Habari za Punde

Watendaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali wametakiwa kuwajibika ipasavyo ili kumaliza mrundikano wa Kesi za Udhalilishaji Nchini.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na watendaji mbali mbali za Serikali wanaoshughulikia masuala ya udhalilishaji  kilichofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa agizo hilo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji mbali mbali za  Serikali zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji  kilichofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.                                                                                         

 Mhe. Hemed ameeleza kuwa Taasisi  zinazosimamia Kesi hizo zina watendaji wenye ujuzi na uzoefu ambapo uwajibikaji wao utasaidia  kutokomeza Janga hilo Nchini.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Jamii ya wazanzibari ina Imani na Serikali yao ambapo kufikia mwisho kwa Kesi hizo kutasaidia Zanzibar kuwa Salama na yenye maendeleo.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed ameeleza kuwa kuchelewa kwa kesi hizo kunapelekea wananchi kukosa na Imani na Serikali yao hali ambayo Serikali ya Awamu ya Nane haifurahishwi na hali hiyo.

Mhe. Hemed amesema Serikali haifurahishwi kuona watuhumiwa wa Kesi za Udhalilishaji wamerundikana rumande bila ya kumaliza kesi zao ambazo ni za muda mrefu  ambapo ni kinyume na haki za kibinadamu.

"Nina uhakika kuna kesi zaidi ya miaka mitano hazijesha kama zipo jamii inavunjika moyo hili linapelekea jamii kutotoa ushahidi baadhi yao wakiamini hakuna kinachofanyika. Tuache tabia hiyo"

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwataka watendaji hao kutotumia kesi hizo kwa kumuonea mtu au kumpendelea yoyote bali watende haki kwa kusimamia Viapo walivyoapa  kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

"Wahusika wakiona Mtu anaonewa tusimamie apate haki yake tusimuonee mtu wala kumpendelea na isiwe kesi hizi ni sehemu ya kujipatia fedha"

Aidha Mhe. Hemed amewataka watendaji hao kuwa wawazi kwa  kueleza Changamoto zinazowakabili akitolea mfano uhaba wa rasilimali watu na vitendea kazi, magari ya kuwapeleka mahabusu na changamoto nyengine ili Serikali iweze kutatua Changamoto hizo.

Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Awadh Juma Haji ameeleza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na kuwasaka wahusika wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na mashahidi ambao wanakataa kufika mahakamani kutoa Ushahidi kwa makusudi au kwa muhali.

Aidha Kamishna Awadh ameeleza kuwa Jeshi la Polisi halifurahishwi na  tabia ya baadhi ya waathirika kujaribu kuweka mazingira kwa kumsaidia mlalamikiwa ambapo amewataka wananchi kutoa mashirikiano ya kutosha ili kumaliza janga hilo Nchini.

Nae Naibu Mrajis wa Mahkama kuu Zanzibar Salum Hassan Bakari ameeleza kuwa Mahkama imeweka Mikakati madhubuti ya kuungana na Rais Dkt Mwinyi kuhakikisha Janga la udhalilishaji linamaliza Nchini akitolea Mfano mashauri kusikilizwa kwa wakati pamoja kupitia Majalada kuona kesi zilizochukua muda mrefu ziweze kumalizwa.

Aidha Naibu Mrajis ameeleza kuwa Mahkama imeshatatua changamoto ya malipo kwa mashahidi hasa wataalamu ili waweze kutoa mashirikiano ya kutosha katika kuendesha mashauri ya udhalilishaji.

kikao kazi hicho kimewakutanisha wadau kutoa Jeshi la Polisi, Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wizara ya jamii, wazee, jinsia na watoto, wizara ya Afya

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

08/06/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.