Habari za Punde

Kliniki ya Magonjwa ya Moyo, Ubongo na Mishipa ya Fahamu yaimarishwa Mloganzila.

Na.Buberwa Aligaesha 

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema uongozi wa hospitali umeamua kuimarisha kliniki za magonjwa ya moyo, ubongo na mishipa ya fahamu katika tawi lake la MNH-Mloganzila kwakua kuna vifaa, watalaamu na eneo tulivu kwa matibabu hayo.

Prof. Janabi amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema kabla ya kuanza kuwaona wagonjwa wa magonjwa ya moyo ambao wamekuja kupata huduma katika kliniki hiyo.

Ameongeza kuwa, kuanzishwa kwa kliniki za magonjwa ya moyo na mishipa ya fahamu kutapunguza msongamano wa wagonjwa Muhimbii-Upanga na kuwezesha hospitali zote mbili kutoa huduma bora na kwa wananchi.

“Hospitali ya Mloganzila ina vitanda 608 hivyo hakuna sababu ya kuwa na msongamano Muhimbili Upanga ikiwa Mloganzila kuna nafasi, huku ni sehemu nzuri kwa wagonjwa wa moyo kutibiwa na mimi nitakuwa na kliniki kila Jumatano” amesema Prof. Janabi 

Prof. Janabi amesisitiza kuwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, ubongo na mishipa ya fahamu waliokuwa Muhimbili Upanga wamehamishiwa Mloganzila hivyo wananchi wasiwe na shaka pale wanapoambiwa huduma zinatolewa Mloganzila.

Naye, Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema Hospitali ya Mloganzila itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa wamejipanga kuhakikisha wananchi wanafurahia huduma za hospitali hii.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu Dkt. Henrika Kimambo ametaja baadhi ya huduma zinazotolewa katika kliniki ya ubongo na mishipa ya fahamu ni pamoja na kiharusi, kupooza, matatizo ya mgongo, misuli na magonjwa yanayoathiri magonjwa ya uti wa mgongo.

Dkt. Henrika ameongeza kuwa kliniki yao ina madaktari wa kutosha na kuwahakikishia wananchi kuwa wategemee kupata huduma bora za matibabu na zinazokidhi matarajio yao.

Akilezea namna alivyohudumiwa Bi. Furaka Upala amesema Hospitali ya Mloganzila inatoa huduma nzuri za matibabu na pia amepongeza namna wateja wanavyopokelewa na kupelekwa maeneo yahuduma kwa muda mfupi na pia hakuna msongamano katika utoaji wa huduma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.