Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewaasa Wasanii wa Filamu nchini kutumia majukwaa ya kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii katika kutangaza kazi zao.
Mhe. Chana ametoa rai hiyo, Mei 6, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mdahalo wa wadau wa tasnia hiyo, uliokuwa na lengo la kupata elimu kuhusu soko la filamu katika dijitali ambao umeongozwa na Mada kuu isemayo "Masoko ya Kazi za Filamu kupitia Mitandao ya Kijamii."
"Hivi majuzi nimeshuhudia utiaji saini wa Ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu na Taasisi ya Mashirikiano kutoka Korea Kusini wenye lengo la uanzishwaji wa shule ya filamu hapa nchini, jambo ambalo litaongeza ubora wa filamu zetu na kupanua wigo wa soko la filamu zetu", amesema Mhe. Chana.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa mikopo kwa Wasanii ambapo kwa sasa ipo katika mazungumzo na benki mbalimbali kutoa mikopo hiyo ili kuwafikia wadau wengine zaidi.
Ameongeza kuwa, Bodi ya Filamu ina makubaliano na Shirika la Maendeleo kutoka Korea Kusini (KOICA) ambapo kuanzia mwezi Juni mwaka huu, shirika hilo litaanza kusomesha Watumishi wa Bodi hiyo hapa nchini na Korea Kusini ili kuwaongezea ujuzi katika kusimia tasnia ya filamu.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na kuweka utaratibu mzuri ambao utasaidia wadau wa filamu kutengeneza filamu zao kwa gharama nafuu, huku akiwaalika wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo, Dkt. Kiagho Kilonzo ameeleza kuwa, Bodi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau katika kujengeana uwezo na kubadilshana uzoefu ambapo mpaka sasa Bodi imeratibu midahalo mbalimbali ambayo imewafikia wadau 750 kwa kipindi cha mwaka 2022/23 katika majukwaa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment