Habari za Punde

Mhe Hemed ashiriki maziko ya Mwanasiasa Mkongwe Nchini Mhe. Hassan Mussa Takrima
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameongoza Viongozi wa Chama na Serikali, Wanafamilia, na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Kumuombea Mwanasiasa Mkongwe Nchini Mhe. Hassan Mussa Takrima iliyosaliwa Msikiti wa Fuoni meli tano Wilaya ya Magharibi B.

 Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifika nyumbani kwa marehemu kutoa Pole kufuatia msiba huo na kueleza kuwa Marehemu alikuwa ni Kiongozi mwenye hekima na busara kipindi chote cha uongozi wake akiwa mtumishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Aidha Alhajj Hemed ameeleza kuwa Marehemu alikuwa ni muumini wa Umoja na Mshikamano na kuwataka wafiwa kuyaendeleza mema hayo pamoja na  kuwa na subira kipindi chote cha Msiba na kuendelea kumuombea Dua  marehemu huyo.

 

Akimuelezea Mheshimiwa Takrima aliekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai amesema Marehemu katika Utumishi wake alikuwa ni Kiongozi wa mfano ambae alitumia Elimu na uzoefu wake katika kukiletea maendeleo Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

 

Marehemu katika uhai wake ameshika nyadhifa mbali mbali ikiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi.

 

Marehemu Hassan Mussa Takrima amefariki usiku wa kuamia leo nyumbani kwake Fuoni Meli Tano na kuzikwa Kijijini kwao Makunduchi Miwaleni.

 

Innaa Lillaahi wainnaa Ilaihi Raajiun.

 

……………….

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

12/02/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.