SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema utalii ni sekta kuu ya uchumi na maendeleo unaoingiza pekee 30% ya
pato la uchumi wa Zanzibar.
Akizungumza na ujumbe wa
watu saba kutoka kampuni ya ujenzi wa reli na uwekezaji ya China, Ikulu
Zanzibar, waliofika kumtembelea, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliwakaribisha wawekezaji hao kuangalia fursa
mbalimbali za maendeleo zilizomo nchini.
Dk. Mwinyi aliwaeleza
wageni hao sekta tatu muhimu za uchumi wa Zanzibar ikiwemo Utalii, Uvuvi na Kumbi
za mikutano, hivyo aliwataka kuangalia namna ya kuwekeza kwenye maeneo hayo ili
kutoa ushirikinao kwaajili ya maendeleo ya Zanzibar na wazanzibari kwa ujumla.
Akiizungumzia sekta ya
Utalii, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wawekezaji hao kwamba Zanzibar ni kisiwa cha utalii chenye vivutio vingi vya
Fukwe za bahari na Hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe ambacho awali kilipokea watalii
zaidi kutokaItalia na wawekezaji wengi walitumia fursa hiyo kuwekeza na baadae
watu wa Ulaya Mashariki waliendelea kuingia Zanzibar, hivyo aliikaribisha Kampuni
ya Ujenzi wa Reli na Uwekezaji kutoka China, kuangalia fursa ya Mji Mkongwe
wenye majengo ya historia kwa kufanya uwekezaji wa hoteli za kisasa ili kuwavutia
Wachina wengi kuingia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, aliwaeleza pia kuangalia
namna ya kuwekeza kwenye kumbi za mikutano ya kimataifa kwani Zanzibar ina
maeneo mengi ya mapumziko kwa watalii na uwekezaji sambamba na kuwakaribisha
kwenye uwekezaji wa visiwa vidogo ambavyo ni vivutio vizuri kwa watalii ili
kutoa fursa kwa mataifa mbalimbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar.
Dk. Mwinyi pia
aliizungumzia sekta ya uvuvi na kuwaeleza wageni hao kwamba uvuvi ni sekta
kiongiozi inayosadifu dhana nzima ya Uchumi wa Buluu kutona na maumbile ya
visiwa vya Unguja na Pemba kuzungurukwa na bahari ya Hindi.
Hivyo aliwaeleza
kuangalia zaidi uwekezaji wa uvuvi wa kina kirefu cha maji kwani Zanzibar ina
rasilimali ya samaki wengi watakaosafirishwa hadi mataifa mengine duniani.
Pia, aliwaeleza
kuangalia namna ya kufanya kilimo cha samaki hai ambacho mazingira ya Zanzibar
yanatuhusu ustawi wa kilimo hicho. Sambamba na kuangalia uwekezaji kwenye sekta
ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege vya kisasa, bandari na
barabara zenye viwango vya hali ya juu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya
uchumi wa Zanzibar.
Akizungumza kwenye hafla
hiyo, Meneja mwendeshaji wa kampuni hiyo ya Ujenzi wa Reli na Uwekezaji ya
China ambae pia ni mkuu wa msafara, Hao Ping Dong alimueleza Dk. Mwinyi, kampuni
yao ina miradi mingi ya mandeleo na tayari imewekeza maeneo mengi duniani.
Alieleza sekta ya ujenzi
ni sekta kuu inayojishulisha zaidi kwenye kamapuni yao pia wamejikita kwenye ujenzi
wa viwanja vya ndege, hoteli na majengo makubwa.
Bw. Ping alieleza
kufurahishwa kwakwe na uwepo wao Zanzibar yeye na wenziwe na kutoa Shukrani
zake kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwapokea Ikulu, Zanzibar. Hata hivyo alimuahidi
Dk. Mwinyi kujenga ushirikiano mzuri baina ya Kampuni yake na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment