DODOMA 15, JUNI, 2023 UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa
Mwaka 2023/24. Pamoja na hotuba hii, nawasilisha vitabu
vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2023/24. Taarifa zilizopo katika vitabu hivi, ndiyo msingi wa
bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 nitakayoiwasilisha katika Bunge lako
Tukufu leo alasiri.
2.
Mheshimiwa
Spika, awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kukutana
tena kwa mara nyingine katika Bunge hili baada ya majadiliano ya bajeti za
mafungu mbalimbali.
3.
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya kipekee kabisa, nitoe pongezi zangu za dhati; kwa
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa uongozi wake thabiti aliouonesha tangu alipoingia madarakani. Kupitia
uongozi wake mahiri, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali
ikijumuisha sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu wezeshi. Aidha,
Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuimarisha hali ya kisiasa nchini na mahusiano ya
kimataifa. Hakika nchi yetu imebarikiwa kuwa na Rais mwenye maono makubwa
katika kuboresha ustawi wa maendeleo wa nchi pamoja na watu wake. HAKIKA
MAMA HANA BAYA.
4.
Mheshimiwa
Spika, napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
uongozi wao mahiri na jitihada zao katika kuhakikisha Taifa letu linakuwa na
maendeleo endelevu.
5.
Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Mahakama
ya
Tanzania na mhimili mzima wa utoaji wa haki kwa kazi
nzuri wanayoifanya. Aidha, pongezi za pekee ziwaendee Wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi na hivyo
kuwezesha shughuli za kiuchumi nchini kufanyika kwa amani, usalama na utulivu.
6.
Mheshimiwa
Spika, vile vile naomba nikupongeze wewe binafsi, na Mheshimiwa Mussa Azan
Zungu (Mb.), Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa Najma Murtaza
Giga (Mb), Mheshimiwa Sillo Daniel Baran (Mb) na Mheshimiwa David Mwakiposa
Kihenzile (Mb) kwa kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa weledi mkubwa. Aidha,
napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mheshimiwa
Sillo Daniel Baran (Mb) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua
(Mb.) kwa ushauri wao mahiri wakati wa uandaaji wa taarifa nilizowasilisha
mbele ya Bunge lako Tukufu leo hii. Maoni na ushauri wao umezingatiwa
kikamilifu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24 ambao
utekelezaji wake utaanza tarehe 01 Julai, 2023.
7.
Mheshimiwa
Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika nafasi ya Waziri
wa Fedha na Mipango. Ninamuahidi kuwa nitaendelea kutekeleza wajibu wangu na
kufanya kazi kwa uaminifu, ufanisi na weledi mkubwa ili kutimiza matarajio yake
aliyonayo kwangu na Wizara ya Fedha na Mipango. Ninawashukuru pia, wanachama
wenzangu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna tunavyoendelea kushirikiana
katika kukiimarisha zaidi chama chetu na kuhakikisha tunatekeleza yale yote
yaliyokusudiwa katika Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/22 – 2025/26 na Ilani ya Chama cha
Mapinduzi. Aidha, kipekee napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Iramba
Magharibi kwa kuzidi kunitia moyo na kushirikiana nami katika utekelezaji wa
majukumu yangu ya kila siku.
MWENENDO WA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2022
Uchumi wa Dunia
8. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2023 inaonesha kuwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imepungua kutoka asilimia 6.3 mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 mwaka 2022. Upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa China na India; madhara ya janga la UVIKO-19; vita kati ya Urusi na Ukraine; na sera za kupunguza ukwasi katika chumi za Ulaya ili kukabiliana na mfumuko wa bei.
Aidha, Uchumi wa dunia unatarajiwa kupungua zaidi na
kufikia ukuaji wa asilimia 2.8 mwaka 2023 kutokana na kuendelea kwa vita kati
ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya Tabia Nchi na Sera za Marekani kuongeza
riba.
Uchumi wa Afrika na Kikanda
9. Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ulipungua kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2021. Aidha, ukuaji wa Pato la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ulikua kwa wastani wa asilimia 4.1 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.3 mwaka 2021. Vile vile, wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa ni asilimia 5.3 mwaka 2022 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2021. Upungufu huo ulitokana na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine uliyosababisha mfumuko wa bei za nishati ya mafuta na vyakula.
Uchumi wa Taifa
Pato la Taifa
10. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2022, thamani halisi ya Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 lilifikia shilingi trilioni 141.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 135.5 mwaka 2021. Aidha, kiwango halisi cha ukuaji wa pato la Taifa kilifikia asilimia 4.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2021. Kiwango hicho cha ukuaji kilitokana na: mikakati iliyochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za vita nchini Ukraine; uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi; na kuongezeka kwa shughuli za utalii. Sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji kwa mwaka 2022 ni pamoja na: sanaa na burudani (asilimia 19.0); madini (asilimia 10.9); fedha na bima (asilimia 9.2); malazi na huduma ya chakula (asilimia 9.0); na umeme (asilimia 7.6). Aidha, kutokana na hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali thamani ya Pato ghafi la Taifa linatarajiwa kufikia dola za Marekani bilioni
85.42 mwaka 2023/24.
11. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2022, Pato
ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi trilioni 170.3 (sawa
na Dola za Marekeni bilioni 77.6) ikilinganishwa na shilingi trilioni 156.4
mwaka 2021 (sawa na Dola za Marekani billioni 69.94). Aidha, kwa mujibu wa
Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa
59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu 57,724,380 mwaka 2021.
Hivyo, Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capita) kwa mwaka 2022 lilikuwa shilingi
2,844,641 ikilinganishwa na shilingi 2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la
asilimia 5.0. Kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa
mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021. Hali hii
inaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini.
Mwenendo wa Mfumuko wa Bei
12. Mheshimiwa
Spika, mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa ndani ya lengo la wigo wa kuwa
chini ya asilimia 5. Mwaka 2022, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia
4.3 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021. Aidha, mfumuko wa bei
hadi mwezi Mei, 2023 umebaki kama ilivyokuwa katika kipindi hicho hicho mwaka
2022 ikiwa ni wastani wa asilimia 4.0. Hali hii imesababishwa na kuongezeka kwa
uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma; na kuongezeka kwa upatikanaji wa
mazao ya chakula katika baadhi ya maeneo nchini na nchi jirani kulikosababishwa
na upatikanaji wa mvua katika maeneo yanayotegemea mvua.
Ujazi wa Fedha
13. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kukabiliana na hatari ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei linalotokana na mitikisiko ya kiuchumi duniani bila kuathiri kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Kutokana na utekelezaji wa sera hiyo, ukuaji wa ujazi wa fedha ulikuwa ndani ya malengo ambapo katika kipindi kilichoishia Aprili 2023, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 17.2 na kufikia shilingi bilioni 39,961.5 kutoka shilingi bilioni 34,087.8 mwezi Aprili 2022. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa asilimia 15.6 hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 31,048.8 mwezi Aprili 2023 kutoka shilingi bilioni 26,861.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Mwenendo wa Viwango vya Riba
14. Mheshimiwa
Spika, viwango vya riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi
kwa mwaka 2023 vimeendelea kupungua na kufikia wastani wa asilimia 15.91 mwezi
Aprili 2023 ikilinganishwa na asilimia 16.31 Aprili 2022. Vilevile, wastani wa
viwango vya riba za amana za muda maalumu na za mwaka mmoja ulipungua hadi
asilimia 6.79 kutoka asilimia 6.81 mwaka 2022. Mwenendo huu ulichagizwa na
utekelezaji madhubuti wa sera wezeshi ya Fedha.
Sekta ya Nje
15. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwezi
Julai 2022 hadi Aprili 2023, urari wa malipo yote ya nje ulikuwa na nakisi ya
dola za Marekani milioni 4,414.2. ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani
milioni 2,516.1 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Hii ilichangiwa na kuongezeka
kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kutokana na
athari hasi za kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na ugavi wa bidhaa duniani
ikilinganishwa na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Urari wa
biashara ya bidhaa ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 6,065.6 kwa
kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na nakisi ya dola
za Marekani milioni 3,556.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.
16.
Mheshimiwa
Spika urari wa biashara ya huduma ulikuwa na ziada ya dola za Marekani
milioni 2,198.7 kwa kipindi cha mwezi
Julai 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni
1,585.1 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 38.7. Hii ilitokana na kuongezeka kwa
mapato yatokanayo na shughuli za utalii na usafirishaji kulikosababishwa na
kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia kutokana na kupungua kwa athari za
UVIKO-19. Vile vile, urari wa biashara ya bidhaa na huduma ulikuwa na nakisi ya
dola za Marekani milioni 3,866.9 kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili
2023 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 1,971.7 kwa kipindi
kama hicho mwaka 2022.
Akiba ya Fedha za Kigeni
17. Mheshimiwa
Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi
mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Hadi kufikia
Aprili 2023, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 4.88
ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi
cha takriban miezi 4.4. Mahitaji ya nchi kisheria ni kuwa na kiasi cha fedha za
kigeni kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa
muda usiopungua miezi 4.0.
Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
18. Mheshimiwa Spika,
thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za nchi washirika wakuu wa
kibiashara imeendelea kuwa tulivu, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za
kiuchumi duniani hususan ongezeko la bei za bidhaa. Hali hii imetokana na
utulivu wa mfumuko wa bei nchini ukilinganishwa na nchi washirika wetu wa
kibiashara, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na uwepo wa chakula
cha kutosha nchini. Katika mwezi Aprili, 2023 dola moja ya Marekani
ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,324.07 ikilinganishwa na shilingi
2,322.16 kipindi kama hicho mwaka 2022. Aidha, katika kipindi cha kuanzia
Aprili 2022 hadi Aprili 2023 dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa
shilingi 2,310.14.
Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
19. Mheshimiwa
Spika, sekta ya benki nchini imeendelea kubaki imara, himilivu na yenye
kutengeneza faida ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha katika kutoa mikopo kwa
sekta za uchumi na kupunguza umaskini. Mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka
kufikia shilingi bilioni 28,702.95 kwa mwaka ulioishia Aprili 2023 kutoka
shilingi bilioni 23,422.5 Aprili 2022 sawa na ongezeko la asilimia 22.5. Aidha,
ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulifikia wastani wa asilimia 15.8 katika kipindi
cha Aprili 2022 hadi Aprili 2023 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 9.1
katika kipindi kama hicho mwaka 2022 na lengo la asilimia 10.7 kwa mwaka
2022/23. Ukuaji huu umechochewa na
utekelezaji wa sera wezeshi za fedha na bajeti, pamoja na hatua zilizochukuliwa
na Serikali ikiwemo ulipaji wa malimbikizo ya madai na jitihada nyingine za kuboresha mazingira ya
biashara na uwekezaji, hali iliyochochea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi
nchini. Aidha, kiwango cha mikopo chechefu kiliendelea kupungua na kufikia
wastani wa asilimia 5.5 Aprili, 2023 kutoka asilimia 8.3 Aprili, 2022.
20. Mheshimiwa
Spika, utendaji wa sekta ndogo ya bima ulikuwa wa kuridhisha ambapo
hadi kufikia Machi 2023, iliandikisha na kutoa leseni 1,196 zikijumuisha
kampuni za bima, kampuni za uwakala na wadau wote wanaohusika na biashara ya
bima nchini. Aidha, kwa upande wa sekta ndogo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana,
mtaji wa soko la hisa kwa kampuni za ndani, uliongezeka kwa asilimia 16.97
Machi 2023 na kufikia shilingi trilioni 10.82 ikilinganishwa na shilingi
trilioni 9.25 katika kipindi kilichoishia Machi 2022. Vilevile, uwekezaji kwenye Mifuko ya UTT AMIS uliongezeka na kufikia shilingi
trilioni 1.44 katika kipindi kilichoishia Machi 2023, ikilinganishwa na
shilingi bilioni 852.21 katika kipindi kilichoishia Machi 2022 sawa na ongezeko
la asilimia 69.17.
21. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia
Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha
ambapo hadi kufikia Machi, 2023, ilitoa jumla ya leseni 1,187 kwa Watoa huduma
daraja la pili ikilinganishwa na jumla ya leseni 736 zilizotolewa Machi 2022,
leseni 780 kwa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo ikilinganishwa na leseni
615 zilizotolewa machi 2022 nakusajili vikundi 37,937 vya kijamii vya huduma
ndogo za fedha ikilinganishwa na vikundi 24,835 vilivyokuwepo Machi 2022.
Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa mafunzo kwa waratibu 115 wa biashara
ya huduma ndogo za fedha kutoka katika mikoa 13 mwezi Mei, 2023. Vilevile,
watoa huduma ndogo za fedha Daraja la Pili walikopeshwa mikopo yenye thamani ya
shilingi bilioni 870 kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.
Deni la Serikali
22. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi
Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 79,100.19 sawa na
ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 69,440.01 kwa
kipindi kama hicho mwaka 2022. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi
bilioni 51,162.60 na deni la ndani ni Shilingi bilioni 27,937.59. Ongezeko la
deni limetokana na: kupokewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli,
viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya. Aidha, Tathmini ya uhimilivu wa deni
la Serikali iliyofanyika Desemba, 2022 imeonesha kuwa deni ni himilivu na
viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha
muda mfupi, wa kati na mrefu.
23. Mheshimiwa
Spika, mnamo Machi 2023, kampuni
za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilianza zoezi la kuifanyia nchi
tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa. Zoezi hilo
lilikamilika ambapo kampuni ya Moody’s Investors Service ilichapisha matokeo ya
tathmini hiyo mwezi Mei 2023 na kampuni ya Fitch Ratings mwezi Juni 2023. Kwa
mujibu wa matokeo hayo, Tanzania imewekwa katika daraja la B2 POSITIVE na
Kampuni ya Moody’s Investors Service na daraja la B POSITIVE na Kampuni ya
Fitch Ratings ambayo yanaashiria taswira chanya kwa nchi kimataifa. Pamoja na
mambo mengine, matokeo hayo yamechangiwa na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi,
usimamizi makini wa deni la Taifa, kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa
sekta binafsi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kuleta maridhiano
ya kisiasa ndani ya nchi. Kukamilika kwa zoezi hilo, kutaiwezesha nchi kutambulika katika masoko
ya fedha ya kimataifa na hivyo, kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa
Serikali na sekta binafsi.
24. Mheshimiwa Spika, maelezo ya
kina kuhusu taarifa ya hali ya uchumi yanapatikana katika Kitabu cha Hali ya
Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022.
MAFANIKIO YA
UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2022/23
25. Mheshimiwa
Spika, kama unavyofahamu Serikali imekuwa ikitekeleza Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 ambao ni
wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano 2021/22 – 2025/26, wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa
Maendeleo ya Watu. Utekelezaji
wa Mpango huu umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na uongozi mahiri wa
Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha
Julai 2022 hadi Aprili 2023 katika sekta mbalimbali ni pamoja na:
(i)
Miundombinu
ya Reli: Kuendelea na ujenzi wa njia ya Reli ya Kati kwa Kiwango cha
Kimataifa ambapo kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) utekelezaji
umefikia asilimia 98.14; kipande cha Morogoro
–
Makutupora (km 422) utekelezaji umefikia asilimia
93.83; kipande cha Makutupora - Tabora (km 371)
asilimia 7.0; kuanza kwa ujenzi wa kipande cha Tabora - Isaka (km 165) ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 2.39; na ujenzi wa kipande cha Mwanza - Isaka (km
341) umefikia asilimia 31.07. Aidha, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja
na: kukamilika kwa ununuzi wa mabehewa 22 ya abiria kwa ajili ya reli ya kati;
kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa 52 ya mizigo na mabehewa sita (6) ya
abiria na kuanza kutoa huduma katika reli ya kati; na kukamilika kwa uboreshaji wa mfumo wa
mawasiliano na umeme katika njia ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
(ii)
Mradi wa
Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Utekelezaji wa mradi kwa
ujumla umefikia asilimia 86.89 ambapo ujenzi wa handaki la kuchepusha maji
(diversion tunnel) na ujenzi wa kingo ndogo za juu na chini umekamilika. Aidha,
ujenzi wa ukuta wa bwawa kuu umefikia asilimia 94.85, handaki la kupeleka maji
kwenye mitambo (power waterway) (asilimia 99.08), jengo la mitambo (power
house) (asilimia 68.30), kituo cha kupokea na kusafirishia umeme (switchyard)
(asilimia
98.87), kingo saidizi za kuzuia maji yasitoroke
(asilimia 84.47). Vile vile, zoezi la ujazaji maji katika bwawa linaendelea
ambapo hadi tarehe 23 Mei, 2023, kimo cha maji ya bwawa kimefikia mita 160.51
ambapo ili kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini cha maji kinatakiwa
kufikia mita 163 kutoka usawa wa bahari.
(iii)
Uboreshaji
wa Shirika la Ndege Tanzania: Kufanyika kwa sehemu ya malipo ya ununuzi wa
ndege nne (4) ambazo ni ndege moja (1) aina ya Boeing 767-300F ya mizigo
iliyowasili tarehe 03 Juni, 2023, ndege mbili (2) aina ya Boeing 737-9 Max
zinazotarajiwa kuwasili Agosti 2023 na Desemba 2023 na ndege moja (1) aina ya
Boeing 787-8 Dreamliner inayotarajiwa kuwasili Februari, 2024; na kuendelea na
ukarabati wa miundombinu katika karakana ya KIMAFA katika Kiwanja cha Ndege cha
Kilimanjaro (KIA) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 85.0. Aidha, ATCL
imeendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga katika vituo 24 ambapo vituo 14 ni
vya ndani ya nchi na vituo 10 ni vya nje ya nchi. Vituo vya ndani ya nchi ni
Arusha; Bukoba; Dar es Salaam; Dodoma; Geita; Kilimanjaro; Kigoma; Songwe;
Mpanda; Mtwara; Mwanza; Songea; Tabora na Zanzibar na vituo vya nje ya nchi ni:
Bujumbura; Entebbe, Hahaya; Guangzhou; Harare; Lubumbashi; Lusaka; Mumbai;
Nairobi na Ndola.
(iv)
Miradi ya
Umeme: Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme
nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji wa umeme. Sekta hii ni wezeshi katika uzalishaji viwandani, kukuza
biashara na kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini. Hadi Mei 2023
uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme
iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa ulifikia MW 1,872.05, sawa na ongezeko la
asilimia 10.5 ikilinganishwa na MW 1,694.55 zilizokuwepo mwaka 2021/22. Aidha,
hatua zilizofikiwa katika utelekezaji wa
baadhi ya miradi
ya umeme ni pamoja na: kukamilika kwa mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I Extension – MW 185
ambapo mitambo yote minne (4) yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 185 imewashwa
na umeme huo kuingizwa katika Gridi ya Taifa; na kufikia asilimia 99 ya
utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji Rusumo (MW 80). Kwa upande wa miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha na kusambaza
umeme, Serikali imeunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kutokea kituo
cha Nyakanazi na imeunganisha Wilaya za Ngara na Biharamulo kwenye kituo cha
gridi ya Taifa cha Nyakanazi. Aidha, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka
JNHPP hadi Chalinze umefikia asilimia 93.5 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme
cha Chalinze umefikia asilimia 64. Vile vile, hadi Mei, 2023 jumla ya vijiji
10,127 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara sawa na asilimia
82.21 vimeunganishwa na huduma ya umeme.
(v)
Ujenzi na
Ukarabati wa Viwanja vya Ndege: Kukamilika kwa upanuzi wa maegesho ya
ndege, uzio wa kiwanja, maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege Mwanza;
kukamilika kwa upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara na Songea;
Kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na kufungwa kwa mfumo
wa kuongozea ndege katika kiwanja cha Ndege Dodoma; na kukamilika kwa ujenzi wa
kiwanja cha Ndege cha Geita. Shughuli zinazoendelea ni pamoja na: ujenzi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Awamu ya Kwanza inayohusisha ujenzi
wa njia ya kuruka na kutua ndege pamoja na jengo la abiria ambapo utekelezaji
umefikia asilimia 18; Kiwanja cha Ndege Iringa (asilimia 50), Songwe (asilimia
98) na Musoma (asilimia 47). Aidha, kazi nyingine zilizofanyika ni kuanza
maaandalizi ya ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma,
Tabora na Sumbawanga.
(vi)
Uendelezaji
wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: kuendelea na zoezi la uchimbaji na
upanuzi wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli hadi kufikia kina
cha mita 15.5 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 96. Bandari ya Tanga: kuendelea na
uboreshaji wa Bandari katika awamu ya pili ambapo utekelezaji wake umefikia
asilimia 99. Bandari za Maziwa Makuu:
Ziwa Victoria: Kuendelea na
maandalizi ya awali ya ujenzi wa Bandari za Bukoba na Kemondo Bay; na kuendelea
na hatua za mwisho za kufanya usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya
Mwanza North ikijumuisha miundombinu
ya Reli (SGR). Ziwa Tanganyika:
kukamilika kwa ujenzi wa Gati katika Bandari mpya ya Karema; na kuendelea na
usanifu wa ujenzi wa jengo la abiria (Passenger
Lounge) na ukuta wa mizigo wa Lighter
Quay katika Bandari ya Kibirizi na gati la Bandari ya Ujiji ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 69. Ziwa
Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa sakafu ngumu katika bandari ya Kiwira na
Itungi; kuendelea na ujenzi wa sehemu ya kuegesha meli (ramp) katika bandari ya
Kiwira; na kukamilika kwa ujenzi wa sehemu ya kuegesha meli katika bandari ya
Ndumbi.
(vii) Kuboresha
Huduma za Usafiri na Usafirishaji wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu
Kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa
kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 83; kuendelea na ukarabati wa meli ya MV Umoja na
MT Sangara ambapo utekelezaji umefikia asilimia 75.8 na 90.7 mtawalia;
kukamilisha taratibu za kupata Mkandarasi wa ujenzi wa meli mpya tatu (3)
pamoja na chelezo ambapo meli mbili (2) zitajengwa katika Ziwa Tanganyika, meli
moja (1) Ziwa Victoria na Chelezo Ziwa Tanganyika.
(viii) Barabara na Madaraja Makubwa: Kuendelea
kuboresha mtandao wa barabara nchini kwa kujenga barabara za mikoa na barabara
zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na barabara za mijini na vijijini.
Miradi ya barabara iliyokamilika ni pamoja na: ujenzi wa barabara kwa kiwango
cha zege sehemu za Lusitu – Mawengi (km 50); Moronga – Makete (km 53.5); na
Kisorya - Bulamba (km 51). Aidha, ujenzi wa madaraja ya Tanzanite (Dar es
Salaam), Wami (Pwani), Kiyegeya (Morogoro) na Kitengule (Kagera) umekamilika.
Vile vile, ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa km 3.2
unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 72.
Kwa upande wa barabara za vijijini na mijini
zinazosimamiwa na TARURA, jumla ya kilometa 163.83 za lami, kilometa 4,724.15
za changarawe madaraja 75 na makalvati 95 yamejengwa. Aidha, barabara zenye
urefu wa kilometa 14,826.35 zimefanyiwa matengenezo.
(ix)
Huduma za
Afya: Serikali imeendelea kuboresha huduma
za kibingwa nchini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake ambapo jumla
ya wagonjwa 25 wamepatiwa huduma ya upandikizaji wa uroto katika hospitali za
Muhimbili na Benjamin Mkapa. Upatikanaji wa huduma hii hapa nchini umepunguza
gharama za kupata huduma nje ya nchi kutoka shilingi milioni 250 hadi kufikia
milioni
70 sawa na punguzo la asilimia 72 ya gharama
zilizohitajika; kuanza kutoa huduma za kibingwa ya kibobezi ya kupunguza uzito
kwa kuweka puto
(Intragastric ballon) katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili – Mloganzila ambapo jumla ya wagonjwa 87 wamepatiwa huduma hiyo;
na kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha
upandikizaji viungo na ukarabati wa wodi za watoto mahututi (NICU) katika
hospitali ya Muhimbili – Mloganzila.
Kwa upande wa hospitali
za rufaa za kanda mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa
ukarabati na upanuzi wa majengo ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya
Bugando; kuendelea na ujenzi wa jengo la huduma za tiba - mionzi kwa magonjwa
ya saratani katika hospitali ya KCMC; na kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa
jengo la wagonjwa mahututi (ICU), jengo la huduma za dharura (EMD), chumba cha
tiba mtandao, katika hospitali ya rufaa Mbeya.
Kwa upande wa
hospitali za rufaa za mikoa
mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya OPD,
afya ya uzazi, EMD, ICU, upasuaji, mifupa, wodi, sehemu ya kufulia, damu salama
na kichomea taka katika hospitali ya Njombe; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la
huduma za afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi
(asilimia 94) katika hospitali ya Simiyu; na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la
afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi katika
hospitali ya Geita ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kufikia ngazi za chini
ambapo inaendelea na: ujenzi wa hospitali 59 na ukarabati wa hospitali kongwe
19 za Halmashauri; ukamilishaji wa zahanati 300 katika halmashauri 184; na
ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya 150, zahanati 300, na hospitali za
Halmashauri
71.
Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za bima za afya, idadi ya watanzania wanaopata huduma za
bima ya afya imeongezeka kutoka asilimia 21.2 mwaka 2019/20 hadi asilimia 30.6
mwaka 2021/22.
(x)
Elimu: Kuendelea
na utekelezaji wa programu ya Elimumsingi na Sekondari Bila Ada ambapo jumla ya
shilingi 295.3 zimetolewa; kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 652.1 kwa wanafunzi 202,877 wa elimu ya juu; kukamilika kwa ujenzi wa
madarasa 8,000 ya shule za sekondari katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara;
kuendelea na ukamilishaji wa madarasa 1,072 ya shule kongwe za msingi;
kuendelea na ukamilishaji wa maboma 809 ya madarasa ya shule za msingi;
kuendelea na ukamilishaji wa vyumba 271
vya maabara za Sayansi katika Shule za sekondari; na kuendelea na ukarabati na
ujenzi wa vyuo 14 vya maendeleo ya wananchi (FDCs) na vyuo vikuu.
(xi)
Maji
Mijini na Vijijini: Hali ya upatikanaji wa maji nchini inaendelea kuimarika
ambapo kwa upande wa vijijini wastani wa upatikanaji wa maji umefikia asilimia
77.0 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 70.1 mwaka 2020. Aidha, kwa upande
wa mijini hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi imeongezeka kutoka asilimia
84 mwaka 2020 hadi asilimia 88.0 mwaka 2022. Vile vile, jumla ya miradi 586 yenye
vituo 5,748 vya kuchotea maji vinavyonufaisha wananchi wapatao 4,086,442 kwenye
vijiji 1,293 imekamilika. Kadhalika, uchimbaji wa visima vitano (5) katika jiji
la Dodoma, ujenzi wa choteo jipya katika mradi wa maji na usafi wa mazingira
mji wa Kigoma, awamu ya kwanza ya mradi wa uboreshaji maji katika miji ya Tinde
na Shelui, ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni 15 katika eneo la
Kisarawe II na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji katika eneo la Kimbiji
umekamilika. Ujenzi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira Arusha unaendelea
ambapo utekelezaji umefikia asilimia 92.67; Mugango – Kiabakari - Butiama
(asilimia 79); na mradi wa majisafi na usafi wa mazingira katika mji wa Lindi
(asilimia 71).
(xii) Kilimo, Mifugo
na Uvuvi
Kilimo: kuzalishwa
na kusambazwa kwa tani 1,004 za mbegu bora za ruzuku za Alizeti kwa wakulima
katika wilaya 39 za mikoa ya Dodoma, Kagera, Mbeya, Mwanza na Singida;
kuzalishwa na kusambazwa kwa tani 80 za mbegu bora za ruzuku za ngano katika
halmashauri ya wilaya ya Makete; kutolewa na kusambazwa kwa tani 449,795 za
mbolea ya ruzuku kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini; kubainisha
mashamba makubwa (Block farms) yenye ukubwa wa ekari 264,841.50 kwa ajili ya
vijana katika mikoa ya Kigoma (ekari 36,719.75) Mbeya (ekari 52,165), Njombe
(ekari 87,000), Dodoma (ekari 33,4543), Singida (ekari 50,000) na Kagera (ekari
5,503.75); kununuliwa kwa viuatilifu lita 106,000 za kudhibiti visumbufu vya
milipuko ya viwavijeshi na lita 82,124
zimesambazwa katika Halmashauri 58 za Mikoa ya Manyara, Singida, Tabora,
Katavi, Tanga, Geita, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma;
kukamilika kwa ujenzi wa vihenge 20 na maghala manne (4) katika Wilaya za Babati,
Mpanda na Sumbawanga; kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula - NFRA
kununua mahindi tani 17,257.857 na mtama tani 1,036.457 na Bodi ya Mazao
Mchanganyiko – CPB kununua mahindi tani
34,484, alizeti tani 2,776, mafuta ghafi tani 85.82, mchele tani 1,797, ngano
tani 277, maharage tani 406, mtama tani 3,035.06, maharage ya soya tani 393,
maharage ya njano tani 30, korosho ghafi tani 523, na mpunga tani 7,065;
kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha TANECU (Newala) cha kubangua korosho
chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 za korosho kwa mwaka; na kuendelea na
ujenzi wa skimu mpya za umwagiliaji 19 kati ya 25 zenye ukubwa wa hekta
45,564.
Mifugo:
Kukamilika kwa ujenzi wa majosho 97 na kuendelea na ujenzi wa majosho 160
kwenye mamlaka 83 za serikali za mitaa; kununuliwa kwa lita 52,560 za dawa ya
kuogesha mifugo kwa ajili ya majosho 2,644 na kusambazwa kwenye mashamba ya
Wizara na Taasisi zake; kuwezesha upatikanaji na usambazaji wa chanjo za mifugo
dozi 679,827,610 za magonjwa mbalimbali ya kipaumbele; kununuliwa kwa mitamba
1,160 na kununuliwa kwa matrekta 3, Bailer 5, mower 5 na Hay rake 5 na
kusambazwa katika mashamba ya serikali; kuhimilisha ng’ombe 60,697 kupitia
kambi za uhimilishaji; kuzalishwa kwa jumla ya dozi 116,558 za mbegu za mifugo
katika kituo cha NAIC kwa ajili ya uhimilishaji; kununuliwa kwa magari 13
yakiwemo Toyota Hard Top (2) na Toyota Double Cabin (11) na pikipiki 1200 kwa
ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za ugani katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa 184; kujengwa kwa minada 19 na kukarabati minada minne (4) katika maeneo
mbalilmbali nchini; kuendelea na ujenzi wa mabwawa 11 katika maeneo mbalimbali
nchini; kununuliwa kwa tani 8.56 za mbegu za malisho na vipando vya miti
malisho 18,025 kutoka mashamba ya Serikali na binafsi na kusambazwa kwa
wafugaji; na kuanzishwa kwa vituo nane (8) vya uwekezaji vya vijana vyenye
uwezo wa kuchukua jumla ya vijana 240 kwa mwaka kwa lengo la kuwawezesha vijana
kupata uzoefu katika kuanzisha na kuendesha miradi ya ufugaji kibiashara,
ambapo jumla ya vijana 238 wamesajiliwa katika vituo Atamizi vya LITA na
TALIRI.
Uvuvi:
Kuendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko – Lindi ambapo usanifu wa
kina umekamilika na kuanza uchimbaji; kuendelea na taratibu za ununuzi wa meli mbili (2) za uvuvi wa Bahari
Kuu zenye vifaa vya kisasa; kukamilika kwa ujenzi wa Maabara ya Utafiti wa
Uvuvi katika kituo cha TAFIRI - Dar es Salaam; kukamilika kwa ukarabati wa
mabwawa makubwa matatu (3) na madogo sita (6) katika Kituo cha Rubambagwe
(Geita); kuendelea na ujenzi wa mashamba darasa sita (6) ya ufugaji wa samaki
katika Halmashauri za wilaya za Kongwa, Iringa, Njombe, Songea, Tandahimba na Ruangwa; kukamilika kwa taratibu za
ununuzi wa boti za uvuvi 158 ikiwa ni awamu ya kwanza kwa ajili ya kukopesha
wavuvi; kuvunwa kwa tani 426,555.46 za samaki zenye thamani ya Shilingi
trilioni 2.86; kuuzwa nje ya nchi kwa
jumla ya tani 29,466.98 za mazao ya uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni
453.8 na idadi ya samaki hai wa mapambo 150,308 wenye thamani ya shilingi bilioni
1.82; na kuendelea na tafiti mbalimbali za kujua uwingi, aina, bioanuwai na
mtawanyiko wa samaki kwenye Maziwa, Bahari na Mabwawa.
(xiii) Madini: Kusainiwa kwa mikataba ya
uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini muhimu na madini mkakati na kampuni tatu
(3) kutoka Australia yenye thamani ya dola za Marekani milioni 667; ununuzi wa
mawe mawili (2) makubwa ya madini ya Tanzanite yenye jumla ya uzito wa kilo
5.22 kutoka kwa mchimbaji mdogo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.24;
kununuliwa na kusimikwa
(commissioning)
kwa vifaa vya utafiti wa jiosayansi na
vifaa vya maabara na uchunguzi; ununuzi wa mitambo
mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo; ununuzi wa mitambo
miwili (2) ya uzalishaji wa mkaa mbadala na utengenezaji wa mkaa unaotokana na
makaa ya mawe; na kuendelea na ujenzi
wa jengo la kuhifadhia sampuli za miamba choronge (core shade) eneo la Kizota - Dodoma ambapo utekelezaji wake
umefikia asilimia 75.
(xiv) Habari, Mawasiliano na TEHAMA:
Kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi mpya wa Kilomita 1,600 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na
vituo 15 vya kutoleo huduma za Mkongo; kuendelea na ujenzi wa njia mpya za
mkongo wa Taifa wa mawasiliano wenye jumla ya kilomita 4,442; kukamilika kwa
uboreshaji wa programu ya Mfumo wa Kidijitali wa Anwani za Makazi; na kukamilika kwa uhakiki wa taarifa za
miundombinu ya Anwani za Makazi pamoja na taarifa za makazi zilizokusanywa
katika Operesheni Anwani za Makazi kwenye Halmashauri 23.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa
kuongeza upanuzi na usikivu wa shirika la utangazaji TBC ambapo shughuli
zilizotekelezwa ni pamoja na: kukamilika kwa taratibu za ununuzi za kuwapata wazabuni
kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa usikivu redio zinazomilikiwa na
TBC katika maeneo tisa (9); na kuendelea na ujenzi wa makao makuu ya TBC Jijini
Dodoma.
(xv) Maliasili na Utalii: Kuimarisha
miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi na kutangaza vivutio vya utalii kupitia
programu maalum ya Tanzania - the Royal
Tour imewezesha kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watalii wa ndani na
kimataifa waliotembelea maeneo ya hifadhi na Makumbusho ya Taifa kutoka watalii
1,711,625 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,818,180 mwaka 2022 sawa na ongezeko
la asilimia 123. Katika ongezeko hilo idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka
kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,454,920 mwaka 2022
sawa na asilimia 57.7 na watalii wa ndani wameongezeka kutoka watalii 788,933
mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022 sawa na asilimia 199.5. Aidha, mapato
yatokanayo na watalii wa kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni
1,310 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 2,527.72 kwa mwaka 2022
sawa na asilimia 93. Vile vile, Serikali imeimarisha ulinzi na uhifadhi wa
rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara na
uvunaji haramu wa mazao ya misitu.
(xvi) Uwekezaji, Viwanda na Biashara: Serikali
imeendelea na juhudi mbalimbali za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji nchini kwa
kufanya mapitio ya Sera mbalimbali ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji
Tanzania ya Mwaka 2022, kuendelea na uwekaji wa miundombinu wezeshi katika
maeneo maalumu ya uwekezaji na kushiriki makongamano mbalimbali ya uwekezaji
yanayofanyika ndani na nje ya nchi. Kutokana na juhudi hizo baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana ni pamoja na usajili wa jumla ya miradi mipya 240 (Wazawa 89,
wageni 94 na ubia 57) katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023
ikilinganishwa na miradi 206 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/22.
Miradi hii inatarajiwa kuwekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 4,387.17 na
kuzalisha ajira 39,245.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni: Kusajiliwa kwa
miradi mitano (5) katika vituo vya mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 15.6 inayotarajiwa kuchangia mauzo nje yenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 12.6 na kuzalisha ajira 1,247; na kukamilika kwa usimikaji wa
Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa Wawekezaji kwa Njia ya Kielektroniki
(Tanzania Electronic Investment Single Window - TeIW) awamu ya kwanza pamoja na
kuunganisha taasisi saba (7).
(xvii) Utawala Bora na Utawala wa Sheria:
katika kuhakikisha kuwa utawala bora na utawala wa sheria unaendelea kushamiri
nchini, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo na miundombinu ya Kitaasisi na
utoaji haki, uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
Kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni; kuendelea na ujenzi
wa Mahakama za wilaya za Liwale ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 70, Kwimba (asilimia 80), na Ulanga (asilimia 35);
kuendelea na ujenzi wa Mahakama za
Mwanzo tisa (9) ambapo Mahakama ya Mwanzo Madale
(Dar es Salaam) utekelezaji umefikia asilimia 75,
Kinesi -
Rorya
(asilimia 99), Mahenge - Kilolo (asilimia 97), Luilo – Ludewa (asilimia 80),
Newala – Newala (asilimia 75), Usevya – Mlele (asilimia 95), Nyakibimbili
- Bukoba (asilimia 90); Kabanga – Ngara (asilimia 80) na Mlimba na Mang’ula
– Morogoro (asilimia 85); kukamilika kwa ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu
Tabora na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi; na kuendelea na Awamu ya Pili ya
ujenzi wa majengo ya Wizara katika mji wa Serikali Mtumba ambapo ujenzi wa
majengo 24 umefikia wastani wa asilimia 60 na ujenzi wa jengo moja (1) la
Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) umefikia asilimia 50 kwa lengo la kuimarisha
utoaji wa huduma kwa wananchi.
(xviii)
Utamaduni,
Sanaa na Michezo: Kutolewa mikopo kwa awamu mbili (2) yenye thamani ya
shilingi bilioni 1.07 kwa wasanii na wadau 45 katika tasnia za utamaduni na
sanaa. Aidha, Serikali imeratibu matamasha mbalimbali yenye lengo la kudumisha
urithi wa utamaduni ikiwemo: Tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika
Julai, 2022 Jijini Dar es Salaam; Tamasha la tano (5) la Utamaduni la Jumuiya
ya Afrika Mashariki, (JAMAFEST) lililofanyika Septemba, 2022 Jijini Bujumbura -
Burundi; Tamasha la 41 la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa la Bagamoyo; na
Tamasha la Msimu wa Utamaduni kati ya Tanzania na Afrika Kusini mwezi Novemba, 2022; na kuandaa na kuendesha
mashindano ya Kimataifa ya Urembo na Utanashati kwa viziwi (Miss and Mr. Deaf International
– MMDI, 2022) ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika Barani Afrika.
Aidha, timu ya mpira wa miguu ya watu wenye ulemavu
(Tembo Worriors) ilifanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya kombe la dunia kwa
watu wenye ulemavu na kuiweka nchi kwenye orodha ya timu kumi bora za dunia; na
Timu ya Taifa ya Wanawake (Serengeti Girls) kushiriki fainali za kombe la dunia
nchini India na kufikia hatua ya robo fainali mwezi Oktoba, 2022.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: Nchi
kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) mwaka 2022 uliofanyika Jijini Arusha na Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri
wa Michezo wa Baraza la Michezo la Afrika Kanda ya IV uliofanyika Jijini Arusha
ambapo Tanzania ilichaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza hilo;
na Tanzania kuwasilisha zabuni ya kuomba kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe
la Mataifa Afrika – AFCON 2027 kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda.
Aidha, kwa namna ya kipekee kabisa napenda kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa juhudi zake za kuleta hamasa kwa timu zetu katika michezo ya Kimataifa kwa
kununua kila goli linalofungwa na timu zetu zinapokuwa katika mashindano ya
Kimataifa ambapo kutokana na juhudi hizo timu ya Simba imepata shilingi milioni
55 na Yanga shilingi milioni 135. YANGA HOYEE!!. Vile vile, napenda
kutoa pongezi kwa klabu ya Simba kwa kuendelea kufanya vizuri kimataifa na
kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika. Aidha, kwa
kipekee kabisa napenda kuipongeza timu ya Yanga kwa kufika fainali ya kombe la
Shirikisho barani Afrika pamoja na kutoa Mfungaji Bora (Mayele) na Kipa Bora
(Diara). HAKIKA TIMU YA SIMBA MNA MENGI YA KUJIFUNZA KUTOKA TIMU YA YANGA.
26. Mheshimiwa Spika, maelezo ya
kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yanapatikana katika Kitabu cha
Mpango, Sura ya Pili.
27. Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa mchakato wa Maandalizi ya Dira ya Taifa 2050
ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango
tarehe 03 Aprili, 2023 Dodoma. Aidha, Serikali imepanga kuyafikia makundi yote
ya wadau katika zoezi la ukusanyaji wa maoni ili kuhakikisha Dira inakuwa na
maono jumuishi. Nitumie fursa hii, kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, maandalizi
ya Dira 2050 yanahusisha tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025, ambapo matokeo
ya tathmini hiyo yataweka msingi wa maandalizi ya Dira 2050. Hivyo, naomba
kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maandalizi ya Dira Bora kwa kizazi cha sasa
na vizazi vijavyo yanategemea ushiriki mkubwa na maoni ya Waheshimiwa Wabunge
na Watanzania wote (ikijumuisha wale waishio nje kwa maana ya Diaspora) na
Washirika wetu wa Maendeleo. Hivyo, usisite kutoa maoni yako pale utapohitajika
kufanya hivyo.
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2023/24
28. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni wa tatu katika utekelezaji wa Mpango wa
Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 –
2025/26) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo
ya Watu. Mpango umeandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26;
Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020;
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24; na Sera na
Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya Maendeleo
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050, Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) 2050, Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika na Malengo ya
Maendeleo Endelevu
2030.
29. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa
Mpango wa mwaka 2023/24, msisitizo mkubwa utawekwa katika sekta za uzalishaji
na zinazozalisha ajira zinazowagusa wananchi wengi ambazo ni kilimo, mifugo, na
uvuvi. Aidha, Mpango huu unalenga kukamilisha miradi mingi ambayo ilianza
katika utekelezaji wa mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano
(2021/22-2025/26), ambao ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira 2025. Vile
vile, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2023/24 unatarajia kuleta
matokeo chanya ikiwemo: kuimarika kwa ukuaji wa Pato la Taifa; kuimarika kwa
miundombinu ya huduma za kiuchumi na kijamii hususan afya, elimu, maji na
umeme; kudhibitiwa kwa kasi ya mfumuko wa bei; kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji
na biashara; kuvutia ushiriki wa sekta binafsi; na kuimarika kwa maisha na
ustawi wa jamii.
Malengo na Shabaha za Uchumi Jumla kwa Mwaka
2023/24
30. Mheshimiwa Spika, malengo na shabaha za
ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2023/24, ni kama ifuatavyo:
(i) Ukuaji
wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka 2023 kutoka ukuaji wa
asilimia 4.7 mwaka
2022;
(ii) Mfumuko
wa bei kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 3.0 hadi asilimia 7.0 katika kipindi
cha muda wa kati;
(iii) Mapato
ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio
ya asilimia 14.4 mwaka 2022/23
(iv) Mapato
ya kodi kufikia asilimia 12.0 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio
ya asilimia 11.5
mwaka 2022/23;
(v) Nakisi
ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa chini ya asilimia 3.0 ya Pato la Taifa
mwaka 2023/24; na
(vi) Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa
bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
31. Mheshimiwa Spika, misingi
itakayozingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni kama
ifuatavyo:
(i) Kuongezeka
kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara;
(ii) Kuendelea
kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili;
(iii) Kuendelea
kuhimili athari zitokanazo na kushuka kwa uchumi wa dunia na kuongezeka kwa bei
za bidhaa na huduma katika soko la dunia;
(iv) Kuendelea
kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini;
(v) Uwepo
wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani; na
(vi) Kuendelea
kuimarika kwa viashiria vya ustawi wa jamii.
Miradi ya Kipaumbele kwa Mwaka 2023/24
32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24,
Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo. Miradi hiyo
inajumuisha: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge
Railway - SGR); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115;
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia
kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358) na
Rumakali (MW 222) – Njombe; Daraja la JPM - Kigongo – Busisi (Mwanza); Ujenzi
wa barabara na Madaraja Makubwa; kuendeleza Kanda Maalumu za Kiuchumi ikiwemo
Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo; na Programu ya Kuendeleza Ujuzi Adimu.
33. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/24
Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia maeneo
matano (5) ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano, 2021/22 – 2025/26 kama ifuatavyo:
(a)
Kuchochea
Uchumi Shindani na Shirikishi: Katika eneo hili nguvu kubwa itaelekezwa
kwenye miradi inayolenga kuboresha miundombinu, kuimarisha mifumo ya kitaasisi
pamoja na miradi inayolenga kuleta mapinduzi ya TEHAMA. Utekelezaji wa miradi
hiyo utaimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza utulivu wa
kiuchumi. Miradi hiyo ni pamoja na:
(i)
Barabara:
miradi itakayotekelezwa ni ile inayolenga kufungua fursa za kiuchumi, za
kuunganisha Tanzania na nchi jirani pamoja na za kupunguza msongamano ikiwemo:
Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupilo - Malinyi – Londo – Lumecha/Songea (km
499); Barabara ya Ifakara - Kihansi - Mlimba - Madeke – Kibena (km 220); na
Barabara ya Makutano – Natta – Mugumu/Loliondo – Mto wa Mbu (km
235); Handeni – Kibaya – Singida (Km 460).
(ii)
Madaraja
Makubwa: kuanza ukarabati wa daraja la Kirumi (Mara); kuendelea na ujenzi
wa barabara unganishi za Daraja la Sibiti (Singida); na kuanza ujenzi wa
Madaraja ya Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro) na Mbambe (Pwani).
