Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Shein Kuongoza Kikao Maalum cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein akiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kilichofanyika katika ukumbi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Unguja Wilaya ya Mjini na (kulia) Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla. 

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar leo kimefanya Kikao chake Maalum kikiwa ni miongoni mwa mwendelezo wa Vikao vyake vya kuwajadili wanachama wake walioomba kuteuliuwa kugombea nafasi za uongozi kwa ngazi za Mikoa na Taifa.

 

Kikao hicho kimeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya CCM,Kisiwandui Zanzibar.

 

Pamoja na mambo mengine Kikao hicho kimepokea na kujadili Mapendekezo ya Wana CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Wenyeviti wa CCM wa Mikoa ya Zanzibar kichama na Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa ngazi hiyo.

 

Nafasi nyingine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya UWT,Wazazi na UVCCM Taifa, Makamu Wenyeviti wa Jumuiya hizo,Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa nafasi mbili (2) kwa kila jumuiya ya Chama,Wajumbe wa Baraza Kuu Taifa,Wenyeviti wa UWT,Wazazi na UVCCM ngazi za Mikoa Kichama pamoja na Wajumbe wa kuwakilisha Jumuiya nyingine ngazi ya Taifa.

 

Aidha katika kuimarisha mfumo imara wa Demokrasia ndani ya Chama na Jumiya zake kupitia mchakato wa uchaguzi wa CCM wa mwaka 2022 tayari baadhi ya ngazi zimekamilsisha uchaguzi huo zikiwemo Mashina,Matawi,Wadi, Majimbo na Wilaya kwa Chama na Jumuiya zake.

 

Pamoja na hayo CCM ilitoa uhuru na uwazi kwa wanachama kuchukua fomu ya kugombea nafasi hizo kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na Chama.

 

Katika kikao hicho  Viongozi mbali mbali walioudhuria  ni pamoja Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

 

Wengine ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeil Ali Maulid pamoja na Wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.