Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi awaomba wafanyabiashara waagiza vyakula kupunguza bei za bidhaa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wafanyabiashara waagizaji wa vyakula na bidhaa kutoka nje ya Nchi , mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
MFANYABIASHARA Ndg.Tofiq Salim Turky akizungumza wakati wa mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, uliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
MFANYABIASHARA Ndg.Abdulghafur Ismail Mohammed akizungumza wakati wa mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, uliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wafanyabiashara nchini kupunguza bei za bidhaa haswa vyakula kwa nia ya kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa kipato cha chini.

Dk. Mwinyi alitoa ombi hilo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na wafanyabiashara mbalimbali na kujadili kupanda kwa bei ya chakula nchini.

Alisema bidhaa za vyakula ikiwemo mchele zimepanda maradufu hali iliyozusha taharuki kubwa kwa kuongeza ugumu wa maisha.

Alisema haijawahi kutokea mchele kupanda bei kiasi kikubwa kama ilivyosasa na kuongeza kuwa ni bidhaa yenye uhitaji mkubwa kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Zanzibar mchele ndio kila kitu ni sawa na wenzetu Arabuni ukiadimika unga, kukosekana mkate kunakuwa na vurugu mitaani, hapa Zanzibar watu wetu tuu Rahimu sana, lakini sasa hivi wamefikishwa pabaya sana, kilo elfu tatu mchele kubwa, haijahi kutokea, tujitahi Ramadhani inakuja na hili ni ombi langu kwenu” Kwa hisia alitamka Dk. Mwinyi.

“Tukubaliane ndugu zangu wafanyabiashara hali ya ndani sio nzuri, sisi tuone tabu mwananchi wa kawaida kununua mchele kwa kilo shilingi 3000, mchele huu huu miaka miwili iliyopita sisi tunaingia madarakani ilikua kilo shilingi 1700, leo tunakaribia mara mbili ya bei, inaumiza watu, pamoja na bei nzuri ilioko bara tukubali kukosa iyo faida kwaajili ya watu wetu kwa kipindi hiki tushushe bei ya ndani” Kwa hisia alizungumza Rais Mwinyi.

Alieleza kuguswa kwake na bei ya awali ya mchele na kueleza hata kama isifikie ilikotoka kutokanana sababu mbali mbali za mabadiliko ya kiuchumi lakini isiwe kwa bei ya 3000 ambayo ni kubwa sana kwa wananchi.

Aliwashauri wafanyabiashara hao kushirikiana kuchukua meli kubwa zitakazobeba zaidi ya tani 30,000 badala ya kuchukua meli ndongo za tani 5,000 kwa nia ya kuwasaidia watu kuondokana na ugumu wa Maisha uliopo, ilizingitiwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unakaribia.

Aliwaeleza wafanyabiashara hao kuchukua meli kubwa kutapunguza utitiri wa meli ndogo zenye kubeba tani kidogo hali aliyoieleza kwamba inaongeza msongamano bandarini.

Kwa upande wao wafanyabiashara walieleza changamoto kubwa iliyosababisha bidhaa kupanda bei ni mkwamo wa utoaji mizigo bandarini pamoja na gharama kubwa za mizigo zinazotozwa bandarini.

Aidha, waliiomba serikali likiwemo Shirika la Bandari kufanya juhudi za ziada kupunguza mkwamo wa utoaji mizigo na kutoa kipaumbele kwa bidhaa zenye mahitaji ya haraka kwa wananchi ili kumpunguzia mzigo wa lawama Mheshimiwa Rais.

“Mzigo wa lawama kwa tatizo hili najua lote unatupiwa serikali, wafanyabiashara tushirikiane kwa umoja wetu kupunguza hali hii, wananchi hawaelewi nini kinaendelea lakini ukweli hasa bandari yetu imezidia sasa mahitaji yameongezeka, lazima kutumiwe njia mbadala ya kuwahisha mizigo, siku 30 nyingi sana mzigo kukaa bandarini” alisema Mfanya biashara Bopar interprize.

IDARA YA MAWASILIANO - IKULU, ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.