Habari za Punde

Mhe. Tabia Asisitiza Matumizi ya Lugha ya Kiswahili Sanifu

Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita akizungumza na waandishi  wa habari wakati alipokuwa akitoa taarifa kuhusiana na maadhisho ya  siku ya Kiswahili Duniani ambayo hufanyika  kila ifikapo Julai 7, huko Ofisini kwake Migombani Mjini Unguja 

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Said Yakub  akijibu baadhi ya maswali  yalioulizwa na  waandishi wa habari Wakati wa mkutano wa waandishi hao uliohusiana  na taarifa ya maadhimisho ya  siku ya Kiswahili Duniani ambayo hufanyika  kila ifikapo Julia 7,hafla iliyofanyika Ukumbi wa wizara ya Habari Migombani Mjini Unguja ,julai 03,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR

 

Na Rahma Khamis Maelezo                                    3/7/2023


Waziri wa Habari Vijana Utadumu na Michezo Zanzibar Mhe, Tabia Maulid Mwita amewataka wananchi kutumia kiswahili sanifu ili kuitunza na kuikuza lugha hiyo.


Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Migombani wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.


Amesema Kiswahili ni lugha mama inayotumika katika sehemu tofauti ndani na nje ya nchi ingawa bado kuna baadhi ya watu wanakichafua kutokana na kukitumia bila ya kuzingatia usahihi wake.


“Licha ya lugha hiyo kuendelea kutumika duniani kote lakini bado kuna mapungufu kwa baadhi ya watumiaji ,wanakiharibu na kukichafua kutokana na kukua kwa utandawazi nchini,”alisema Waziri Tabia.


Aidha amefahamisha kuwa mambo ya utandawazi yamepelekea kuharibu kiswahili hivyo wamejipanga kuhakikisha kiswahili kinatumika na kuwataka wanahabari kuhamasisha matumizi bora ya kiswahili kwani viongozi wote wakuu ni wadau wa kiswahili.


Akizungumzia kuhusu mikakati ya Serikali katika kulinda Utamaduni wa Mswahili Waziri Tabia ameeleza kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapokuja wageni wanatumia lugha rafiki ili wageni hao waweze kufuata utamaduni wa Zanzibar bila kuharibu Utalii.

Aidha amefahamisha kuwa katika kuelekea siku ya Kiswahili Duniani  , Julai 4 wanatarajia kufanya mkutano maalum na wahariri wakuu wa Vyombo vya Habari katika Ukumbi wa Idriss-Abdul Wakili Kikwajuni ambapo katika mkutano huo watajadili  Nafasi ya wahariri Wakuu katika matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari.


Katika hatua nyengine Waziri amefafanua kwamba Julai 5 kutafanyika mjadala mpana  katika Ukumbi huohuo ambapo mada kuu itakuwa ni Kiswahili ni nyenzo ya ukombozi wa fikra kwa maendeleleo ya kiuchumi Barani Afrika.


Waziri Tabia ameongeza kwa kusema kuwa Julai 6 kutafanyika matembezi yatakayoanzia Skuli ya Sekondari Dkt Shein  hadi Ukumbi wa Ziwani Polisi ambako kutafanyika ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo.


Hata hivyo Waziri huyo amewaomba wananchi kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya kiswahili ili kukitangaza na kukitumia zaidi duniani kote.


Nae Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Said Yakubu amesema ushirikiano kati yao na Zanzibar upo karibu sana  hasa katika shughuli za kiutamaduni kwani wanafanya kazi kwa pamoja na  wamekuwa wakipanga mipango ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanakwenda sawa.

 

Siku ya Kiswahili duniani huadhimishwa kila ifikapo Julai 7 ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Ziwani Polisi na kuhudhuriwa na wageni kutoka ndani na nje ya nchi ikikwemo Urusi,Ghana ,Ujerumani ,Comoro na Mombasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.