Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa Aongoza Kikao cha Nane cha Kamati Kuu ya Sensa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni  Mwenyekiti wa  Kamati ya Kitaifa ya Sensa akizungumza wakati alipofungua kikao cha kamati hiyo kwenye ukumbi wa hoteli  ya Verde, Zanzibar Oktoba 11, 2022. Kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza, Hemed Suleiman Abdulah.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni  Mwenyekiti wa   kamati hiyo wakati alipofungua kikao cha kamati hiyo kwenye ukumbi wa hoteli  ya Verde, Zanzibar Oktoba 11, 2022. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza, Hemed Suleiman Abdulah.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

Na.Ali Mohammed. OMPR. 

Kukamilika kwa zoezi la Sensa ya watu na Makazi limechangiwa kwa kiasi kikubwa na miongozo iliyokuwa ikitolewa na viongozi Wakuu wa nchi.

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa kamati kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na Makaazi, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa katika kikao kazi kilichofanyika Ukumbi wa Hoteli Verde, Mtoni jijini Zanzibar.

Alisema, kamati imeridhishwa na taarifa za matokeo ya awali ya sensa ya watu na Makaazi ambayo imeoneshwa asalimia 98% ya watanzania wamehesabiwa mijini na vijini.

Mhe. Majaaliwa alisema Watanzania wengi waliona umuhimu wa kuhesabiwa na kutoa ushirikiano mkubwa kwa makarani, hali hii itairahisishia Serikali kufikia malengo iliyojiwekea kwa wananchi wake.

Aidha, alisema asilimia mbili 2% iliyobakia ni ya wale ambao hawakuhesabiwa kutokana na mazingira ya kutatanisha waliyokua nayo. Hata hivyo, watu hao bado wanakwenda katika Ofisi za Serikali za Mitaa waliopo kwa lengo la kutaka kuhesabiwa ingawa muda wake umeisha.

Akizungumzia kuhusu kutolewa kwa taarifa Rasmi ya Sensa ya watu na Makaazi, Mhe Majaaliwa alisema kwamba taarifa hiyo inatarajiwa kutolewa na Rais wa Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ifikapo tarehe 31 mwezi huu katika Uwanja wa Jamuhuri, Mkoani Dodoma.

Alisema katika hafla hiyo, makundi mbali mbali yanatarajiwa kualikwa wakiwemo viongozi wastaafu, viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama Vya Siasa, Mashirika binafsi na wageni kutoka nchi mbali mbali pamoja na wananchi kwa ujumla.

Alisema, zoezi la uwekaji wa anuani za Makaazi katika miji na vijiji litakuwa endelevu hivyo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wa vijiji kuendelea kulisimamia zoezi hili katika sehemu zote zinazoendelea kujengwa.

Nae Mwenyekiti mwenza wa kamati hio ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza kuwa haikua kazi rahisi sana kukamilisha zoezi hilo, kwani imepitia katika changamato na nyakati tofauti lakini kupitia hekma na busara za viongozi pamoja na ushirikiano wa wananchi jambo hili limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha, Mhe. Hemed aliwashukuru watanzania wote na Wadau mbali mbali walioshiriki katika jambo hili ambalo litairahisishia Serikali kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Hata hivyo, aliwataka viongozi kuendelea kujitolea katika utendaji kazi kwa kulipambania Taifa pamoja na kuwataka kila mmoja kujifunza kupitia jambo hili kwani litabakia kuwa ni historia kwa vizazi vya Sasa na baadae.

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

11.10.2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.