STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 10 Agosti,2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Jumuiya ya
Ulaya (EU) kwa Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopata misaada kutoka
Jumuiya hiyo kwa ajili ya kuendeleza
miradi mbali mbali ya Maendeleo.
Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo alipozungumza
na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Jestas Abouk Nyamanga , aliefika Ikulu
Zanzibar kwa kujitambulisha pamoja na mazungumzo mafupi.
Amesema ni jambo jema kwa Zanzibar,
hususan kisiwa Cha Pemba kuwa miongoni
mwa maeneo ambapo miradi mbali mbali ya maendeleo itatekelezwa chini ya
Ufadhili wa EU hapa Tanzania, ikiwemo
mradi wa ‘kuboresha mtazamo wa Majiji’ (green City), ambao unakusudiwa
kutekelezwa katika miji mitatu ya Tanzania ya Tanga, Mwanza na Pemba.
Alisema tangu kuingia madarakani kwa
Serikali ya Awamu ya nane, yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa (GNU), kumekuwepo
dalili za EU kurejesha Uhusiano wake na Zanzibar kufuatia kuwepo kwa Demokrasia.
Aidha, Dk.Mwinyi alieleza kuwa Utalii
ni sekta kuu ya Uchumi wa Zanzibar, na kusema Zanzibar imejipanga kuimarisha
sekta hiyo baada ya kuathirika kutokana
na Ugonjwa wa Covid-19.
Alimtaka Balozi huyo kuendeleza
mazungumzo na mamalaka zinazosimamia
Utalii nchini Ubelgiji ili kufanikisha lengo la kuwepo safari za ndege za moja kutoka
Ubelgiji hadi Zanzibar na hivyo kuleta matumaini ya kuongeza ujio wa Watalii hapa nchini.
Akigusia suala la kuwepo fursa za Biashara
nchini Ubelgiji, Dk. Mwinyi alisema Diplomasia ya Uchumi inazingatia umuhimu wa
kuangalia fursa za biashara, hivyo akasema pamoja na kuwepo changamoto mbali
mbali katika utayarishaji wa Dagaa kwa wajasiriamali hapa nchini, Serikali itaishughulikia
changamoto hiyo hatimae fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo.
Alisema Zanzibar imekuwa
ikishughulikia miradi mbali mbali kwa
ajili ya maendeleo, hivyo kuwepo kwa
taasisi zinazotoa mikopo nafuu ni jambo jema
na kubainisha namna Serikali itazingatia namna itakavyoweza kupata mikopo hiyo kupitia mashirika hayo ya Fedha
yaliopo EU.
Aidha, alisema Zanzibar itashukuru
kupata fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu kupitia sekta ya
uchumi wa Buluu.
Mapema Balozi wa Jamhuri ya Muuungano
wa Tanzania nchini Ubelgiji, ambapo pia anaiwakilisha Tanzania nchini
Luxenbourg na Jumuiya Umoja wa Ulaya (EU Jestas Abouk Nyamanga amesema kuanza
kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Ubelgiji na Zanzibar kuanzia mwezi
Oktoba mwaka huu, kutaongeza idadi ya
Watalii watakaozuru nchini.
Alisema mawasiliano yamefanyika kuona
kunakuwepo usafiri wa ndege ya moja kwa
moja kati ya Ubelgiji – Zanzibar kwa
wastani wa mara mbili kwa wiki na hivyo kuongeza idadi ya ujio wa Watalii baada
ya kuathirika kutokana na Ugonjwa wa Covid -19, ambapo kabla ya ugonjwa huo
wastani wa watalii 16,000 walikuwaa
wakizuru nchini kila mwaka.
Alisema katika mazingira ya sasa
Watalii kutoka nchi hiyo hutumia Shirika la Ndege la Qatar, jambo ambalo lina
changamoto mbali mbali.
Aidha, alisema nchi hiyo ina fursa
mbali mbali za msomo ya juu, hususan katika kiwango cha Master na PHD, hivyo
akatoa wito kwa Vyuo vikuu vya Zanzibar,
ikiwemo SUZA pamoaj na wananchi wengine wenye uwezo kuhamasika ili
kutumia fursa ziliopo.
Balozi Nyamanga alisema mahusiano
kati ya Tanzania na Ubelgiji yameimarika na kubainisha fursa kadhaa za
kibiashara, ambapo Tanzania inaweza
kufanya, ikiwemo kuuza minofu ya samaki, dagaaa, mbogamboga, mchele pamoja na
viungo vya aina mbali mbali.
Alisema Zanzibar inaweza kunufaika na
fursa hiyo kupitia uuzaji wa Dagaa, mkazo ukiwekwa katika utayarishaji na
uhifadhi bora wa dagaa hilo ili kuliongezea thamani, pamoja na usafirishaji wa viungo ikiwemo Pilipili.
Kuhusiana na Uwekezaji, Balozi
Nyamanga alisema Luxembourg ni kituo
kikuu cha Mashirika ya Fedha pamoja na
Mabenki , huku akibainisha kuwepo Kampuni zinazoonyesha nia ya kutoa mikopo
nafuu kwa Zanzibar, hivyo akaiomba Serikali kubainisha maeneo yanayoweza
kutumika.
Akizungumzia mahusiano ya Tanzania na
Jumuiya Umoja wa Ulaya, Balozi Nyamanga alisema kuwa ni mazuri, ambapo EU imekwua
ikiendelea kutoa misaada, hususan ya kifedha kwa Tanzania.
Alisema EU imetenga kiasi cha Euro
Milioni 554 kwa Tanzania ili kuiwezesha kuingia katika soko la Ulaya pamoja na
Euro Milioni kumi kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa Asali ya Nyuki.
Aliitaja mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora, Dodoma na Pemba kuwa itanufaika na msaada huo, lengo likiwa ni
kuzalisha asali yenye viwango .
Aidha, alieleza kuwa katika kipindi
cha mwaka 2021 – 2027 EU imeahidi kusaidia Tanzania kiasi cha Euro Milioni 425,
ambapo Euro Milioni 703 zimelengwa katika uboreshaji wa mitazamo ya Majiji
(green city) katika miji mitatu ya Tanga, Mwanza pamoja na Pemba.
Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili
ya kuimarisha miundo mbinu pamoja na masoko katika miji hiyo.
Aidha, Balozi huyo aliishukuru
Serikali kwa kutilia mkazo uimarishaji
wa sekta ya Uchumi wa Buluu, akibainisha kiasi cha Euro Milioni 140
zilizotengwa na Jumuiya hiyo kwa ajili ya uimarishaji wa Uchumi wa Buluu ambapo
miongoni mwa matumizi yake yatahusisha mikopo kupitia Sekta binafsi.
WAKATI HUO HUO; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi alikuwa na mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania
Shibu Mamo Kedida.
Katika mazungumzo hayo yaliofanyika
Ikulu Zanzibar viongozi hao
walizungumzia haja ya kuendeleeza mahusiano na mashirikiano ya kihistoria
kati ya Zanzibar na Ethiopia katika njanja mbali mbali kwa maslahi ya Mataifa hayo na wananchi wake.
Miongoni mwa maeneo ya mashirikiano
yaliogusiwa ni pamoja na Utalii, Michezo, utamaduni, masuala ya Anga pamoja na
elimu.
Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment