Habari za Punde

Suluhisho la Ucheleweshaji wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Lapatikana

Kamishina wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali A.Milanzi akizungumza na Washiriki wa Mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo - National Project Management Information System (NPMIS) yanayofanyika Jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo - National Project Management Information System (NPMIS) yanayofanyika Jijini Arusha.

Na. Ramadhani Kissimba,WFM - Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekuja na suluhisho la tatizo lililokuwa linasababisha baadhi ya Miradi ya Maendeleo kuchelewa kutekelezwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mlolongo mrefu uliokuwepo katika hatua za awali za utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Hayo yamesemwa na Kamishina wa Idara ya Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt Mursali Milanzi wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo - National Project Management Information System (NPMIS) yanayofanyika Jijini Arusha.

 

Dkt. Milanzi amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wadau wengine kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali wakati wa uratibu au utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo changamoto ambazo zimekuwa zikipelekea kupunguza kasi ya utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi mbalimbali nchini.  

 

‘’Napenda kuchukua nafasi hii kuelezea kwa ufupi baadhi ya changamoto ambazo Wizara ya Fedha na Mipango na wadau wengine wanaoratibu au kutekeleza miradi na programu za maendeleo wamekuwa wakikabiliana nazo kwa muda mrefu ikiwemo, barua za miradi mipya na inayoendelea kupokelewa bila kuwa na viambatisho muhimu vya nyaraka za miradi, baadhi ya viambatisho kuwa vikubwa na kushindwa kuingizwa kwenye majalada na upatikanaji usioridhisha na usio wa haraka wa taarifa za miradi pindi zinapohitajika’’. Alisema Dkt. Milanzi.

 

Dkt. Milanzi aliongeza kuwa katika kutatua changomoto hizo, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikisha wadau mbalimbali imeona ije na suluhisho kwa kuanzisha Mfumo utakaohusika moja kwa moja na Utekelezaji wa Miradi na Programu za Maendeleo nchini, Mfumo ambao umezingatia mahitaji ya wadau wote na utendaji kazi wa majukumu ya kila mdau nchini katika uratibu na utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo.

 

Aidha, Dkt. Milanzi alisema kuwa kuna umuhimu wa Mfumo huu kuanza kutumika ipasavyo na ndio maana Wizara ya Fedha na Mipango ikaandaa Waraka wa Hazina Na.5 wa mwaka 2020/21 kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo na Waraka wa Hazina Na. 1 Kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/23 unaosisitiza uzingatiaji na utekelezaji wa Mfumo huu.

 

 

Awali akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. John Sausi amesema lengo la uanzishwaji wa Mfumo huo ni kutaka Serikali kuwa na orodha ya Miradi yote inayoitekeleza na kuwa na taarifa sahihi ya miradi hiyo.

 

Dkt. Sausi aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuuboresha mfumo huu kulingana na mahitaji ya wadau na kuwaomba washiriki na wadau wote wanaotumia Mfumo huo kuendelea kutoa maoni yatakayosaidia kurahisha utendaji kazi wa Mfumo huo.

 

 

Pia kwa kumalizia Kamishina wa Idara ya Mipango ya Kitaifa, Dkt. Milanzi alisema kuwa utumiaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo – National Project Management Information System (NPMIS) utasaidia kuongeza ufanisi kwenye uibuaji, upangaji, uwasilishaji, uchambuzi, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya Miradi ya Maendeleo, pamoja na kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za Miradi ya Maendeleo iliyopo katika hatua mbalimbali za mzunguko wa utekelezaji wa miradi (Project cycle).

 

Mafunzo hayo ya matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo yanahudhuriwa na washiriki 58 ambapo washiriki 26 wanatoka katika Ofisi za Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa na Watumishi 32 kutoka katika Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.