RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Madaktari Bingwa wa Moyo kutoka Nchini Kuwait wa Taasisi ya “Children’s Heart Charity Association” ukingozwa na Kiongozi wa Ujumbe huo Dr.Faisal Al Saedie (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-2-2023.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema timu ya
madaktari bingwa wa moyo waliopo nchini wakitokea Kuweit inatoa mchango mkubwa
kwa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Alisema uwepo wa timu hiyo umeongeza nguvu za kiutendaji
kwenye hospitali walizofikia madaktari hao na kueleza ni sehemu ya jitihada za
Serikali ya awamu ya nane ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
Afya nchini.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza
na timu hiyo iliyoongozwa na mwenyeji wao, Waziri wa Afya, Nassor
Ahmed Mazrui.
Alisema tatizo la moyo bado linaendelea kuwasumbua
wananchi wa Zanzibar na kueleza kuwa timu hiyo imekuja kutoa mchango zaidi kwa
watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo.
Alisema bado kuna watoto wengi wanaokabiliwa na tatizo
hilo na kuongeza kwamba timu ya madaktari hao anaamini itakuwa mchango mkubwa
wa watoto wengi kupata matibabu wakiwa nchini.
Alisema Serekali imekua ikitumia gaharama kubwa ya
matibabu ya moyo kwa kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi na kueleza mbali ya
gharama za tiketi na matibabu ambazo wagonjwa na familia zao yanawagharimu
lakini Serikali imekua ikibeba mzigo mkubwa kugharamia matibabu hayo.
Alisema Serikali ina lengo la kuona inatoa huduma zote
nchini na kwamba magonjwa yote yanatibiwa ndani ya nchini bila ya kutumia
gharama kubwa nje ya nchi ndio maana imejenga hospitali za kisasa kutoa wepesi
kwa wananchi wake.
Dk. Mwinyi aliiahidi timu ya madaktari hao kushirikiana
nao kwa kipindi chote watakachokuwepo nchini pamoja na kuwaasa kwamba wasisite
kuiuomba Serikali endapo watakwama kwenye ufanisi wa kazi zao.
Alisema uwepo wa timu hiyo ni faida kubwa kwa Serikali
pia aliwaomba mchango wao kiutendaji na kuendelea kuiunga mkono Serikali hasa kwenye
hospitali zake mpya za Wilaya zilizojengwa ambazo zinahitaji wataalamu wa aina
zote kuongeza nguvu ya kuwatumikia wananchi pamoja na kuwashauri kwenye masuala
ya afya. Pia Dk. Mwinyi aliishukuru timu hiyo kwa kukubali kwao kufanyakazi na
Serikali.
Naye
Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, aliishukuru
timu ya madaktari hao kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kukubali
kujitoa kuongeza nguvu kuimarisha sekta ya afya nchini.
Alisema timu ya madaktari hao kwa kushirikiana na
madaktari wenyeji wa hospitali ya Mnazi Mmoja wamefanikiwa kuwahudumia watoto
33 waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo ya moyo, 30 kati yao walitibiwa na
kuruhusiwa kurejea majumbani mwao na watatu bado wanaendelea na matibabu
hospitali hapo.
Mmoja wa Madaktari hao, Dk. Fesal Al - Said akizungumza mbele ya Rais aliishukuru
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, kwa mapokezi yao na
ushirikiano inaowapatia tokea siku waliyofika nchini.
Alisema lengo la ujio wao Zanzibar ni kutoa ushirikiano
kwenye kutatua matatizo ya watoto yanayowakabili hasa matatizo ya moyo.
Alisema taasisi yao ya kuwasaidia watoto wenye matatizo
ya moyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo nchini
kwaajili ya kutoa misaada ya matibabu kwa watoto hao.
Walisema lengo la taasisi yao ni kuokoa maisha ya watoto
wanaosumbuliwa na matatizo hayo ili
kuwasaidia kufikia ndoto zao kwenye maisha yao ya baadae.
Hivyo, alishukuru ushirikiano wanaendela kuupata kutoka
kwa wenyeji madaktari wenzao ambao alieleza ni wakupigiwa mfano.
Timu hiyo ya madaktari kutoka taasisi ya kuwasaidia
watoto wenye matatizo ya moyo kutoka Kuweit imekuja na madaktari 40 wakiwa
wamegawanyika wengine wapo Dar es Salaam na wengine Dodoma.
Nchi ya Kuweit ni taifa kutoka Asia Magharibi ambayo inapakana na nchi za
Iraq kwa upande wa Kaskazini, Saudi Arabia Kusini, pia inachangia mipaka ya
bahari na nchi ya Iran.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment