Na Maulid Yussuf WMJJWW Zanzibar
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi Siti Abbas Ali amesema ipo haja kwa Wasaidizi wa Sheria wa Wilaya zote kupatiwa Mafunzo ya kuondosha Vitendo vya ukatili wa Jinsia kwa Wazee na watoto ili kusaidia kupunguza vitendo hivyo nchini.
Bi Siti ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa mrejesho wa vikundi kazi vya Wasaidizi wa Sheria vya Wilaya zote za Unguja katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji kijinsia, katika ukumbi wa Bima uliopo Mpirani Unguja.
Amesema wananchi wengi wamepata uwelewa juu ya masuala ya Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na wamekuwa na mwamko wa kuviripoti katika sehemu mbalimbali, kutokana na juhudi za Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto katika kutoa elimu pamoja na kutoa msaada wa kisheria.
Amesema Wananchi wanahaki ya kupewa elimu ya kujikinga na vitendo hivyo vya udhalilishaji na kuwataka Wazee kukaa pamoja na watoto wao kuwaelimisha na kufatilia nyendo za watoto wao ili kuwatambua pale watakapopatwa na tatizo lolote ikiwemo la udhalilishaji.
Aidha Mkurugenzi Siti amesifu kazi nzuri inyofanywa na wasaidizi wa sheria wa Wilaya zote na kuwaahidi kulipatia ufunmbuzi tatizo lao ya posho ili liweze kuwasaidia katika kujikimu kimaisha.
Pia ameitaka Wizara kuhakikisha inawapatia Elimu ya kisheria katika vipengele muhimu ili viweze kuwasaidia katika utendaji mzuri wa kazi zao.
Wakiwasilisha ripoti ya mpango kazi katika kipindi cha mwezi wa Octoba hadi disemba, baadhi ya wasaidizi wa sheria wa Wilaya mbalimbali wamesema pamoja na mipango waliyojiwekea kafika utekelezaji wao, wameona kuwepo mizozo katika ndoa hali inayopelekea talaka za kiholela na kupelekea watoto kusambaratika.
Hivyo wameshauri elimu ya ndoa izidi kutolewa kwa wale wanojiandaa kufunga ndoa ili kupunguza talaka za kiholela pamoja na udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Nao wasaidizi wa Sheria wameomba kupatiwa posho kwa wakati pamoja na kuwataka masheha kusimamia suala la kupiga miziki hadi usiku wa manane kwani ni miongoni mwa vichocheo vva vitendo vya udhalishaji.
Wamesema mafanikio mengi yamepatikana kupitia taluma wanayoitoa katika Skuli, mikutanoni, na sehemu za mikusanyiko ya watu lakini changamoto nyingi zimekuwa zikijitokeza ikiwemo badhi ya Wazee kukosa muda wa kuzungumza na watoto wao majumbani jambo ambalo linarejesha nyuma jitihada zao.
Pia uelewa mdogo juu ya utaratibu wa kesi za Mahakamani namna ya kuripotiwa kesi hizo pamoja na kuoneana muhali katika kutoa ushahidi.
No comments:
Post a Comment