Habari za Punde

Hutuba ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani 1 Disemba 2022 Pemba

 

HOTUBA YA MGENI RASMI, MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA OTHMAN MASOUD OTHMAN, WAKATI WA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI,TAREHE 1 DISEMBA 2022

PAHALA: KISIWANI PEMBA

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;

Waheshimiwa Mawaziri;

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais;

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;

Wakuu wa Wilaya mliopo;

Maafisa Wadhamini nyote mliopo;

Mwenyekiti, Bodi ya Tume ya UKIMWI Zanzibar;

Ndugu Makamishna wa Bodi ya Tume ya UKIMWI;

Mwakilishi, Shirika la ‘UNAIDS’ na Wawakili wengine wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN);

Mkurugezni Mtendaji, Tume ya UKIMWI Zanzibar;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Assalamu Alaykum!

Naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kukutana tena katika siku hii muhimu ya leo. Aidha nichukue nafasi hii kuishukuru Tume ya UKIMWI Zanzibar kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho haya ya Kilele cha Siku ya UKIMWI Duniani.

Ndugu Wananchi,

Kama inavyofahamika, siku ya leo tunaungana na   Jamii ya Kimataifa Duniani, katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo  huadhimishwa ifikapo tarehe Mosi Disemba  ya kila Mwaka; Siku hii huwa ni ukumbusho kwa Nchi-Wanachama wa Umoja wa Mataifa na Jamii ya Kimataifa, juu ya azimio la kuwa na jamii iliyo salama, kutokana na maradhi ya UKIMWI.

Maadhimisho haya hufanyika kwa lengo la kuikumbusha jamii kuwa maradhi ya UKIMWI bado yapo; Aidha tunapata fursa ya kujitathmini katika utekelezaji wa mikakati tuliyojiwekea ya kupambana na maradhi haya; Na pia kuonyesha mshikamano wa pamoja na msaada kwa watu wanaoishi na VVU; na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao kutokana na maradhi ya UKIMWI.

Ndugu Wananchi,

Siku hii hubeba ujumbe makhsusi yaani kauli mbiu na ambapo Ujumbe wa Mwaka huu unasema, ‘TOA HUDUMA ZA UKIMWI KWA USAWA’, Ujumbe huu unakusudia kutoa msisitizo kuhusu huduma zote zinazohusiana na maradhi ya UKIMWI, zikiwemo za elimu kwa jamii, uhamasishaji wa mabadiliko ya tabia, huduma za kujikinga na maambukizo ya VVU, na huduma za matibabu, zinawafikia watu wote kwa usawa na hakuna mtu ambaye anakosa au anabaguliwa kupata huduma hizo.

Ndugu Wananchi,

Tukumbuke kwamba nchi yetu imeungana na Mataifa mengine ulimwenguni, katika kuyafikia malengo mbali mbali ya kiulimwengu. Malengo haya ni pamoja na kuzifikia ‘95 Tatu’, ifikapo Mwaka 2025 Sambamba na lengo la kumaliza tatizo la UKIMWI ifikapo 2030. (1. Asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wanajitambua; 2. asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU, ambao wanajitambua, wawe wanatumia Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) na 3. Asilimia 95 ya wanaotumia dawa za ARVs, wawe wameweza kupunguza idadi ya virusi mwilini na kuwa chini ya virusi 1,000.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloratibu Mapambano Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), lilitoa taarifa juu ya hali ya dunia katika kufikia malengo hayo. Taarifa hiyo imeonesha kwamba kasi ya kuyafikia Malengo ya 2025, bado si ya kuridhisha.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hadi kufikia Disemba 2021, idadi ya maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI kwa mwaka, yamepungua kwa asilimia 32 tu, ukilinganisha na lengo la kupunguza kwa asilimia 83. Kiwango cha maambukizo mapya kwa vijana wa kike wa rika-baleghe (adolescents) kimeongezeka kwa mara tano zaidi ya malengo ya mwaka 2025. Utumiaji wa vifaa na huduma za kinga kwa makundi maalum, nao umepungua na kufikia baina ya asilimia 27 hadi 53, ikiwa ni asilimia ndogo, kwa kuweza kuyafikia malengo ya 2025.

Ndugu Wananchi,

Kwa upande wetu wa Zanzibar, hali imekuwa sio mbaya katika kuyafikia malengo tuliyojiwekea, yakiwemo yale ya kuzifikia ’95- Tatu’ ifikapo mwaka 2025. Hadi kufikia Septemba, taarifa zinaonesha kwamba ‘95’ ya Kwanza tulikuwa bado hatujaifikia. Lengo la ‘95’ hii, kama ilivyokwisha- elezwa ni kwamba, asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wanajitambua; na hapa kwetu hadi kufikia mwisho wa Septemba Mwaka huu, tulikuwa na asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU, ambao tayari wanajitambua. Kwa upande wa ‘95 ya Pili’, ambayo inalenga asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU, ambao wanajitambua, wawe wanatumia Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs). Hadi kufikia Septemba tulikuwa na asilimia 99.9 ya watu wanaoishi na VVU wanaojitambua ambao wanatumia dawa za ARVs, hii ni kuonesha kwamba

shabaha hii tumeifikia kabla ya kufikia muda wake. ‘95 ya Mwisho’ inalenga asilimia 95 ya wanaotumia dawa za ARVs, wawe wameweza kupunguza idadi ya virusi mwilini na kuwa chini ya virusi 1,000. Hadi kufikia Septemba mwaka huu tulikuwa na asilimia 94.3 ya wanaotumia dawa za ARVs, ambao wameweza kupunguza idadi ya virusi.

Ndugu Wananchi,

Takwimu hizi zinatuonesha kwamba, tupo katika hatua nzuri ya kuzifikia shabaha za ‘95 Tatu’ ifikapo 2025, shabaha ambazo kama tutazifikia, basi tutakuwa tupo katika uwezekano mkubwa wa kufikia Lengo la Mwaka 2030 la Kumaliza Tatizo la UKIMWI. Hata hivyo, mtazamo wa ujumla wa takwimu hizi hautupi picha halisi katika kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma za upimaji, matibabu na kuweza kupunguza idadi ya Virusi.

Takwimu zinatuonesha kwamba, katika kutumia huduma za ushauri-nasaha na upimaji wa maambukizo ya VVU, wanaume bado tuko nyuma ukilinganisha na wanawake. Takwimu za watu waliopimwa Virusi vya UKIMWI mwaka huu hadi Septemba, zinaonesha wanawake waliojitokeza kupima katika vituo vya ushauri nasaha ni wengi, ukilinganisha na wanaume. Kati ya watu Laki Moja Elfu Thelathini na Tatu Mia Nne na Mbili (133,402), waliojitokeza kupima afya zao, Elfu Sabiini na Tatu na Khamsini (73,050) walikuwa ni wanawake, ukilinganisha na wanaume ambao ni Elfu Sitini Mia Tatu Khamsini na Mbili (60,352). Aidha katika watu Elfu Saba Mia Nane Arubaini na Sita (7,846) wanaotumia dawa za ARVs wanaume ni Elfu Mbili Mia Nne Ishirini na Moja (2,421) ukilinganisha na wanawake Elfu Tano Mia Nne Ishirini na Tano (5,425).

Ndugu Wananchi,

Taarifa hizi zinatuonesha kwamba ndani ya jamii yetu upatikanaji na utumiaji wa huduma za UKIMWI haupo sawa kwa watu wote. Kuna watu ambao wanafikiwa na huduma na kuzitumia, na wapo pia kundi la watu ambalo halifikiwi na huduma, na hivyo hushindwa kuzipata huduma hizo.

