Habari za Punde

UVCCM Zanzibar : Yasema Uwekezaji wa SMZ Katika Sekta ya Michezo ni Fursa kwa Vijana

Na. Is-Haka Omar - ZANZIBAR.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar umempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa juhudi endelevu za kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa, amesema kuwa Rais Dk.Mwinyi ameendelea kuimarisha sekta ya michezo ili vijana wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wa vipaji vyao kupitia sekta hiyo.

Mussa,alieleza kwamba juhudi hizo za kuwekeza katika michezo ni hatua kubwa na muhimu inayotakiwa kuthaminiwa na kupongezwa kwani, vijana wengi watapata nafasi ya kujiajiri wenyewe kupitia sekta hiyo.

“ UVCCM Zanzibar tunampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa maamuzi yake sahihi ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kujenga miundombinu rafiki ya michezo katika maeneo mbalimbali nchini.”,alisema Naibu Katibu Mkuu Mussa.

Katika maelezo yake Mussa, alifafanua kwamba ukarabati wa Viwanja vya michezo mbalimbali katika viwanja vya Taifa vya Amaan cha Unguja na Gombani kwa upande wa Pemba, ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta hiyo itakayotoa nafasi ya kuendelea kuchezwa ligi mbalimbali nchini katika mazingira rafiki.

Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu Mussa, alisema dhamira ya kufanya Mapinduzi ya kimaendeleo katika michezo ilianza kustawi pale Rais Dk.Mwinyi, alipofanya harambee ya kuchangia ligi kuu,ujenzi wa viwanja vya kisasa katika maeneo mbalimbalinchini. 

Sambamba na hayo Naibu Mussa,alieleza kwamba hatua hizo sio za kufikirika bali ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ukurasa wa 245,ibara ya 187 kipengele cha michezo vifungu vidogo vya (a) hadi (k) vinavyoeleza kwa kina dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya michezo.

Aidha, aliwasihi vijana wa makundi yote nchini kuheshimu,kuthamini,kushiriki kikamilifu masuala ya michezo pamoja  na kutunza miundombinu ya michezo ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.