Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais
Bi. Mary Maganga na Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakiwa
katika kikao na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo wa Serikali ya
Jamhuri ya Burundi Mhe. Prof Sanctus Niragira leo Juni 08, 2023 jijini Dodoma.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
Tanzania na Burundi zimekubaliana kuendeleza
ushirikiano katika kulinda rasilimali zilizopo katika Ziwa Tanganyika hatua
inayolenga kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi baina ya mataifa hayo mawili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt. Selemani Jafo mara baada ya kumalizika kwa kikao baina yake na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Burundi Mhe. Prof Sanctus Niragira kilichofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Jafo amemhakikishia Prof.Niragira kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha inasimamia kikamilifu Mkataba wa Nchi Wanachama wa Mkatataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika ili kuhakikisha rasilimali zilizomo zinaleta tija namanufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
“Namshukuru Waziri mwenzangu wa Burundi kwa kuja nchini kwetu na kuona namna bora matumizi na usimamizi wa Ziwa Tanganyika ambalo linaunganisha mataifa yetu na wannachi wetu, kikao kimewakutanisha wataalamu kutoka zetu na kwa pamoja tumejadiliana na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuhifafdhi mazingira ya ziwa letu,” amesema Dkt. Jafo.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha diplomasia katika ya nchi yetu hatua inayosaidia kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali zikiwemo za mabonde ya mito, bahari na maziwa ikiwemo Ziwa Tanganyika hatua inyozidi kuimarisha ushirikiano na mshikamano ya baina ya Tanzania na Burundi.
Kwa upande wake Waziri Mhe. Prof Niragira aliishukuru Tanzania kwa mwaliko huo huo kwa Serikali ya Burundi ambao umeleta tija katika namna ya kusimamia rasilimali za maji ikiwemo Ziwa Tanganyika ambalo linaunganisha nchi ya Burundi.
Amesema uhusiano wa nchi hizi mbilio umezidi kuimarika baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika Desemba 16, 2021 mkoani Kigoma ambao umekuza mipango ya maendeleo endelevu ikijumuisha uboreshaji wa miundombinu ya kimsingi, ufadhili wa maendeleo ya ndani na usimamizi shirikishi kupitia miradi tofauti.
Prof. Niragira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Usimamizi endelevu wa Ziwa amesema nchi yake itaendelea ksuhirikiana na Tanzania katika kusimamia rasilimaliza za Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Mkurugenzi Mtendaji wa Bonde la Ziwa Tanganyika Bw. Tusanga Mukanga Sylvain watendaji wa Ofisi hiyo pamoja na watendaji wa wizara za kisekta.
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama imeendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zinazolenga kuhakikisha usimamizi endelevu wa Rasilimali za ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za maji na Ziwa Tanganyika.
No comments:
Post a Comment