Habari za Punde

Dk.Mwinyi Ameipongeza Taasisi ya Milele kwa Juhudi Zake Kuiunga Mkono Serikali Katika Miradi Mbalimbali ya Maendeleo.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi wa Kijangwano na Birikau, wakati wa ziara yake kukagua ujenzi wa barabara yenye kilimota 4.5, inayotoka Kijangwani hadi Birikau Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Taasisi ya Milele kwa juhudi zake za kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kijangwani hadi Birikau yenye urefu wa kilomita 4.3 inayojengwa kiwango cha lami.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alileza kuwa asasi zisizo za Kiserikali ziko nyingi lakini Taasisi ya Milele imekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Serikali.

Alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikisaidia katika ujenzi wa skuli, nyumba, misikiti pamoja na miradi kadhaa ya maendeleo.

Aidha, Rais  Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari ukamilishaji wa ujenzi wa barabara hiyo fedha zake zimeshatiwa kwenye bajeti ya mwaka huu.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa hatua waliyoichukua ya kutotaka kulipwa fidia ya vipando vyao vilivyoathirika wakati wa ujenzi wa barabara hiyo.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed aliwaeleza wananchi kwamba katika mambo yaliyopangwa kufanywa kiswani pemba ni pamoja na kujenga jengo jipya la abiria pamoja na njia ya kurukia na kutulia ndege na kuweza kutua ndege kubwa.

Aliongeza kuwa bandari ya Mkoani nayo itajengwa ili iweze kupokea meli za makontena hatua ambayo itapunguza gharama kwa wananchi pamoja na ujenzi wa barabara ya Chake  Wete na Mkoani hadi Chake.

Afisa Mdhamini wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Ibrahim Saleh Juma alitumia futrsa hiyo kuipongeza Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation pamoja na Milele kwa pamoja kwa wazo lao la kusaidia ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wanaishi katika maeneo hayo.

Mapema Rais Dk. Mwinyi alikagua shughuli za wajasiriamali pamoja na kuwakabidhi wajasriamali bodaboda.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua tano zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wajasiriamali wanasaidiwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia katika kuwapatia mtaji, soko, elimu, kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao pamoja na zana za kufanyia kazi.

Rais Dk. Mwinyi  pia, aliweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya ya Chake huko Ole ambako alieleza jinsi alivyoridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa watendaji wa sekta ya umma kufanya kazi kwa bidii  katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwani tayari Serikali imeshawaongezea maslahi yao.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi la skuli ya Sekondari Pujini na kueleza jinsi Serikali ilivyodhamiria kujenga skuli za ghorofa kama hizo ili kupunguza changamoto ya uhaba wa madarasa.

Alieleza azma ya serikali ya kujenga na kuzifanyia ukarabati skuli zote za zamani ili ziweze kukidhi kusaidia katika kuondoa changamoto katika sekta hiyo ya elimu.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alitembelea mabwawa ya kufugia samaki huko Kibaridi Pujini na kuwaeleza wafugaji wa samaki kwamba serikali itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wanapatiwa vifaranga.

Aidha, Rais Dk.Mwinyi alieleza hatua zitakazochukiliwa katika kuhakikisha vikundi vyote vinapatiwa mitaji na kuiagiza Wizara husika kwuawekea mazingira maalum wafugaji hao.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano.

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.