Habari za Punde

WIMBO MSONDO NAMBA SITA

 
Na.Adeladius Makwega-BUJORA–MWANZA.

Juma moja limepita kuna kundi moja la mitandao ya kijamii niliona walinialika katika kundi hilo lenye wapenzi wa muziki wa zamani (ZILIPENDWA), mjadala ukiwa  juu ya muziki wa ala  wa Tanzania ambapo  nyimbo  kadhaa ambazo zililirekodiwa enzi za RTD zilijadiliwa kwa kina.

Katika mjadala huo wapo waliokuwa wakidai wao wanafahamu zaidi ya wengine, niliufuatilia kwa makini bila ya kuchangia lolote lile. Katika mjadala huo nilibaini kuwa katika Tanzania ya sasa imekuwa nadra mno kusikia muziki wa ala mpya umetolewa iwe kwa mwnamuziki binfasi au kundi la wana muziki hao.

Kama muziki wa ala upo na umerekodiwa kwa sasa basi ni katika vikundi vya vyombo vya ulinzi Jeshi la Polisi au Jeshi la wananchi pekee.Walio wengi Muziki wetu mara nyingi umekuwa ukitazamwa katika dhana ya nyimbo zenye maneno tu.

Swali ambalo linabaki je ni kwanini sasa muziki huo hautungwi sana kuliko ilivyokuwa awali?

Swali hili kwangu limenizidi kimo kabisa kulijibu, niliwatafuta wadau kadhaa wa utayarishaji na urekodiji wa muziki Tanzania waliofanya kazi hizo na wanamuzki wazamani. Majina matatu yalikuja akilini mwangu, Crisipin Lugongo, James Mhilu na Silvanus Haule, wote hao wakiwa wahandisi wa sauti(Sound Engineers) wa  RTD.

Silvanus Haule nilipomtafuta nilijulishwa kuwa alifariki dunia, kwa hiyo majina ya Crispin Lugongo na James Mhilu yalikuwa ndiyo majina yaliyosalia katika orodha yangu. Majibu yao wakisema kuwa sasa kuna uhaba wa watungaji wa muziki huo.

“Nyimbo hizo zote sikurekodi mimi, wakati huo walikuwepo wahandisi wengi wa sauti akiwamo John Ndumbaru, Gaundence Makunja,Onesmo Kirombo na Edmundi Mria miongoni mwao hao kila mmoja alifanya kazi hizo kwa nyakati tofauti tofauti wakiwa na Bendi ya NUTA JAZZ BAND-NJB na zingine nyingi.”

Nakumbuka mwaka 2010 nikiwa TBC taifa, niliwahi kuomba mkanda wenye nyimbo za ala za Msondo 1-6 wa NJB. Nilipoomba mkanda huo ulikuwa umeshakaa katika maktaba hiyo kwa miaka kama 37-40 nilikutana na kitu ambacho sikupata majibu.

Disemba 5, 1975 NJZ walikwenda RTD kurekodi nyimbo mbili wa kwanza ni AZIMIO LA TANU na wa pili ni MSONDO NAMBA 6.Ndiyo kusema Msombo nambari 1-5 zilirekodiwa awali kati ya mwaka 1960-1974.

Nilipoitazama kaseti hii kuliandikwa maandishi Dunia ya Mfanyakazi yaliyoandikwa kwa mkono.Kwa hoja hii niliona kuwa wimbo huo japokuwa ulikuwa muziki wa ala ulikuwa pia ni wimbo wenye maneno. Pembeni kulikuwa na maneno usicheze wimbo huu ni kiashiria cha kipindi.

Nilipowauliza wakutubi wa maktaba hii akiwamo Mzee Nanguka na Mama mmoja anayefahamika kama Neema walinijibu kuwa wimbo huo ulikuwa ni kiashiria cha kipindi cha Jioni Njema tangu miaka ya 1970 hadi kipindi hicho kilipobadilishwa kiashiria chake kilichokuwa kinaruka hewani kila siku jioni.

