Habari za Punde

Mhe Othman: Pitieni mfumo wa ukusanyaji wa mapato nchini kuongeza ufanisi

 


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa Bodi ya Mapato  Zanzibar (ZRB),  kuangalia pengo la Kisera katika mfumo wa ukusanyaji mapato nchini na kuufanyia mageuzi  sahihi ili kuongeza ufanisi na kukuza kiwango cha mapato Zanzibar.

Mhe. Othman ameyasema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, alipozungumza na Kamshina wa ZRB ndugu Ramadhani Juma Mwenda aliyefika ofisini kwa Makamu kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala mbali mbali yanaoweza kuchangia ufanisi na kukuza kiwango cha mapato yanayokusanywa Zanzibar.

Mhe. Makamu amefahamisha kwamba yapo maeneo mengi ya Mapato ambayo yanaweza kufanyiwa mageuzi zaidi ya  kisera na kisheria jambo litakalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa kupitia vyanzo tofauti vilivyopo nchini.

Aidha  Mhe. Othman amesema hatua ya hiyo pia itasaidia sana kuwepo vyanzo zaidi vya mapato yatakayoweza kuchangia kasi zaidi ya maendeleo ya nchi kutokana na kiwango kikubwa zaidi cha mapato kuweza kukusanywa.

Mhe. Othman amesema kwamba yapo maeneo mengi ambayo baada ya mageuzi ya kisera na kisheria kufanyika yataweza kutumika kukusanyia mapato zaidi na nchi ikaweza kuendelea kwa kasi kubwa  kwa kiwangpo cha mapato yatakayopatikana kuliko ilivyo sasa.

Pia Mhe. Othman amesema kwamba kuna haja ya kuchambua zaidi viwango  vya malipo vinavyokana na ushuru wa stamp hasa katika kutafautisha mapato ya aina hiyo kupitia miradi  mikubwa na inayoanzishwa nchini ile ya kawaida  ambapo viwango vyake vinaweza kuwa tafuati kuliko ilivyo sasa.

Aidha amesema kwamba  kuna fursa nyingi za mikopo ya kifedha katika mabenki mbali mbali nchini  zinazoweza kutumika kibiashara lakini zimekuwa zikitumika zaidi kwa bikopo ya watu binafsi  kuliko mashirika ambayo yanaweza kuwa  na kiwango cha tija zaidi katika kasi ya ukusanyaji mapato nchini.

Amefahamisha kwamba pia eneo la utayarishaji wa mikataba ya kibisashara kupitia watu binafsi, mashirika na taasisi nalo ni muhimu kuangaliwa kwani linaweza kusaidia kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato na kuchangia kasi zaidi ya kukuza uchumi wa Zanzibar.  

Mhe. Othman ameshauri pia katika jitihada za kuongeza kiwango cha mapato bodi hiyo kuangalia uwezekano katika utaratibu wa Benki za Kiisalamu kwa kuwa bado kunachangamoto kwenye eneo hiilo na itakapotatuliwa itachangia kiwango cha mapato kuongezeka nchini.

Naye Kamshida wa Bodi  hiyo ndugu Ramadhani Juma Mwenda, ameeleza kwamba ZRB inaendelea kufanya mageuzi  katika  mifumo yake ya ndani  ya ukusanyaji mapato jambo linalochangia kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa  Zanzibar kupitia bodi hiyo.

Amesema kwamba  kutokana na hali hiyo wamefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu  kimeongezeka kutoka  shilingi bilioni 131 hadi 135 kwa kipindi cha miezi mitatu.

Amesema pia jitihada kubwa imefanywa katika kudhibiti udanganyifu na uvujaji wa mapato  sambamba na kutengeneza mazingira bora ya ulipatiji  kodi  za aina mbali mbali jambo linalochangia kuongeza ufanisi na mafanikio zaidi ya kukusanya kodi.

 

MWISHO

Imetolewa na Ofisi ya  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo cha Habari leo tarehe 17.10.2022.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.