Habari za Punde

Wizara ya Fedha na Mipango Yafanyia Kazi Maelekezo ya Kupitia Upya Tozo za Miamala ya Kielektroniki

Na Benny Mwaipaja, Sirari, Tarime. 

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imepokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi CCM kuhusu kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu gharama za tozo za miamala ya kielektroniki ili kuleta unafuu wa wananchi.
 
Dkt. Nchemba alisema hayo kwa nyakati tofauti Wilayani Tarime mkoani Mara alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea mpaka wa Tanzania na Kenya katika mji wa Sirari na kuzungumza na wananchi, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA.
 
Alisema kuwa wataalam wa Wizara yake wanayafanyia kazi maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Mhe. Rais, Chama Tawala pamoja na maoni ya wananchi kuhusu jambo hilo na kuahidi kuwa muda si mrefu Serikali itakuja na majawabu baada ya kufanya marekebisho kadhaa ili kuleta unafuu.
 
Dkt. Nchemba alisema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha ukusanyaji wa mapato kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaenda sambamba na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka miundombinu wezeshi inayolenga kuibua wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa na hatimaye kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
 
“Serikali imepokea maoni ya Watanzania wakati wa kutekeleza nia hii njema ya Serikali kwa wananchi wake na kwa hiyo baada ya kupokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuyazingatia maoni ya wananchi yanayoendelea kutolewa, tunalifanyia kazi suala hilo na punde tutaleta majawabu” Alisema Dkt. Nchemba huku akishangiliwa na wananchi wa Sirari waliokusanyika kumsikiliza.
 
Alisema kuwa Serikali inahitaji Fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati pamoja na miradi mingine ya huduma za jamii ambayo pia inahitaji fedha ndo maana kuna kugusana gusana kwa wale wenye unafuu ili kushiriki kuchangia maendeleo hayo.
 
Aliitaja baadhi ya miradi ambayo haiwezi kusimama kwa kukosa fedha ikiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 6, Mradi wa Reli ya Kisasa-SGR unaogharimu zaidi ya sh. trilioni 23, upanuzi wa bandari, miradi ya TARURA, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, mradi wa elimu bila malipo, ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na nyumba za walimu, na ujenzi wa vyuo vya ufundi. 

Aidha, alisema shughuli zingine muhimu ambazo haziwezi kusimama ni ulipaji wa mishahara kwa watumishi, kugharamia miradi ya kilimo ikiwemo utoaji ruzuku kwenye mbolea, utoaji wa ruzuku ya mafuta ili kukabiliana na mfumko wa bei, na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ambayo inahitaji fedha nyingi.
 
Aliwasihi watanzania kuendelea kuiunga mkono Serikali yao na kumwombea afya njema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwani ana nia njema ya kuharakisha maendeleo ya wananchi na amefanya hivyo kwa vitendo katika kipindi kifupi alichoshika madaraka ya nchi ambapo miradi mbalimbali ya kimkakati na ya kijamii imetekelezwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea kabla yake.
 
Alitolea mfano wa baadhi ya miradi inayokusudiwa kutumia fedha zitakazopatikana kwenye tozo kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo elfu 17 kabla ya Januari, 2023 pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi-VETA katika wilaya 72 ambazo hazina vyuo hivyo ambapo jumla ya sh. bilioni 200 zitatumika kujenga vyuo hivyo.
 
Kuhusu mazingira ya ufanyaji biashara katika mpaka wa Sirari na mkoa wa Mara kwa ujumla, Dkt. Nchemba aliiagiza TRA kuhakikisha kuwa inafanyakazi yake ya kukusanya kodi bila kuathiri biashara za wananchi na kuacha kutumia mabavu kukusanya kodi hizo. 

Aidha, aliwasihi wananchi kushiriki katika maendeleo ya taifa lao kwa kulipa kodi kwa hiari na kuwafichua wafanyabiashara wasio waaminifu wanaofanya magendo na hivyo kuikosesha serikali mapato na hivyo kuathiri mwenendo wa uchumi kwa kuleta ushindani usio sawa.
 
Aliahidi kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali za kodi zinazokwaza ukuaji wa biashara nchini ili kuifanya sekta hiyo ya biashara iweze kukua, kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi.
 
Kwa upande wa wafanyabiashara, Dkt. Nchemba aliwataka kuacha kufanya biashara za magendo mipakani kwani Serikali haiwezi kuhalalisha biashara hiyo.
 
Awali wabunge wa Mkoa wa Mara, wakiwemo Mbunge wa Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara, Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mara Mhe. Ghati Chomete, Mbunge wa Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki na Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe. Dkt. Jeremiah Amsabi, waliwasilisha kero za wananchi wa mkoa wa Mara ikiwemo mahusiano duni baina ya Askari, Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA hali waliyosema inakwaza ustawi wa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo hususan wanaoishi katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Sirari.
 
Miongoni mwa changamoto hizo ni kukamatwa kwa wananchi wakiwa na bidhaa wanazonunua nchini Kenya kwa bei nafuu ikilinganishwa na bei ya nyumbani ikiwemo saruji, mabati, sukari, mbolea na baadhi ya bidhaa nyingine ndogondogo ambazo wananchi wanazipata kutoka Kenya lakini wakiziingiza Tanzania, hata kama ni bati kumi au mifuko miwili ya Saruji, wanakamatwa.
 
Akiwa ameambatana na Kamishna wa Idara ya Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alitembelea Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Sirari na kuzungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA katika mpaka huo wa Tanzania na Kenya.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.