Habari za Punde

Serikali kuhakikisha inasaidia upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano kwa Jeshi la Polisi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Kamishna wa Polisi Zanzibar. Hamad Khamis Hamad, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 4-8-2022, alipofika kujitambulisha.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kijitambulisha, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 4-8-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha inasaidia upatikanaji wa usafiri  pamoja na vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya Jeshi la Polisi Zanzibar ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Kamishna  mpya wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad, aliefika kujitambulisha.

Amesema pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na dhima ya moja kwa moja  kushughulikia masuala ya Usafiri na mawasiliano kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifanyia kazi changamoto ya upungufu wa magari  pamoja na vifaa vya Mawasiliano  inayolikabili Jeshi hilo ili liweze  kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na uongozi wa Jeshi hilo, huku akimpongeza Kamishna huyo kwa uteuzi huo.

Aidha, alimpongeza Kamishna Hamad kwa kukabidhiwa jukumu hilo, ikizingatiwa uzoefu wa kutosha alionao pamoja na na kuifahamu vyema Zanzibar katika masuala mbali mbali, yakiwemo ya kiuhalifu.

Nae, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad alimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi kuangalia uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa Usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano pale hali itakaporuhusu, ili kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza vyema majukumu yake ya kukabiliana na uhalifu.

Alisema Jeshi la Polisi Zanzibar, kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi Tanzania, linakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya usafiri na upungufu wa vifaa, hususan  vya mawasiliano.

Alisema upatikianaji wa vifaa hivyo ni muhimu katika kukabiliana na makosa mbali mbali, akibainisha huwazesha askari kufika maeneo ya matukio wa wakati muafaka.

Alisema katika kipindi hiki Uongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar unaendelea kushughulikia mradi wa Ujenzi wa majengo mbali mbali, ikiwemo nyumba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, kituo cha Polisi Mkokotoni pamoja na ukarabati wa majengo ya Polisi Ziwani Unguja.

Aidha, CP Hamad alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri hya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa uteuzi wake na kubainisha faraja kubwa aliyonayo kutokana  uteuzi huo, huku akisiistiza azma yake ya kushirikiana kikamilifu na taasisi na Vikosi vya SMZ katika kukabiliana na uhalifu nchini.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.