Habari za Punde

Mhe Hemed: Simamieni vyema ukusanyaji wa mapato

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na watendaji wakuu wa Serikali wanaofanyia kazi Pemba kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Makonyo- Wawi leo

Sehemu ya watendaji wakuu wa Serikali wanaofanyia kazi Pemba wakimsikiliza 
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Makonyo- Wawi leo


NA Ally Mohammed, OMPR

Watendaji wakuu wa taasisis za serikali Pemba wametakiwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato na matumizi mazuri ya fedha za serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa agizo hilo katika kikao kazi kilichowakutanisha wakuu wa mikoa, wilaya, maafisa wadhamini makatibu tawala na viongozi wengine wa serikali ya mapinduzi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha  makonyo Wawi chake chake Pemba.

Amesema kuwa viongozi hao ndio watendaji wakuu wa serikali kwa kisiwa cha pemba hivyo ni vyema kusimamia ipasavyo ukusanywaji na matumizi ya fedha za serikali kwa maslahi ya taifa.

Aidha makamu wa pili amewataka watendaji wao kuacha muhali kwenye ukusanyaji wa mapato kwani serikali inahitaji fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mhe.hemed amewataka watendaji hao kila mmoja kwenye maeneo yake kutoa elimu juu ya utumiaji wa mashine za elektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ili kuongezeka kwa pato la taifa.

Sambamba na hayo makamu wa pili wa rais amewataka wakurugenzi halmashauri na manispaa kubadilika kwenye usimamizi wa miradi.

Akigusia suala la nidhamu kwa viongozi na wafanyakazi makamu wa pili wa rais amesema kuwa ni vyema viongozi kuwasimamia watendaji walio chini yao ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi,

“Kuna watu hawaji kazini, kuna watu wanaondoka bila mda kufika, hawawajibiki vizuri kazini na wengine wanatumia majina ya viongozi kujinufaisha wao wenyewe viongozi chukueni hatua” amesema

Sambamba na hayo makamu wa pili wa rais amewaagiza maafisa utumishi kukaa na watendaji wao pamoja na kuwapa elimu ili kujua haki na wajibu wao kwa mujibu wa  sheria  ya utumishi wa umma namba 2 ya mwaka 2011 na kanuni zake ya mwaka 2014.

“fateni utaratibu na sheria za utumishi zinavyosema kwa watendaji walio chini yenu, asionewe mtu, asidhulumiwe mtu lakini chukueni hatua kisheria” amesema

Akizungumza kwa niaba ya viongozi na watengaji wakuu wa taasisi wanofanyia kazi Pemba mkuu wa mkoa wa kusini Pemba mhe. Matar Zahor Masoud amemuahidi makamu wa pili wa rais wa Zanzibar kuyasimamia yele yote ambayo amewaagiza kwa maslahi ya taifa.

Mhe. Matar amewataka viongozi wenzake kuacha matabaka katika utendaji wa kazi na kuongeza ushirikiano baina yao ili kuleta ufanisi mzuri katika kazi za kuwahudumia wananchi wa Zanzibar na watanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.