweta alisema kuwa sehemu kubwa ya jamii nchini imeendelea kukumbatia utamaduni wa kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu kwa madai mbalimbali ikiwamo ya kuhofia aibu au kuwaona hawatakuwa na uwezo wa kushiriki shughuli za kijamii ikiwamo elimu.

 

Alisema kuwa hata kuwa  Wilaya ya Iringa Kwa muda mrefu kumekuwa na kampeni mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hasa juu ya haki zao za msingi ikiwamo elimu.

 

Makweta alisema kuwa pamoja na kampeni hizo, bado kilio cha watu wenye ulemavu kupata mahitaji yao muhimu ili waishi kama makundi mengine kwenye jamii hakikomi na bado Kuna changamoto lukuki ikiwamo miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu, ni moja ya vilio vinavyowafanya baadhi kushindwa kupata elimu.

 

Mkoa  Iringa ni kati ya mikoa inayokabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa elimu jumuishi kubwa ikiwa miundombinu isiyo rafiki.

 

Alisema kuwa baadhi ya wazazi wanasema changamoto hizo ndiyo sababu kwa baadhi yao kushindwa kuwapeleka watoto shuleni.

 

Nae Leo sambala Katibu wa wa shirikala watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) mkoa wa Iringa  alisema miundombinu isiyo rafiki kwenye shule nyingi za msingi na sekondari ni kati ya vikwazo vinavyoikabili elimu hiyo mkoani hapo.

 

Alisema kama suala la miundombinu halitapewa uzito, watoto hao watashindwa kujifunza ipasavyo.

 

“Ni kweli shule zetu zinakabiliwa na miundombinu isiyo rafiki, hakuna vifaa vya kujifunzia hasa kwa walemavu wasioona, hapa hakuna kujifunza,” anasema na kuongeza;

 

Sambala alisema kuwa Walemavu wa kutoona wanahitaji vifaa maalum ambavyo sio kila shule inavyo, kwa hiyo huyu hatajifunza kama ataingia darasani na kukosa vifaa hivyo.” 

 

Kephason ni mwanafunzi mwenye ulemavu wa kuona alisema shule jumuishi anayosoma  bado ina changamoto za kimiundombinu  na kupelekea kuwa na ugumu kutoka sehemu moja hadi nyengine awapo kwenye  mazingira ya shule na kupelekea kukosa ari ya kuendelea na masomo kama wanafunzi wengine na kuitaka serikali kufanya jitihada madhubuti kurekebisha hili kwani kwa mwenendo huu wanafunzi wengi wenye ulemavu wanaamua kuacha shule ili kuepukana na changamoto za kimiundombinu wanazokutana nzao mashuleni kwani  huwaathiri kisaikolojia.

 

Alisema kuwa elimu jumuishi imepewa kipaumbele zaidi kuliko aina nyingine na inachukuliwa kama njia bora

 

Mwalimu wa shule ya msingi ambao inatoa elimu jumuishi, John Kijazi alisema kwa mfano  watoto wenye ulemavu wa miguu, wao wanakabiliwa na uhaba wa vibaiskeli, jambo linalowafanya washindwe kujifunza ipasavyo.ili mtoto mwenye ulemavu wa viungo apate elimu bora lazima awe na uhakika wa kutoka hatua moja hadi nyingine kwa baiskeli.

 

Kijazi alisema kuwa miundombinu kwa watoto wenye ulemavu bado ni shida wanahitaji madarasa, walimu wa kutosha, mazingira rafiki ili kupata elimu bora.

 

Alisema kuwa bado kuna changamoto kubwa hasa kutokana na kuwa na walimu wachache, madarasa na mitaala isiyo rafiki kwa wanafunzi viziwi. 

 

Kijazi alisema kuwa hili ni kundi lililosahaulika hivyo juhudi binafsi zinahitajika kwa wadau wote wa elimu kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora.

 

Christopher Hinju Afisa wa elimu maalum Iringa Hinju alisema kuwa Serikali imeahidi kuwa itawaajiri walimu zaidi wa kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye uziwi

 

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa elimu jumuishi kutoka shirika lisilo la kiserikali la  Iringa Development of youth disabled and children care (IDYDC) shirika lisilo la kiserikali  linalotekeleza mradi wa Inclusive Media Project  unaofadhiliwa na Internew Tanzania  katika mkoa wa Iringa kupitia Mratibu wa  mradi Reuben Magayane katika kikao cha kimkakati kilichohusisha wadau wa elimu na waandishi wa habari amesema lengo la mradi ni kutumia vyombo vya habari  kupaza sauti juu ya elimu jumuishi na kuibua maswala ya makundi maalumu na walemavu kupitia vyombo vya habari jambo ambalo limekuwa halipewi kipaumbele kwenye vyombo vya habari huku ikiiasa jitihada jumuishi kutoka kwa waandishi wa habari,jamii na serikai ili kufikia lengo la elimu kwani Msingi wa mafunzo mbalimbali katika jamii ni chachu ya kuondoa mawazo mgando juu ya watu wenye mahitaji maalumu kuwa hawawezi, 

 

Magayane alisema kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kutoa ushirikiano hitajika kwa watu wenye mahitaji maalumu hasa katika upande wa elimu.

 

Na kwa mujibu wa jarida ya Shirika la Kuhudumia watoto Duniani (Unicef) , kati ya watoto watano ni wawili tu wapo shuleni.Sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, inataka haki sawa kwa watu wenye ulemavu ikiwamo elimu, ajira, nafasi za uongozi na kuboresha miundombinu.

 

Hata hivyo, wengi wanakabiliana na miundombinu isiyorafiki ambayo ni kikwazo katika upataji wa elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.