Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman Anayeshughulikia Fedha na Utawala Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisakimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman Anayeshughulikia Fedha na Utawala Mhe. Mohammed  Nasser Al  Wahaibi , alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 24-7-2022, akiongozana na Balozi wa Oman Nchini Tanzania Mhe. Saud Hilal Al Shidhani na Balozi Mdogo wa Oman anayefanyia Kazi zake Zanzibar Mhe. Said Salim Al Sinawi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman Anayeshughulikia Fedha na Utawala Mhe. Mohammed Nasser Al Wahaibi, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 24-7-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman Anayeshughukijia Fedha na Ytawala Mhe. Mohammed Nasser Al Wahaibi, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 24-7-2022, akiongozana na Balozi wa Oman Nchini Tanzania Mhe. Saud Hilal Al Shidhani  na Balozi Mdogo wa Oman anayefanyia Kazi zake Zanzibar Mhe. Said  Salim Al Sinawi.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi na kumueleza kwamba Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mazungumzo hayo yalifanyika leo Ikulu Zanzibar wakati Rais Dk. Mwinyi alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi akiwa amefuatana na ujumbe wake akiwemo Balozi wa Oman nchini Tanzania Saud Hilal Al Shidhani.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Katibu Mkuu Mohammed Nasser Al Wahaibi kwamba kwa kiasi kikubwa Oman imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya, elimu na mengineyo bila ya kusahau hatua ya nchi hiyo kusaidia ujenzi wa jengo la Beit al Jaib.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo kwa kutambua kwamba Oman ni mshirika mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano kwa sekta binafsi kati ya pande mbili ili kuweza kutoa fursa mbali mbali za maendeleo hasa ikizingatiwa umuhimu wa sekta hiyo katika maendeleo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake huku akipongeza hatua za nchi hiyo kuendelea kuziunga mkono juhudi hizo.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Oman inatambua uhusiano na ushirikiano wa kihistroa uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuziendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.

Katibu Mkuu Wizara Mohammed Nasser Al Wahaibi alisema kuwa nchi ya Oman kwa kupitia Balozi zake hapa nchini zitaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta zake za maendeleo.

Pia, alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika maendeleo jamabo ambalo limeweza ksuaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma uchumi na medneleo nchini Oman.

Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Fedha na Utawala Mohammed Nasser Al Wahaibi alizipongeza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alimpa salamu Rais Dk. Mwinyi zilizotoka kwa Sultan wa Oman Haitham bin Tariq Al Said ikiwa ni pamoja na kueleza namna nchi hiyo itakavyoendelea kuunga mkono vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya maendeleo ya Wazanzibari.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuendelea na ziara yake kisiwani Pemba hapo kesho (Julai 25,2022) ikiwa ni pamoja na kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo inayotekelezwa kwa fedha za ahuweni ya UVIKO -19.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.