Waziri wa Fedha na Mipango Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa katika mazungumzo na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. David Malpass, na kujadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki hiyo, yatakayoiwezesha nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.(kushoto kwa Waziri) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Dkt.Saada Mkuya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar.Mhe. Dkt.Saada Mkuya, akizungumza wakati wa mkutano na Rais wa Benki ya Dunia Bw.David Malpass, wakati wa mkutano wa kujadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia yatakayowezesha Nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo yalioyofanyika Jijini Washington DC.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Dunia Bw.David Malpass na Ujumbe wake baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliofanyika Jijini Washington DC.
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. David Malpass, na kujadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo, yatakayoiwezesha nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Katika majadiliano hayo, Bw. Malpass, alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuvutia ushiriki wa Sekta Binafsi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na katika kukuza uchumi wa nchi na maisha ya watanzania Tanzania.
Aidha, Bw. Malpass alihamasisha juhudi zaidi katika kulinda uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa ni nguzo katika kukuza uchumi na kushauri Sekta binafsi kupewa kipaumbele katika kusukuma ajenda ya maendeleo jambo ambalo litachochea uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuboresha Maisha ya watu.
Vilevile, Rais Malpass ameishukuru Tanzania kwa kuridhia kuwa wenyeji wa mikutano miwili mikubwa ya kimataifa ambayo ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uendelezaji wa Rasilimali Watu (Africa Human Capital Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Julai mwaka huu, na Mkutano wa Mapitio ya Utekelezaji wa Nusu Muhula wa Mgao wa Fedha katika Mzunguko wa 20 wa IDA (IDA 20 Mid-Term Review) mahususi kwa ajili ya utoaji mikopo na misaada kwa nchi wanachama wa Benki ya Dunia, utakaofanyika mwezi Desemba 2023 visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Rais Malpass, kwa kuisaidia Tanzania kutimiza agenja zake mbalimbali za Maendeleo katika kipindi chake cha uongozi kama Rais wa Benki ya Dunia.
Alisema katika kipindi chake cha uongozi, Bw. Malpass ameimarisha ushirikiano wa Benki ya Dunia na Tanzania na kumfahamisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya Dunia, Tanzania imepata fedha za mkopo nafuu na misaada mbalimbali iliyosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kimkakati.
Aidha, amerejea shukrani zake kwa Benki ya Dunia kwa kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi 29 ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati ambayo imefikia gharama ya zaidi ya shilingi trilioni 16.7, ambapo miradi 24 ni ya kitaifa na mingine 5 ni ya kikanda.
No comments:
Post a Comment