Na Abdulrahim Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) kwa kuendelea kusimamia Uchumi wa Tanzania kuimarika hasa katika kipindi hichi cha kuzorota kwa hali ya Uchumi Duniani.
Mhe. Hemed ametoa Kauli hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Kuu ya Tanzania Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Amesema Uchumi wa Tanzania unazidi kuimarika kuzingatia Sera na Miongozo iliyopo katika kufikia Malengo waliojiwekea Benki hiyo ili kuisadia Serikali katika kudhibiti Uchumi wake.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imelenga kusaidia Wananchi wake kupitia Miradi mbali mbali ya maendeleo kwa lengo la kuikuza Zanzibar kiuchumi.
Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa licha ya Zanzibar kuathirika kiuchumi kwa kupungua Watalii kutokana na mripuko wa maradhi ya Uviko 19 kwasasa inaendelea kupokea Watalii wengi kutoka Mataifa mbali mbali ambao wanahitaji huduma tofauti za kifedha Nchini.
Ameeleza kuwa ni vyema Benki hiyo kufikiria zaidi njia bora ya kuweka huduma za kubadili Fedha ili wageni wanaokuja Nchini kuweza kupata huduma hiyo kwa wakati na kwa urahisi zaidi.
Ameishauri Benki hiyo kufanya uchunguzi yakinifu kuona maeneo muhimu ya kuweka huduma hiyo kwa mujibu wa uhitaji wa wananchi ili kuepuka matatizo wanayokumbana nayo wageni wanapokuwa Nchini.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania kukamilisha taratibu za Malipo kwa wananchi walioathirika kwa kuweka Fedha zao katika Benki ya FBME kwa kuzingatia taratibu husika.
Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kuzingatia Fura za ajira kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa Upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Florens Luoga amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa B.o.T inaendelea kuishauri Serikali katika Masuala mbali mbali ya kukuza Uchumi hasa katika kipindi hichi cha kuzorota kwa Uchumi Duniani ili kutafuta Njia mbadala za kupata Fedha kwa ajili ya kuendeleza Ujenzi wa Miradi katika kuwaletea Maendeleo endelevu Wananchi wake.
Ameeleza kuwa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeathirika na Mripuko wa uviko 19 na Vita baina ya Ukraine na Urusi ambapo Benki hiyo inaendelea na jitihada mbali mbali ili kukuza Uchumi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment