Habari za Punde

Benki ya NMB yaahidi kuendelea kutoa mikopo kwa wawekezaji sekta ya nishati nchini

Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB Afred Shao akizungumza wakati wa Kongamano la Nishati lililofanyika Jijini Dar es Salaam.

Benki ya NMB imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kutoa mikopo kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa sekta ya nishati nchini kwa lengo  la  kusaidia ukuaji wa sekta hiyo.

Akichangia mada wakati wa Kongamano la Nishati lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, Alfred Shao, Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, alisema benki hiyo ina bidhaa nyingi za kifedha mahususi kusaidia wawekezaji katika sekta ya nishati chini.

Shao alisema benki hiyo ikiwa ni mshauri wa uwekezaji aliyeidhinishwa pia inatoa huduma za ushauri kwa wateja na pia wakati mwingine husaidia kutafuta mitaji kwa makampuni mapya.

“Sisi kama benki tunaelewa kuwa uwekezaji katika sekta ya nishati  unahitaji mitaji mikubwa. Tuna fedha za kutosha kutoa mikopo kwa wadau  kwenye sekta ya nishati.  Kwa sasa tunaweza kutoa mkopo wa mpaka milioni 300 kwa mtu mmoja,” alisema Shao.

Alisema benki hiyo pia imejenga ushirikiano mzuri na mashirika ya kifedha ya kimataifa kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) na ina mpango wa kuanzisha hati fungani za kijani.

"Tulifanikiwa kutoa Hati Fungani Maalum ‘NMB Jasiri Bond’ mwaka huu ambayo ilikuwa na mwitikio mzuri sana tunatarajia kutoa hati fungani ya kijani inayolenga sekta ya nishati jadidifu," alisema.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Exaud Kigahe wakati wa hafla hiyo alisema Serikali inatarajia kutumia fursa kwenye maeneo ambayo hayajatumika hasa katika nishati jadidifu yaani renewable energy na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kufanya kazi na sekta binafsi katika kukuza sekta hiyo.

Alisema Serikali tayari imeanza utekelezaji wa mkakati wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya kupunguza urasimu usio wa lazima miongoni mwa taasisi zake.

“Kwa nchi yetu haipo kwenye kiwango kizuri cha mazingira ya kufanya biashara. Tumepiga hatua kubwa kuweka mazingira mazuri ya biashara kama sehemu ya juhudi zetu za kuvutia wawekezaji zaidi nchini na hii itatusaidia kuongeza ushindani," alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.