Habari za Punde

WHO WAKUTANA NA WATENDAJI WA AFYA ZANZIBAR

Naibu waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis hafidh akizungumza na wajumbe wakati akifunga  mkutano wa kukagua utekelezaji wa miezi sita wa Mpango Kazi wa Pamoja wa Mwaka 2022 Kati ya shirika la Afya Duniani  (WHO) na Wizara ya Afya  Zanzibar huko hoteli ya Verde Mtoni. 
Mwakilishi mkaazi wa shirika la Afya Duniani WHO Dkt. Andemichael Ghirmay akizungumza wakati wa mkutano wa kukagua utekelezaji wa miezi sita wa mpango kazi wa pamoja wa mwaka 2022 Kati ya shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya Zanzibar.
Wajumbe wa mkutano wa kukagua utekelezaji wa miezi sita wa mpango kazi wa pamoja Kati ya shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya  wakifuatilia mkutano huo huko hotel ya Verde Mtoni Zanzibar.

PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR

Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar                   26/8/2022

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amesema  Wizara ya afya ina jukumu la kutoa huduma bora za afya Nchini kwa kulinda na kutibu ili kupunguza madhara mbalimbali yatokanayo  na maradhi katika jamii.

Ameyasema hayo huko Verde Mtoni katika mkutano wa pamoja kati ya WHO na Wizara ya Afya wa mapitio ya kukagua utekelezaji wa mpango kazi wa miezi sita wa mwaka 2022.

Amesema Mkutano huo ni muhimu katika kufuatilia, kutathmini na kujifunza kwa ajili ya kuboresha Utekelezaji wa mpango kazi wa pamoja kwa kuboresha sekta ya afya.

“Ninawahimiza Washirika wengine wa Maendeleo kufanya hivyo,kwani natarajia wakati ujao itakuwa mipango ya pamoja kati yetu na Washirika wa Maendeleo katika Afya itakua mizuri Zaidi,”naibu Waziri alisema.

Aidha amefahamisha kuwa Zanzibar ina changamoto ya vifaa vya mama na mtoto hivyo kufanyika kwa mkutano huo kutasaidia kupatiwa misada Zaidi na kupunguza vifo vya mama na mtoto  vinavyojitokeza  mara kwa mara katika jamii.

“Serikali yetu inashukuru kwa misaada mbalimbali ya Washirika wa Maendeleo inayopelekea kufikia malengo hayo, hivyo  kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru nyote kwa misaada yenu mnayotupatia,”alisema.

Nae Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani WHO Zanzibar Dr Andemichael Ghirmay amesema uhusiano uliopo kati ya Wizara ya Afya  na Shirika hilo wa kimaendeleo katika sekta ya afya umepelekea kuimarisha mipango ya kufuatilia, kusimamia na kutathmini uwajibikaji wa matumizi ya vifaa vya matibabu na kupata huduma bora .

Nao washiriki wa mkutano huo wamesema kuwa wao  ndio wenye dhamana ya wagonjwa wanaopata huduma, hivyo watajiitahidi kuhakikisha kua wanatoa huduma bora zitakazoimarisha  afya za Wananchi  .

Aidha wamefahamisha kuwa kupitia mashirikaino ya pamoja kati yao na Shirika la Afya Duniani WHO watahakikisha wanapunguza vifo vya  mama wajawazito pamoja na wazanzibar kunufaika kupitia huduma hiyo.

Mkutano huo wa siku mbili uliwashirikisha watendaji mbalimbali wa Afya kutoka Unguja na Pemba wakishirikiana na watendaji wa Shirika la Afya Duniani WHO .   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.