Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kushiriki katika Mambo Yenye Kheri na Yanayomridhisha Mwenyenzi Mungu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkaribisha tende Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi kwa ajili ya kupata Iftari iliyoandaliwa na Mhe.Rais wa Zanzibar kwa Wananchi wa Makundi Maalum wa Mkoa wa Kusini Unguja iliyofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohammed Shein SUZA Tunguu Wilaya ya Kusini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kukubali kwao kujumuika naye kwenye futari ya pamoja aliyowaandalia, ikiwa ni kawaida yake aliyojipangia kila ifikapo mwenzi mtukufu wa Ramadhan katika kutekeleza ibada ya mfungo huo.

Katika hafla hiyo Rais Dk. Mwinyi aliwasa wananchi hao kuendelea kuishi na kudumisha amani iliyopo nchini, kuishi kwa kushirikiana katika mambo yenye heri na yanayomridhisha Mwenyezi Mungu (S.W).

“Leo tumekuja kujumuika pamoja nanyi ndugu zetu wa Kusini Unguja kama mlivyosikia juzi tulikua Kaskazini Unguja….

….Nakushukuruni nyote kwa muitikio wenu kuja kuungana nami kwenye hafla hii, nilitamani watu sote tungeshiriki lakini isingewezekana, nimemuomba Mkuu wa Mkoa huu awawakilishe wananchi kwa makundi na amefanya hivyo, basi nimefurahi hata nyinyi mliowakilisha wenzenu tumefurahi pamoja, Mwenyezi Mungu akulipeni kila la kheri” alisifu Dk. Mwinyi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa huo, Hadid Rashid Hadid alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba wananchi wa Mkoa huo wanafurahishwa na matendo anayoyafanya ya kuwaletea wananchi wa Zanzibari maendelo kila uchao.

“Mhe. Rais tunachokuomba wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja, endelea na hatua zako ulizozidhamiria za kutuletea maendeleo katika nchi yetu na Mkoa wetu wa Kusini Unguja.”Alipongeza RC Hadid.

Kwa upande wa wananchi wa mkoa huo walitumia fursa hiyo pia kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kujumuika nao kwenye futari ya pamoja, aidha, walimueleza kuwa mkoa wao uko salama na daima wanafurahishwa na amani na utulivu ya mkoa wao na nchi kwa ujumla.

Vile vile, walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa  kutunukiwa tunzo tunzo maalum ya watu mashuhuri walioleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji Afrika, iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya “Global Water Changemakers” kwenye Kongamano la Umoja wa Mataifa nchini Marekani Machi 22 mwaka huu na alikabidhiwa juzi Ikulu, Zanzibar na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambae ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Maji duniani kanda ya Afrika ya Kusini.

Aidha, walimueleza Dk. Mwinyi kwamba tunzo hiyo ni ishara njema kwa anayowafanyia wananchi wake na kumueleza kati ya matangi 10 ya maji safi na salama, aliyowajengea wananchi wa Zanzibar Unguja na Pemba yenye ujazo wa kila moja lita milioni moja matatu kati yao pia yamejengwa Mkoa wa KUsini Unguja.

Walimueleza Dk. Mwinyi kwamba wanazidi kumuombea mazuri, aendelee kuyafanikisha kwa wananchi wa Zanzibar katika ustawi wa miundombinu ya barabara, afya elimu na jamii kwa ujumla.

Hafla hiyo ya dhifa ya kuwafutarishwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja iliandaliwa na Rais Dk. Mwinyi ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali, vyama vya siasa na wananchi wa makundi yote wakiwemo wazee, wajane, wenyeulemavu watoto na watoto yatima. Ikiwa ni utaratibu aliojiwekea kila ifikapo mwezi Mtukufu wa Ramadhan kujumuika pamoja na wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba na waumini wa dini ya kiislam katika dhifa ya futari ya pamoja ili kujenga umoja, mshikamo, upendo na ushirikiano na kuimarisha amani baina ya viongozi na wananchi.

Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wakijumuika na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi , katika Iftari Maalum aliyomyika katika ukumbi wa mikutano wa Dk.Ali Mohamed Shein SUZA Tunguu Wilaya ya Kusini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi  akizungumza na kuwahukuri Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kumalizika kwa Iftari Maalum aliyowaandalia katika ukumbi wa mikutano wa SUZA Tunguu Wilaya ya Kati Unguja. 
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akisoma dua baada ya kumalizika kwa Iftari maalum iliyoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa Wananchi wa Makundi Maalum wa Mkoa wa Kusini Unguja iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dk.Ali Mohamed Shein SUZA Tunguu Wilaya ya Kati Unguja. 
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid akitowa maelezo ya zawadi zilizotolewa na Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa hafla ya Iftari iliyoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dk.Ali Mohamed Shein SUZA Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.