Habari za Punde

DC Kusini aanza kazi asisitiza ushirikiano kutekeleza majukumu

 

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Rajab Yussuf Mkasaba amesisitiza umuhimu wa kuwepo mashirikiano katika kutekeleza majukumu yake kwa azma ya kuwatumikia wananchi ipasavyo na hatimae kufikia lengo lililokusudiwa.

Hayo aliyasema leo huko katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja iliyopo Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya makabidhiano ya Ofisi yaliyofanyika ofisini hapo kati yake na Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Marina JoelThomas ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kati katika Mkoa huo.

Katika maelezo yake Mkuu huyo mpya wa Wilaya alieleza kuwa mashirikiano ndio msingi mkubwa wa utendaji kazini kwani bila ya kuwepo mashirikiano ya pamoja hakuna maendeleo yatakayofikiwa.

Alieleza matarajio yake kwamba kuwepo mashirikiano ya pamoja kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa kazi hasa kwa umuhimu wa ofisi hiyo sambamba na kwenda na kasi ya maendeleo iliyokusudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa mbali ya kuwepo kwa mashirikiano suala la kuimarisha amani, umoja, utulivu na mshikamano nalo ni suala la lazima katika Wialaya hiyo kwa lengo la kuwatumikia wananchi.

Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo ya Kusini Unguja alieleza kwamba mashirikiano ya pamoja yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi  (CCM).

Aliongeza kuwa Rais Dk. Mwinyi ana maono makubwa katika kuwapelekea wananchi wake maendeleo hivyo, mashirikiano ya pamoja yatasaidia katika kufikia lengo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati ambaye alikuwa akikaimu Wilaya hiyo Marina Joel Thomas alimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya hiyo na kuwaomba viomgozi na watendaji wote wa Wilaya hiyo kumpa mashirikiano mabwa ili iwe rahisi katika kutekeleza majukumu yake.

Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kati alieleza mafanikio pamoja na changamoto zilizopo katika Wilaya hiyo na kusisitiza kwamba kwa mashirikiano ya pamoja anamatumaini makubwa kwamba ufumbuzi wa changamoto mbali mbali ziliopo utapatikana.

Nae Mwalimu Said Hamad Ramadhan kwa niaba ya Wazee wa Wilaya hiyo alimkaribisha Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Kusini Unguja na kumueleza kwamba kwa niaba ya wazee wote wa Wilaya hiyo wamempokea na wako tayari kufanyakazi nae pamoja na kushirikiana nae wakati wote.

Mwenyekiti  wa CCM Wilaya  Abdulazizi Hamad Ibrahim akitoa neno la ukaribisho kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kwa niaba ya chama hicho Wilaya, aliahidi kumpa ushirikiano mkubwa Mkuu wa Wilaya huyo mpya na kusisitiza kwamba juhudi za makusiudi zitachukuliwa katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa kwa vitendo.

Mapema Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mbaraka Omar Kasongo alimuahidi Mkuu wa Wilaya huyo mashirikiano makubwa ili Ofisi hiyo iweze kutekeleza kwa vitendo maono ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi katika kuwatumikia wananchi ambapo tayari ishara kubwa ya mafanikio na maendeleo zimeanza kuonekana.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja aliteuliwa Agosti 03 mwaka huu 2022 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi na kumuapisha mnamo Agosti 05,2022 katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar .

 

Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja,

Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.