RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al
hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameihimiza jamii kujikita kwenye malezi yenye
maadili ya kiislamu kwa watoto na vijana ili wawe na tabia njema zitakazomridhisha
Mwenyezi Mungu (S.W).
Al - hajj
Dk. Mwinyi alitoa nasaha hizo wakati wa ufunguzi wa msikiti wa masjid Al
- Jumaa, uliopo Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema jamii imegubikwa
na wingu la matatizo yanayosababishwa na mporomoko wa maadili, kujaa madhila ya
udhalilishaji, kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya, wizi wa mazao ya
kilimo na mifugo kulikosababishwa na kukosa malezi bora yenye hofu ya uchamungu
ukosefu wa maadili.
“Vijana wetu wafundishwe
dini yao vizuri, wafundishwe kitabu cha Mwenyezi Mungu, wafundishwe tabia
njema, tutapunguza matatizo yanayotokea ukubwani” Aliasa Dk. Mwinyi.
Al - hajj
Dk. Mwinyi pia alizinasihi jamii
kutumia nyumba za ibada kuwafundisha vijana mustakbali mwema wa ustawi wa
maisha yao kupitia madrsa na nyumba za ibada ikiwemo misikiti, aliongeza malezi
hayo yanaanzia kwenye nyumba za ibada ili kuondosha matatizo yanayoisumbua
jamii.
Akieleza neema za mwezi
mtukufu wa Ramadhani, Al - hajj Dk. Hussein
Mwinyi aliwasihi jamii kukithirisha ibada na kujitahidi kwenye kuongeza ibada
ya sala za taraweikh aliyoieleza kwamba inakuja mara moja tu kwa mwaka pamoja
na kuwanasihi waumini wa msikiti huo, kuendeleza ibada za sala za sunnah.
Hata hivyo, Al - hajj Mwinyi
aliahidi kuujengea uzio msikiti huo ili uiendaene na hadhi yake na uendelee kudumu
na kuwa imara.
Hakika hatua nyengine Al - hajj Dk.
Mwinyi aliwataka waumini wa msikiti huo kuendelea kuutunza na kuuenzi ili udumu
kwaajili ya vizazi vya sasa na baadae.
Akizungumza kwenye ibada hiyo ya sala ya Ijumaa, Katibu
Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume aliwasihi waumini wa
dini ya kiislamu kuutumia vyema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kujitathmini na
kujipima mema na mabaya yao mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuongeza bidii ya
kufanya ibada hasa kwa siku chache zilizobakia kabla ya kumalizika kwa ibada ya
mfungo wa mwezi huo.
“Huu ndio mwezi wa kikuthirisha kheri na kufanya
mazuri zaidi yatakayompendezesha Mwenyezi Mungu, ili kupata msahama wake na sio
kupoteza muda na kuanzisha michezo isiyo na tija kwenye jamii” Alishauri Katibu
huyo.
Mapema, akisoma risala ya ufunguzi wa msikiti huo Ustadhi
Abdalla Makame Makame, alisema ujenzi wa msikiti ulichukua miezi minne tokea
kunza hadi kukamilika kwake.
Alieleza ulianza kujengwa Novemba 11 mwaka 2022 na
ulikamilika tarehe 13/03/2013 ambao unatarajiwa kuchukua hadi waumini 612. Pia
alieleza ujenzi wa msikiti huo ulikuja kutokana na kuongezeka kwa mahitaji
ikiwemo ufinyu wa nafasi kwa msikiti wa awali uliosababishwa na kuongezeka kwa
waumini wengi kijijini hapo baadhi yao wakiwa wahamiaji katika eneo hilo.
Ust. Makame aliongeza sababu nyengine ya kujengwa
kwa msikiti huo ni kupisha utanuzi wa ujenzi wa barabara inayotarajiwa kutoka Dunga
Mitini kuelekea Chwaka.
Ujenzi wa msikiti wa masjid Al – Jumaa uligharimu shilingi
milioni 178.148 ambao ulifadhiliwa na shekh Said Saleh.
IDARA
YAMAWASILIANO, IKULU ZANZI
No comments:
Post a Comment