Habari za Punde

Sensa 2022: Wananchi watakiwa kutoa ushirkiano

 Na Mwashungi Tahir -Maelezo  

 

Wananchi wametakiwa  kutoa ushirikiano katika kutoa takwimu sahihi kwa makarani wa sensa watakapo fika kwenye kaya zao ili lengo Liweze kutimia

 

Hayo yamesemwa na masheha wa shehia mbalimbali za Unguja  walipotembelewa na kikosi cha uhamasishaji wakati wakipatiwa mafunzo ikiwa ni muendelezo wa ziara zao za kutoa taaluma juu ya zoezi la sensa.

 

Wamesema,  wananchi watakapotoa taarifa kwa usahihi, wataisaidia serikali kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo  nchini.

 

Wamesema  taarifa hizo sahihi ndizo zitakazowezesha kupatikana kwa  masuala ya afya, elimu na miundombinu mbalimbali kama vile barabara sambamba na taarifa za kaya juu ya  watu wenye mahitaji maalumu.

 

Aidha, waliwatoa hofu  wananchi kwamba  taarifa watakazozitoa kwa makarani  zitakuwa  siri kwa ajili ya matumizi ya kitakwimu pekee.

 

Masheha hao pia  wameahidi kuifanyia kazi elimu waliyopewa kuhusu sensa na kwamba watakuwa  mabalozi katika kuwafikishia  wananchi na  kufikia lengo lililokusudiwa.

 

Kwa upande wa Waratibu wa mafunzo hayo ya masheha wamewasihi  kwamba kuhakikisha kila mwananchi anashiriki katika sensa kwa maendeleo endelevu ya taifa.

 Hata hivyo  Waratibu hao wamewaomba makarani  ambao watakaopatiwa jukumu hilo kukusanya taarifa kwa umakini  wakati wa mchakato huo kwani takwimu hizo ndiyo dira ya maendeleo.

 

Nae  Ofisa Habari Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Sofia Abdalla Ali,  amewaomba masheha hao kuyafanyia kazi  mafunzo hayo kwa lengo la kurahisisha majukumu kwa makarani wataofika kwenye kaya zao. Na amewataka kutoa mashirikiano kwa watendaji wa sensa watakapo fika kwenye shehia zao.

 

Vituo vilivyofikiwa na kikosi kazi hicho ni pamoja na Rahaleo, Regezamwendo, Dunga Kiembeni,  Charawe na Ukongoroni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.