(iii) Usafiri wa Majini: Ujenzi na Ukarabati
wa Meli katika Maziwa Makuu ikijumuisha: Kukamilisha ujenzi wa meli mpya ya MV.
Mwanza Hapa Kazi Tu; kukamilisha ukarabati wa meli za MV Umoja na MT. Sangara;
kuanza ujenzi wa meli mpya (Wagon ferry) katika Ziwa Victoria na meli mpya
(Barge/Cargo
ship) ya kubeba shehena ya mizigo katika Ziwa
Tanganyika
(iv) Bandari: Bandari ya Dar es Salaam, kuendelea uchimbaji wa kina na upanuzi wa
lango la kuingilia na kugeuzia meli na uboreshaji wa Gati Na. 8 – 11 na
kuendelea na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati Na. 12 -15; Bandari ya Tanga, kuendelea na
uboreshaji wa Bandari ya Tanga na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya gati
la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga); Bandari ya Mtwara, kuendelea na
maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena za mizigo; Bandari ya Bagamoyo, kuanza maandalizi ya utekelezaji wa bandari;
kuendelea na uboreshaji wa Bandari za Bukoba, Kemondo Bay na Mwanza North katika Ziwa Victoria; Kuendelea na ujenzi wa
Access Road, Cargo Shed, Passenger Wharf and Lounge) pamoja na kuendelea na
ujenzi wa Passenger Lounge na ukuta wa mizigo wa Lighter Quay katika Bandari ya Kibirizi na
gati la Bandari ya Ujiji katika Ziwa Tanganyika.
(v)
Usafiri
wa Anga: Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Msalato,
Mwanza, Mtwara, Kigoma, Sumbawanga, Shinyanga, Songwe, Mpanda, Tabora, Bukoba,
Geita, Iringa, Ruvuma (Songea), Simiyu, Lake Manyara, Tanga, Moshi, Lindi na
Mara (Musoma), Dodoma, Manyara na Arusha.
(vi) Nishati: Kuendelea na utekelezaji wa
miradi ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme (nishati) ikiwemo: Kufua Umeme
wa Maji Kikonge (MW 300); Kufua Umeme wa Maji Malagarasi (MW 49.5); Uimarishaji
wa Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization); Njia ya Kusafirisha Umeme wa
Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; na Njia ya
Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 – North – West Grid Extension (Iringa –
Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi).
(vii) Mapinduzi ya TEHAMA: Kuendelea na
ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya
Anwani za Makazi na Tanzania ya Kidijitali; kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji
wa Vifaa vya TEHAMA; na ujenzi wa Kituo Kikuu na Vituo vidogo vya Kuendeleza Ubunifu katika TEHAMA.
(b)
Kuimarisha
Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Huduma: miradi itajielekeza katika kukuza
sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi. Miradi hiyo ni pamoja na:
programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili; mradi wa kuimarisha
miundombinu ya masoko ya mifugo na mazao yake; kuimarisha miundombinu ya
umwagiliaji kwa kujenga skimu mpya 25 na kukarabati skimu 30 zenye jumla ya
hekta 95,005 katika mikoa mbalimbali; na kuimarisha huduma za ugani. Aidha,
msukumo wa pekee utawekwa katika kuboresha Viwanda Vidogo – SIDO na Kiwanda cha
Mashine na Vipuri KMTC; kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi (SEZ) na kongani
za viwanda.
(c)
Kukuza
Biashara na Uwekezaji: Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara
na uwekezaji pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za
maendeleo. Kipaumbele kitakuwa katika kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango
Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Blueprint); kuboresha huduma za
biashara na masoko; kuratibu programu za kuimarisha mifumo ya udhibiti wa
uwekezaji inayolenga katika kupunguza gharama za uwekezaji nchini; na kuendelea
kuboresha na kuimarisha huduma zitolewazo kwa wawekezaji katika Kituo cha
Huduma za Mahali Pamoja.
(d)
Kuchochea
Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa imelenga kuboresha maisha ya watu
pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii. Miradi hiyo ni pamoja na: miradi ya afya kwa
kuimarisha huduma za afya katika
hospitali za kitaifa, hospitali za rufaa za kanda na mikoa; hospitali za halmashauri; vituo vya
afya na zahanati; kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi; kugharamia elimumsingi na sekondari bila ada; utoaji wa mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu; kuendelea na
ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya
mikoa na wilaya, miji midogo na vijijini; na kuendelea kupanga, kupima na
kumilikisha ardhi pamoja na kuimarisha mipaka ya kimataifa.
(e)
Kuendeleza
Rasilimali Watu: Kuendelea na utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali
ya kukuza ujuzi nchini ili kuongeza ajira kwa vijana kwa kutoa mafunzo ya
ufundi na stadi za kazi kupitia programu mbalimbali zikiwemo: kuimarisha programu ya Taifa ya kukuza ujuzi
nchini; kuboresha mfuko wa maendeleo ya vijana; kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa vituo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu; na kutekeleza Programu ya
Taifa ya Kukuza Kazi za Staha.
34. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, sekta
ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ilipewa jukumu la kugharamia
shilingi trilioni 21 sawa na asilimia 17 ya Bajeti ya kutekeleza Mpango wa Tatu
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. Katika kutekeleza
jukumu hilo la kimkakati, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na wadau
wengine imeweza kubainisha jumla ya miradi 48 inayoweza kutekelezwa kwa
utaratibu wa PPP.
35. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2023/24
miradi mikubwa ambayo ipo kwenye maandalizi ya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP
ni pamoja na: kuzalisha umeme kwa
kutumia nishati ya jua katika mikoa ya Dodoma (Zuzu MW 60) Kilimanjaro (Same MW
50) na Singida (Manyoni MW 100); Mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji wa
Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222); mradi wa miundombinu ya kusambaza gesi
katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara ;na mradi wa kusafirisha umeme
wa Tanzania – Malawi – (TAMA) interconnection
wenye urefu wa km 82.
36. Mheshimiwa
Spika, Miradi mingine ni: Reli ya Dar es Salaam (Dar -Commuter Rail);
Reli ya Mtwara-Bamba Bay; Uendeshaji wa Reli (Rolling stocks); Uendeshaji wa
Barabara ya haraka (expressway) kutoka Igawa-Tunduma; Barabara za kupunguza
msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Inner and Outer Ring Roads);
Barabara za haraka kutoka KibahaChalinze-Morogoro hadi Dodoma na kuunganisha
Jiji la Dodoma na Dar es Salaam kwa barabara za haraka; Bandari kavu katika
eneo la Kisiwa/Mgao – Mtwara; na Kuboresha na Upanuzi wa bandari katika Ziwa
Victoria - Mwanza na Nansio - Ukerewe.
37. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
Umuhimu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Serikali inaendelea na hatua
za mwisho za utekelezaji wa takwa la kisheria la kuanzisha Kituo cha Ubia
(PPP-Center) kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa jukumu hili
kubwa na la kimkakati. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2023/24, Serikali imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 2.82 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya Ubia (PPP
Faciliatation Fund-PPPFF) ili kuwezesha maandalizi ya maandiko ya miradi ya
maendeleo yenye mvuto wa uwekezaji wa sekta binafsi nchini. Vile vile, Serikali
imejipanga kukabili changamoto za kisheria, kimfumo na kiutendaji zilizochangia
kuchelewa kwa miradi ya ubia kwa zaidi
ya muongo mmoja. Katika kuhakikisha hilo, Serikali iliwasilisha muswada wa marekebisho
ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta Umma na Binafsi, Sura Na 103 ambapo tarehe 13
Juni, 2023 Bunge lako Tukufu liliuridhia na kuupitisha. Hivyo, ni rai yangu kwa
Mawaziri wenzangu na watendaji wa Serikali kutumia fursa hiyo kushirikiana na
Sekta Binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
38. Mheshimiwa Spika, maelezo ya
kina kuhusu miradi ya kipaumbele kwa mwaka 2023/24 yanapatikana katika Kitabu
cha Mpango, Sura ya Tatu.
