Habari za Punde

Kilupi : Hakuna wa kuzuia ushindi wa CCM

KATIBU Mstaafu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Organaizesheni CCM Zanzibar Ndg. Casian Gallos Nyimbo(kushoto),akimkabidhi nyaraka za kiutendaji Katibu mpya wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni Ndg.Omar Ibrahim Kilupi, huku Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui leo Tarehe 31/01/2023.

Na.Is-Haka Omar. -ZANZIBAR.

KATIBU mpya wa Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Ndg.Omar Ibrahim Kilupi, amesema chini ya uongozi wake hakuna Chama chochote cha kisiasa kitakachozuia ushindi wa CCM  mwaka 2025.


Msimamo huo ameutoa leo wakati akikabidhiwa ofisi ya idara hiyo Kisiwandui na aliyekuwa Katibu wa Idara ya Organazesheni Ndg. Galos Cassian Nyimbo huko Kisiwandui Zanzibar.

Kilupi alisema Chama hicho kina tiketi ya kudumu ya kuongoza dola kutoka kwa wananchi wanaokiamini na kukipenda kutokana na usimamizi mzuri wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2022.

 

Alifafanua kwamba CCM ni Chama mwalimu na kiongozi wa vyama vingine vya kisiasa kwani imejiwekea mfumo imara wa kiuongozi na utendaji kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.


Alisema kwamba CCM kupitia ibara ya 5 ya Katiba yake imeweka wazi dhamira yake ya kushinda bila vikwazo kwa kila uchaguzi wa dola.


Alisema idara hiyo inahusika moja kwa moja ma masuala yote ya uchaguzi hivyo jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Dola wa mwaka 2025.


“Nachukua nafasi hii kwanza kukishukru Chama Cha Mapinduzi kilichoamua kunipa dhamana hii kubwa, naahidi kutumia uwezo wangu wote kuhakikisha kinashinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi wowote utakaotokea kuanzia hivi sasa.
Pia ofisi yangu ipo wazi muda wote nipo tayari kushiriana na wanachama,viongozi na watendaji wote wa CCM na wale wenye mawazo na fikra za kujenga chama chetu.”, alisema Kilupi.


Aidha Kilupi aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadili,ueledi na ubunifu ili kwenda sambamba na malengo ya Chama Cha Mapinduzi.

 

Katika maelezo yake Katibu huyo, amewataka maofisa wa idara hiyo kuwajibika katika majukumu yao ya kikazi.


Alisema kama dhamira ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kinavyotaka ni kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja na ndiye na yeye anavyotaka maofisa hao wa idara kuzingatia hilo.

 
"Kila mtu awajibike kwenye kwenye nafasi yake na ninachoamini ni kuwa tukifanya kazi kwa pamoja tutafanikiwa na hatutoweza kushindwa kufikia dhamira ya CCM ya kuhakikisha ushindi wa chama kila uchaguzi,"alisema


"Ninashukuru kwa mapokezi yenu pia ninampongeza Katibu aliyepita Galos kwa kazi nzuri yenye uadilifu hivyo anastahili pongezi kubwa,"alisema


Alisema kama ilivyokawaida na desturi ya chama ni kukabidhiana vijiti vya uongozi na kinachotakiwa ni kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.


Kupitia hafla hiyo ya makabidhiano Ndgu.Kilupi, aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kasi yao kubwa ya kutatua changamoto za wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.


Naye Katibu mstaafu wa Idara hiyo Ndg. Casian Galos Nyimbo, amesema idara hiyo ndio chombo mahsusi cha kufanikisha masuala yote ya uchaguzi wa Chama hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa juhudi kubwa.


Pamoja na hayo aliwataka watumishi katika idara hiyo kutoa ushirikiano mkubwa kwa kiongozi mpya aliyekabidhiwa ofisi ili wafikie kwa haraka malengo endelevu ya Chama Cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.