Habari za Punde

Wadau Wapitisha Ripoti ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Jenifa Christian Omolo, akifungua warsha ya wadau kwa ajili ya kujadili na kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, Dodoma.

Na. Joseph Mahumi, WFM, Dodoma 

Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha Tanzania inatimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 (SDGs), ambayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kuondoa umasikini katika jamii.
 
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati akifungua warsha ya wadau kwa ajili ya kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, kabla ya kuwasilishwa katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani Mwezi Julai, 2023.

Serikali imewasilisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu 2030 kwa wadau kuijadili na kuipitisha kabla ya, huku wadau hao wakiipongeza Serikali kwa uwazi na kupiga hatua kubwa ya utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu 2030.

“Mchakato wa kufanya mapitio ya utekelezaji wa SDGs umekuwa shirikishi, na wa uwazi, ukishirikisha wadau wote muhimu nchini wakiwemo: Serikali Kuu; Sekta Binafsi; Asasi za Kiraia; Bunge; Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Utafiti, pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu” aliongeza Bi. Omolo.

Bi. Omolo alisema kuwa Tanzania, ilichagua kutekeleza ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu kwa kuyaasili katika mipango na mikakati ya kitaifa na ya kisekta na wakati mchakato wa kupitishwa kwa SDGs unafanyika, Tanzania ilikuwa inaandaa mpango wake wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 – kwa upande wa Tanzania Bara, na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini 2016-2020 au MKUZA III, kwa upande wa Zanzibar.
 
Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali Milanzi, amelima kuwa malengo yaliyofanikiwa katika ajenda kwa kipindi cha miaka mitano yametokana na ushirikiano wa wadau katika upatikanaji na matumizi ya takwimu.
 
“Serikali imekusudia kuimarisha zaidi upatikanaji wa takwimu ili kusaidia kurahisisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030” alisema Dkt. Milanzi.
 
Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa, Septemba 2015, zilipitisha ajenda ya 2030 ya kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo, pamoja na mambo mengine, iliainisha Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ambayo kwa kifupi yanajulikana kama SDGs.
Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa - Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mursali Milanzi, akizungumza jambo wakati wa warsha ya wadau kwa ajili ya kujadili na kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Jenifa Omolo (wa nne kulia), katika picha ya pamoja na wadau kutoka mashirikia ya Umoja wa Mataifa (UN), baada ya kufungua warsha kwa ajili ya kujadili na kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Jenifa Omolo (wa tano kulia), akiwa katika picha ya pamoja na wadau kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), baada ya warsha kwa ajili ya kujadili na kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.