Nichukuwe fursa hii kuiomba Tume ya UKIMWI, Wizara ya Afya kupitia Kitengo Shirikishi cha UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma, na wadau wetu wote ambao wanashirikiana nasi katika mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI, kuzifanyia tathmini kwa kina takwimu zetu, ili kubaini makundi ya jamii ambayo yamekuwa yakiachwa nyuma, katika kuzifikia huduma za kinga, matibabu na nyenginezo, zinazohusiana na maradhi. Kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi katika kujitathmini kwa kina, juu ya namna tunavyozifikia shabaha na malengo tuliyojiwekea.

Aidha ni vvema kuvibaini na kuvifanyiakazi, vikwazo na changamoto zinazowazuwia baadhi ya makundi, kushindwa kuzifikia au kuzitumia huduma zilizopo ipasavyo. Tumezisikia takwimu za hali ya unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.  Niwaombe Tume ya UKIMWI kwa kushirikiana na ZAPHA+ kuyafanyia kazi mapendekezo ya ripoti hiyo, na kuandaa mpango maaalum wa kukabiliana na tatizo la unyanyapaa, ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia kwa baadhi ya watu kushindwa kuzifikia au kuzitumia huduma zilizopo.

Ndugu Wananchi,

Niwanasihi sana, tusijisahau na wala tusijidanganye kwani tatizo hili bado lipo na linatisha; ukitaka kujua tishio la UKIMWI kwa Ulimwengu mzima na kwa rika zote, hebu tafakari pale ‘lilipojitega’ (kila mmoja wetu anapajua vyema ila hatuwezi kukwepa tusinase hapo ili maisha yaendelelee!. Hivyo kila mmoja yupo hatarini, au kama wanavyoita wataalamu wetu, ‘at-risk’.

Nitoe wito kwa kila mmoja wetu awe ni ‘askari’ wa kupiga-vita UKIMWI; Kukemea uambukizi wa makusudi au hata wa bahati mbaya; tulaani udhalilishaji wa aina zote; tuepuke unyanyapaa; na tusisahau hata dua kwa ndugu zetu waliotangulia na sisi tuliopo hai, kama lengo na dhamira ya Siku hii inavyojieleza.

Aidha wakati wengine wanapaza sauti katika kueleimisha jamii kama vile viongozi wa dini na taasisi za kiraia, sisi katika Serikali tunawajibu wa ziada katika mapambano haya. Hivyo niwaombe Viongozi wetu hasa katika ngazi ya Mikoa kuyafanyia kazi malalamiko ya Wananchi pale kunapojitokeza kuwepo kwa mazingira hatarishi ambayo huchochea vitendo vya uasharati na kuongeza maambukizi zaidi ya VVU na UKIMWI. Hatusaidii kabisa kuona kila uchao tunaongeza Vilabu vya Starehe bila udhibiti kila kona ya nchi yetu. Huku ni kujitia kitanzi wenyewe! Tunapaswa kutafakari zaidi na kuchukua hatua!

Ndugu Wananchi,

Mwisho kabisa, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nachukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati wadau wote wanaosaidia juhudi za Serikali yetu katika kupambana na maradhi haya. Shukrani za pekee ziende kwa Washirika mbalimbali wa Maendeleo ambao wanaziunga mkono jitihada zetu kwa hali na mali ili kuhakikisha kwamba tunafikia malengo yetu kwa pamoja. Hayo ni pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UNAIDS, UNFPA, UNICEF, WHO na UNESCO); Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu (Global Fund); PEPFAR, USAID, CDC, Foundation For Civil Society, RFE, AMREF na mengi mengineyo kwa uzito ulio sawa. Ni imani yangu kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kufikia shabaha zetu na za Ulimwengu, za kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Aidha nichukuwe fursa hii kuzishukuru taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali, Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini, na Jamii kwa ujumla, kwa kuungana nasi katika mapambano haya. Ninawatakia kila la kheri na kuwaomba tusichoke kuendeleza vita hivi, ili tatizo la UKIMWI lisiwe janga la taifa.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA!

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.