“Zile nyimbo zilikuwa muziki wa ala tu, kama muziki wa ala, hazikuwa na maneno, NJB walikuwa wanakuja wanarekodi nyimbo zao za maneno alafu wanarekodi wimbo wa ala wanaondoka.”

Jibu hili alitoa injinia Crispini Lugongo, maelezo haya ya iniinia Lugongo yalijibu swali hilo la jina la Dunia ya Mfanyakazi kuwa ni wimbo mwingine ulirekodiwa siku hiyo pia.

Huku NJB wakiwa na kikosi cha watu 16 akiwamo Abel Baltazar aliyepiga Solo Guitar, Said Mabela aliyepiga Solo Giitar na Trumpet, Abdalla alipiga Rhythm Guitar, Amed Omary naye alipiga  Rythm Guitar, Seleiman Mwanyiro alicheza Base Guitar, Josephy Lusungu alicheza Trumpet, Mnenge Ramadhani alipuliza Alto Saxophone, Juma Hassan  alipuliza Torner Saxophone, Juma Akida,Muhidin Maalimu na Hassan Bichuka walikuwa waimbaji, Mohammed Omary Tumba, Zahama, Seleiman Said na Hassan Bakari walikuwa mafundi mitambo, nayeaye Mabruki  Khalfani alipiga Drum.

Katika wimbo Msondo Namba 6 kwa kuwa ulikuwa muzki wa ala Juma Akida, Muhidin Maalimu na Hassan Bichuka waliokuwa waimbaji walikaa kimya tu.

Muziki wa ala wakati huo ulikuwa ni sehemu ya burudani iwe redioni na hata katika kumbi za starehe, hoja hiyo inaungwa mkono na injinia James Mhilu.

“Walikuwa kabla ya kuanza kuimba nyimbo zenye maneno ukumbini kwanza walipiga nyimbo zao za ala. NJB na baadaye JUWATA JAZZ BAND (JJB) walikuwa na mpiga Second Solo anaitwa Hamisi Kiza yeye ndiye aliyekuwa akitunga nyimbo zote za ala la Msondo.”

Injinia Mhilu anasema hta kurekodi muziki wao walifunidiswa na waswedeni na wengine kwenda nje ya nchi. Mimi nilikuwa narekodi nyimbo hizo studio kwa kurekodi vyombo vitupu alafu narekodi sauti tu ili kuondoa mwangi kwa kurekodi pamoja, baadaye ndiyo anazichanganya sauti na vyombo na kupata wimbo kamili.

Kwa mtindo huo RTD wanazo ala za muziki  nyingi sana za kila nyimbo alizorekodi  wakati huo zenye maneno lakini hilo halifahamiki na wengi isipokuwa yeye na wenzake wachache waliowahi kuzirekodi wanatambua na zote  zipo katika maktaba yao.

RTD (TBC Taifa sasa) walikuwa na studio kubwa mbili moja ya Dar es Salaam na nyingine ya Dodoma ambapo kazi hiyo ilifanyika.

Bendi za NJB, JJB na baadaye OTTU zilikuwa mali ya vyama vya wafanyakazi ndiyo kusema hata nyimbo hizo ni mali ya vyama hivyo. Hoja hiyo inakataliwa na maanjini hawa ambao sasa wamestaafu utumishi wa umma kwa kusema kuwa

“Bendi zote zilipokuwa zikienda RTD kurekodi walikuwa wakipatiwa malipo fulani. RTD waliwaambia kuwa nyimbo hizi zitatumika katika vipindi na pia viashiria vya vipindi na hata bendi ilipokwisha kupokea malipo ya RTD ndipo walirekodi, kwa hiyo nyimbo hizo ni mali ya RTD na siyo NJB, JJB au OTTU.” Injinia Lugongo.

Mwanakwetu upo?

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.