Na Ally Mohammed, OMPR
Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali
wametakiwa kusimamia ipasavyo watendaji walio chini yao na kutatua changamoto
zilizopo ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Agizo hilo katika Kikao Kazi kilichowakutanisha Makatibu Wakuu na manaibu Katibu wakuu wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi kilichofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Amesema Makatibu Wakuu ndio Watendaji Wakuu wa Serikali hivyo ni vyema kusimamia ipasavyo ukusanyaji na utumiaji wa Fedha za Serikali kwa Maslahi ya Umma.
Aidha Mhe. Hemed amewataka Makatibu Wakuu kusimamia Watumishi na kufuata utaratibu uliowekwa Kisheria kwa Watumishi na kuchukua hatua Stahiki hasa kwenye Vitengo vya Manunuzi na Wahasibu ili kuhakikisha Fedha za Serikali hazipotei na kuishia Mikononi mwa wachache.
Pia Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar amewataka Makatibu Wakuu hao kusimamia ipasavyo ukusanyaji
wa Mapato kwa Taasisi zao ili Serikali iweze kufikia Malengo iliyojipangia kwenye
Bajeti ya Serikali na kufanya mambo yake ya kimaendeleo kwa Wananchi wake kwani
ukusanyaji wa Mapato kwa sasa bado hairidhishi.
Mhe. Hemed amewataka Watendaji hao kuacha Muhali
kwa watendaji walio chini yao na kutomuonea yoyote bali kila Katibu Mkuu afuate
Wajibu wake na kuwataka kufuata Sheria iliyopo kwa Watumishi Serikalini na
kuamua kwa mujibu wa Sheria hizo.
Akigusia Suala la Nidhamu Serikalini Mhe. Hemed amewataka Makatibu Wakuu hao kwenda kusimamia Watendaji ambao hawawajibiki ipasavyo na kuwatolea Taarifa za haraka wale wote ambao hawapo kwenye Mamlaka zao ili Serikali iweze kuchukua hatua na wale ambao wapo kwenye Mamlaka zao ni lazima wawachukulie hatua stahiki kulingana na Sheria ya Utumishi inavyosema.
“Kuna Watumishi hawaji kazini, kuna
watumishi wanapokea pesa bila ya kufanya kazi ya aina yeyote kuna watumishi
wasiokuwa na nidhamu chukuweni hatua na sio kila mtumishi
anaeharibu munamrejesha utumishi bila ya maelezo yeyote, chukueni hatua”
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka watendaji hao kuondosha Malalamiko yaliyopo kwa Watumishi wao na kusimamia haki za wafanyakazi ili kuleta ufanisi mkubwa wa kazi
“Ni lazima Wakurugenzi Utumishi kukaa na wafanyakazi wao kuwapa elimu na kuwasikiliza shida zao na kuweza kuzitafutia ufumbuzi stahiki ili na wao waone kuwa serikali inawajali”
Mhe. Hemed amewataka Makatibu Wakuu kuongeza ushirikiano na kuimarisha Mawasiliano baina yao na Watendaji wa chini ili kuimarisha utendaji wa kazi Serikalini.
Akigusia suala la ajira zilizotangazwa hivi karibuni Mhe, Hemed amemtaka Katibu Mkuu Utumishi wa Umma kukamilisha mchakato huo wa kuwafatilia walioomba nafasi hizo za walimu na madaktari ili kuondosha chanagamoto ambapo serikali imepanga kuwaondoshea wananchi changamoto zote zinazowakabili ikiwemo skuli na hospitali.
Pia ameitaka Wizara ya Afya kuajiri madaktari wataalamu ili kuweza kufanya kazi za kitaalamu kwenye mahospitali ambayo yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni
No comments:
Post a Comment