Habari za Punde

TAMWA ZNZ yafanya mkutano Pemba na asasi za kiraia

Wadau wa asasi za kiraia wakiendelea na mkutano wa asasi za kiraia kisiwani Pemba uliolenga kujadili mbinu bora za ushawishi na utetezi katika ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.
Mratibu wa TAMWA-ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akiwasilisha mada wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said akizungumza wakati wa mkutano huo.

ASASI za kiraia kisiwani Pemba zimeeleza kuwa kuwepo kwa mpango na mkakati wa pamoja wa ufuatiliaji wa rasirimali za umma katika jamii utasaidia kuongeza uwajibikaji wa taasisi za umma katika kusimamia rasilimali hizo kwa maendeleo ya nchi.

Walisema hayo wakati wa mkutano wa asasi za kiraia kisiwani humo uliolenga kujadili mbinu bora za ushawishi na utetezi katika ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi.

Wakizungumza katika mkutano huo ulionadaliwa na Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), walieleza kuwepo kwa mfumo huo utasaidia kuongeza uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuondosha vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kwenye uongozi.

Akizungumza katika mkutano huo ambao ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi kwa ufadhili wa ubalozi wa Norway, Omar Khamis, alihimiza kuwepo kwa mpango wa pamoja wa ushawishi na utetezi kwa asasi za kiraia ili kusaidia kukabili kwa pamoja changamoto zinazokwaza wanawake kupata haki zao.

Alieleza, “suala la ushawishi na utetezi kwenye ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi katika jamii tunaweza kulifanikisha kwa kuweka mkakati wa pamoja ambao utatusaidia kujua changamoto na kuzitaftia ufumbuzi kwa pamoja kuliko kila taasisi kusimama kivyake.”

kwa upande wake Sifuni kutoka Jumuiya ya Mwamvuli wa Asasi za kiraia Pemba (PACSO), alieleza mjadala huo umefungua ukurasa mpya kwa asasi za kiraia kuwa na uwezo wa kufuatilia na kuiwezesha jamii kutambua rasilimali zote ambazo ni muhimu kwa maendeleo yao.

“Wengi tulikuwa hatuujui mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya umma (PETS) lakini baada ya taaluma hii tutaitumia kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kusaidia jamii kuwa na ufahamu wa kutosha na hatimae kuondokana na urasimu wa rasilimali za umma ambazo hupelekea kuwakosesha wanajamii haki zao za msingi,” alieleza Stara.

Akiwasilisha mada ya mfumo bora wa utetezi na ufuatiliaji wa matumizi ya umma, Muhammad Nabil Omar, alifahamisha kuwa uwepo wa mfumo huo katika jamii huimarisha uwezo wa Wananchi katika kusimamia rasilimali zao na kufanya maamuzi sahihi Ili ziweze kutumika kikamilifu kwa maslahi ya jamii nzima.

Nae mratibu wa TAMWA-ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alihimiza asasi za kiraia kuongeza jitihada za kutambua mbinu muhimu za uchambuzi wa matatizo ya kijamii hasa za uongozi kwa wanawake ili ziwawezeshe kuandaa mipango sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kushirikiana na  jamii husika. 

"Kuna umuhimu mkubwa sana kwa asasi za kiraia kutambua mbinu muhimu za uchambuzi wa matatizo ya kijamii katika ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya uongozi, na hii itatusaidia kujua ukubwa, udogo, uzito, sababu na madhara yake katika jamii," Fat-hiya Mussa Said, mratibu TAMWA-ZNZ ofisi ya Pemba. 

Mapema mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, akizumza kwenye mkutno huo alieleza kuwa jamii ina haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika upatikanaji wa haki kwenye matumizi ya rasilimali za umma Ili kuweza kufikia malengo ya kuijenga nchi kwa pamoja.

Mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi (SWIL) unaendelea kutekelezwa Zanzibar na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), ufadhili wa ubalozi wa Norway, Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.