Habari za Punde

Kikundi cha Sanaa cha Safi Chawavutia Wengi Johannesburg

 

Baadhi ya Wasanii wa Kikundi cha Ngoma na Sarakasi cha Safi kutoka jijini Dar es Salaam wakitumbuiza wakati wa sherehe ya Mabalozi ya kuadhimisha miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuasisiwa kwake iliyofanyika Mei 27, 2023 Johannesburg Afrika Kusini.


Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (aliyevaa koti) akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waliohudhuria hafla ya Mabalozi ya kuadhimisha miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuasisiwa kwake iliyofanyika Mei 27, 2023 Johannesburg Afrika Kusini. Wa nne kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Fatma Hamad Rajab.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waliohudhuria hafla ya Mabalozi ya kuadhimisha miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuasisiwa kwake iliyofanyika Mei 27, 2023 Johannesburg Afrika Kusini. Wa tano kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Fatma Hamad Rajab (wa tatu kushoto).

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Johannesburg Afrika Kusini

Kikundi cha Ngoma na Sarakasi cha Safi kutoka jijini Dar es Salaam kimekuwa kivutio katika viunga vya jiji la Johannesburg Afrika Kusini kwa kutia fora kwa kutoa burudani safi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika Mei 25, 2023 na wakati wa sherehe ya Mabalozi ya miaka 60 ya Umoja wa Afrika tangu kuasisiwa kwake iliyofanyika Mei 27, 2023 Johannesburg Afrika Kusini.

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu anasema “Kikundi hiki kimependwa sana na watazamaji wakati wote, nilimuona Mhe. Rais Cyril Ramaphosa akirekodi kwa simu yake muda wote wakati kikundi hiki kinaonesha sarakasi pamoja na ngoma huku wakiwa wamependeza kwa mavazi yao ya kitanzania”.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa mwezi Machi 2023 wakati wa ziara yake rasmi ya kikazi nchini humo na imekuwa na faida ya kuuza utamaduni wa Tanzania katika mataifa mbalimbali ya Afrika yalihudhuria maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo yanawakilishwa na Mabalozi takriban 40 wanaowakilisha nchi zao Afrika Kusini na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa nchi hiyo.

Aidha, hafla hiyo ya Mabalozi imehudhuriwa na viongozi wa Tanzania wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Fatma Hamad Rajab pamoja na viongozi wengine kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.