Vihatarishi vya Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka
2023/24 na Mikakati ya Kukabiliana Navyo
39. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango
unaweza kuathiriwa na vihatarishi vya
ndani na nje. Vihatarishi hivyo ni pamoja na: mabadiliko ya viwango vya riba za
mikopo katika soko la ndani na nje; uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli
za binadamu; migogoro na hali ya siasa inayojitokeza kwa nchi jirani, kikanda
na kimataifa; na kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
40. Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari
zinazoweza kusababishwa na vihatarishi husika, Serikali inalenga kuchukua hatua
mbalimbali ikijumuisha: kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti
matumizi yasiyo ya lazima ili kupunguza utegemezi katika misaada na mikopo
kutoka nje; kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza
mazingira ili kudhibiti uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu;
kuimarisha mikakati ya kisera ili kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi
duniani; na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kugharamia shughuli za
maendeleo.
Ugharamiaji wa Mpango 2023/24
41. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2023/24 Serikali imetenga shilingi bilioni 14,077.2 kwa
ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo. Kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni 10,795.1 sawa na asilimia 77.0 ya bajeti ya maendeleo ni fedha
za ndani na shilingi bilioni 3,282.1 sawa na asilimia 23 ya bajeti ya maendeleo
ni fedha za nje. Fedha hizi zitakusanywa kutoka katika mapato ya kodi na yasiyo
ya kodi, misaada na mikopo nafuu, mikopo ya ndani na mikopo ya nje yenye
masharti ya biashara. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi
katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo kupitia utaratibu wa ubia kati ya
sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi
ya maendeleo kupitia ushiriki wa sekta binafsi.
Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango 2023/24
42. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha
kuwa mipango ya maendeleo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, suala la
ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji limeendelea kupewa
msukumo wa pekee katika shughuli za kila siku za Serikali. Katika kutekeleza
hilo, mwaka 2022/23, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na taasisi
nyingine za Serikali ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi 211 kati ya
lengo la miradi 300 iliyopangwa kufuatiliwa katika kipindi cha mwaka 2022/23.
Aidha, miradi iliyofuatiliwa ilihusisha miradi kutoka sekta za ujenzi,
uchukuzi, viwanda, elimu, afya, utawala bora, kilimo, mifugo, maji na biashara
inayotekelezwa na serikali pamoja na sekta binafsi.
43. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kuimarisha uratibu na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2023/24 kupitia Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya
Miradi ya Maendeleo wa Mwaka 2022; Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango
wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26; Mwongozo wa
Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/24; Mwongozo wa
Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma wa Mwaka 2022; Sheria ya Bajeti, Sura 439;
Mpango Kazi na Mtiririko wa Mahitaji ya Fedha; Waraka Na. 5 wa Hazina wa Mwaka
2020/21 Kuhusu Matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo
(NPMIS); na Waraka Na. 1 wa Hazina kuhusu
Utekelezaji wa Bajeti.
44. Mheshimiwa Spika, Pamoja na Sheria hizo na miongozo hiyo, Serikali pia inaendelea
na maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ambapo hatua iliyofikiwa
ni kukamilika ukusanyaji na uchambuzi wa maoni kutoka kwa wadau na kuanza kwa
uandishi wa Taarifa ya Kizio (Baseline
Report). Kukamilisha kwa uandishi wa Taarifa Kizio kutajenga msingi wa
uandishi wa Sera ambayo inatarajiwa kutatua changamoto za uratibu wa shughuli
za ufuatiliaji na tathmini chini. Aidha, shughuli ya ufuatiliaji na tathmini ni
suala mtambuka na inahusisha wadau mbalimbali katika ngazi tofauti, Serikali kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana na Wizara, Idara Zinazojitegemea,
Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na sekta binafsi katika kuratibu na
kusimamia ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.
45. Mheshimiwa Spika, Wizara, Idara Zinazojitegemea,
Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaelekezwa kuzingatia maelekezo yaliyoainishwa
katika Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi na Programu za Maendeleo wa Mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na: kuandaa Mpango
Kazi wa mwaka wa ufuatiliaji na tathmini; kutenga rasilimali fedha
zitakazowezesha shughuli za ufuatiliaji na tathmini; kuimarisha mifumo ya ndani
ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo; kufanya ufuatiliaji na
tathmini ya miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mipango kazi iliyowekwa; na
kuendelea kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya ufuatiliaji na
tathmini.
46. Mheshimiwa Spika, Serikali inazielekeza
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya
Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuaandaa taarifa za
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo na kuziwasilisha
Wizara ya Fedha na Mipango. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na
tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa husika Wizara ya
Fedha na Mipango.
MAJUMUISHO
47. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza
hapo awali, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 ni wa tatu katika
utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 –
2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa
Maendeleo ya Watu”. Utekelezaji wa Mpango utaendelea kuimarisha
mahusiano ya kisiasa, ulinzi na diplomasia ya uchumi na nchi nyingine,
kuendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya maendeleo, kuchochea uwekezaji
viwandani hususan kwa kutumia rasilimali watu na malighafi zinazopatikana kwa
wingi nchini ikiwemo mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, madini, misitu na gesi
asilia, kuimarisha viashiria vya uchumi jumla, kuboresha mazingira ya uwekezaji
viwandani ikiwemo kuimarisha majadiliano na wawekezaji wa ndani na nje pamoja
na kuendeleza mashirikiano na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
48. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kutekeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji
ili kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi, kufungua fursa zaidi za ajira na
maendeleo ya watu, kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi zikiwemo huduma za
afya, elimu, umeme na maji safi na salama mijini na vijijini pamoja na
kuimarisha miundombinu wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa ajili ya masoko ya
kimataifa hususan ya nchi jirani.
49. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na athari za
majanga mbalimbali ya asili na yasiyo ya asili yakiwemo mabadiliko ya tabianchi,
magonjwa na vita. Aidha, tutaendelea kuimarisha utekelezaji kwa kuweka mipango
madhubuti ya kupunguza athari zitokanazo na vita inayoendelea kati ya Urusi na
Ukraine ikiwemo kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa mbalimbali na kushuka kwa
kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kukabiliana na Athari za UVIKO–
19.
HITIMISHO
50.
Mheshimiwa
Spika, kwa niaba ya Serikali ninaomba kutumia fursa hii kuwashukuru wadau
wote wa maendeleo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo,
Taasisi za Elimu na Tafiti, Sekta Binafsi, Asasi za
Kiraia, Taasisi za Dini na Wananchi wote kwa namna walivyojitoa na kushiriki
kikamilifu katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na
kuimarisha uchumi wa Taifa letu. Wadau hao wamekuwa na mchango mkubwa katika
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Kwa msingi huo, ninawaomba na
kuwasihi wadau wote waendelee kushirikiana na Serikali yetu inayoongozwa na
Rais shupavu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
51.
Mheshimiwa
Spika, kipekee kabisa niwashukuru Mawaziri,
Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Viongozi wote wa Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea,
Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika
maandalizi ya taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24. Aidha, hotuba hii isingeweza kukamilika
bila jitihada kubwa zilizofanywa na watumishi wote wa Wizara ya Fedha na
Mipango. Hivyo, kwa dhati ya nafsi yangu naomba nitoe shukrani za pekee kwa
Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na
watendaji wote wa Wizara ya Fedha na
Mipango na taasisi zilizo chini ya Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Natu
El-Maamry Mwamba kwa kujitoa usiku na mchana kukamilisha kwa wakati na kwa
ubora Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Mwaka 2023/24.
52.
Mheshimiwa
Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu, napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla kwa kutenga muda wao kunisikiliza. Aidha,
napenda kuwataarifu wadau wote kuwa, hotuba hii pamoja na vitabu vya Taarifa ya
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka
2023/24 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.
53.
Mheshimiwa
Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na
kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24.
54.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment