Habari za Punde

MAJALIWA: SH BILIONI 54 KUJENGA MRADI WA MAJI RUANGWA/NACHINGWEA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa madarasa katika  Shule ya Msingi Ndandawale wilayani Ruangwa, Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Chimbila wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ndandawale wilayani Ruangwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasalimia baada ya kukagua ujenzi wa madarasa katika shule  yao ya Msingi akiwa katika ziara ya wilaya hiyo, Julai 4, 2022.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 54 kwa ajili ya kugharamia mradi wa maji wa Chiuwe utakaohudumia wilaya za Ruangwa na Nachingwea.

Ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Julai 4, 2022) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Mchenganyumba, Mbecha na Chimbila ‘B’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya ya Ruangwa.

Mheshimiwa Majaliwa alisema maeneo mengi ya wilaya hiyo maji yake ni ya chumvi, hivyo Serikali ilifanya utafiti na kubaini kuwa chanzo cha maji cha Chiuwe maji yake hayana chumvi na ni ya kutosha kuweza kuhudumia vijiji vya wilaya hiyo na wilaya jirani ya Nachingwea.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kitakachowezesha kutekelezwa kwa mradi huo ambao kukamilika kwake kutamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo.

Vilevile, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote kujiandaa kuhesabiwa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sensa na viongozi kwenye maeneo wanayoishi. Zoezi hilo limepangwa kufanyika nchini kote Agosti 23, 2022.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wa wilaya ya Ruangwa Mhandisi Lawrence Mapunda alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza itahusisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 21 vya wilaya ya Nachingwea.

Mhandisi Mapunda alisema ujenzi wa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 utakamilika mwaka 2025/2026. “Kwa sasa utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua ya manunuzi na unatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu kwa awamu zote.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza tatizo la upatikanaji maji wilayani Ruangwa kwa zaidi ya asilimia 80. Chanzo cha maji cha Chiuwe kilichopo Nyangao kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 15 kwa siku huku mahitaji ya wilaya ya Ruangwa kwa siku ni tani milioni tisa.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.