Habari za Punde

Jeshi la Polisi lifanye kazi kwa uadilifu kusimamia kesi za wahanga wa matendo ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia - Wito

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amelitaka jeshi la polisi kufanya kazi kwa uadilifu, ushirikiano na kujitolea katika kusimamia kesi za wahanga wa matendo ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ili ziweze kutokomezwa nchini.


Amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa huduma ya mkono kwa mkono na madawati, katika Ukumbi wa Chuo cha polisi, Ziwani Mkoa wa Mjini Unguja.

Mhe. Riziki amewataka maafisa hao kushiriki kikamilifu katika kuzipokea taarifa na kuzifanyia kazi ili kuweza kufikia malengo ya kutokomeza ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kutatua changamoto za kesi zinazowakabili wahanga wa udhalilishaji kwa njia ya mkono kwa mkono ili waweze kupata haki zao.

Mhe. Riziki amesema kuwa Wizara imeandaa mpango kazi wa kufanya mabadiliko ya Sheria ya hifadhi ya mtoto ya mwaka 2011 pamoja na Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2018 kwa ajili ya kutokomeza vitendo hivyo kwa wanawake na watoto nchini.

Vilevile, amesisitiza mashirikiano na jeshi la polisi na wadau wengine ili kufanya kazi kwa pamoja ili kutokomeza matendo ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia nchini.

Aidha, amewataka maafisa hao wa polisi kujiepusha na vitendo vya kupokea rushwa ambavyo vitapelekea kutia dosari kwa jamii Taasisi husika.

Mhe. Riziki amewataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi ili kutoa taarifa mapema mara tu yanapotokea matendo hayo ya udhalilishaji nchini.

Wakati huohuo,  amempongeza Kamishna wa polisi wa Zanzibar kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuunga mkono Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto katika harakati za mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
"Nampongeza Kamishna wa polisi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutembelea jamii ili kujua changamoto zinazowakabili, ili kushirikiana na Wizara yetu kuweza kuzitatua". alieleza Mhe. Riziki.

Vilevile, amefurahishwa kwa elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii na kusema kuwa jamii imepata muamko mkubwa wa kuripoti matendo ya udhalilishaji kutokana na kuendelea kupatiwa elimu kuhusu matendo hayo.

Nae Kashmina wa polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa utendaji wa kazi kwa watendaji wa huduma za mkono kwa mkono na dawati la jinsia.

Aidha, amewataka kuwa wawajibikaji na waaminifu, maafisa ambao wamechaguliwa kufanya kazi katika Hospitali mpya ambazo zinazotarajiwa kufunguliwa na kufanya kazi nchini.

Vilevile, ameahidi kuendeleza na kuboresha mashirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.