Habari za Punde

Ndg.Mbeto :Amtembelea Aliyewahi Kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema kinathamini mchango mkubwa wa viongozi,watendaji na makada wastaafu wa kitaifa waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Serikali na Chama hicho.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,mara baada ya kumtembelea kada wa CCM Ali Mzee Ali aliyelazwa katika hospitali ya Alrahma iliyopo Kilimani,Zanzibar.

Mbeto,alisema mafanikio yaliyopatikana nchini yametokana na juhudi kubwa za kiutendaji zilizoasisiwa na makada hao ambao ndio waliongoza na kuweka misingi imara ya kimaendeleo.

Alieleza kuwa hatua hiyo ya kumtembelea kada huyo Ali Mzee, ni sehemu ya utamaduni wa viongozi wa CCM na Serikali zake kuwatembelea wagonjwa na viongozi wastaafu kwa lengo la kuwajulia hali sambamba na kuwafariji.

“Viongozi wa CCM na SMZ tumekuwa na utamaduni wa kuwatembelea viongozi wetu hasa wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan,hivyo hata Mzee Ali ni miongoni mwa viongozi hao na hali yake inaendelea vizuri muda wowote anaweza kuruhusiwa kurudi kwake aendelee na majukumu mengine.”,alifafanua Mbeto.

Naye kada wa CCM  Saleh Mohamed, alieleza kuwa wameridhishwa na huduma za kiafya zinazotolewa na hospitali hiyo kwani hali ya kiongozi huyo wa zamani Mzee Ali, inaendelea kuimarika.

Mzee Ali Mzee amewahi kushika wadhifa mbalimbali Serikalini zikiwemo Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar,mshauri wa Rais na Mjumbe wa Kamati ya maridhiano ya kisiasa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.