Habari za Punde

Tuzienzi na kuzithamini rasilmali za nchi zituletee maendeleo - Mhe Othman

 

Mkoa wa Kusini Unguja,

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha  ACT- Wazalendo Zanzibar Mhe, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba rasilimali za nchi zilizopo ni mali ya wananchi na kwamba kila kiongozi mwenye dhamana anawajibika kuzisimamia kwa uwazi, uaminifu na uadilifu ili kuleta maendeleo kwa niaba ya wananchi wenyewe.

Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo  huko Chwaka Wilaya ya Kati Unguja, alipohutubia wananchi na wafuasi wa Chama hicho  katika mkutano wa hadhara akielekea kukamilisha mfululizo wa mikutano ya aina hiyo katika wilaya zote za Unguja na Pemba tokea kuruhusiwa kwa mikutano ya kisiasa nchini Tanzania.

Mhe Makamu amefahamisha kwamba nchi zote  duniani zilizoweza kupiga hatua hazikuwa na miujiza bali imetokana na viongozi wao kuwa waadilifu , waamini na wanaowajibika  vyema kwa wananchi sambamba kuwa na uwezo mkubwa wa kupanga na kujiamulia wenyewe mambo ya nayohusu maendeleo yao.

Aidha Mhe. Othman mesema kwamba ili Zanzibar iweze kuendelea na kupiga hatua  katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na maendeleo inahitaji uwajibikaji na uadilifu kwa viongozi wanaoshika nafasi mbali mbali ili kuweza kuleta maendeleo ya wanachi katika sekta na nyanja tofauti. 

Amefahamisha kwamba ahadi ya chama hicho kwa wananchi wa Zanzibar ni kupigania jitihada za maendeleo kwa pamoja na kwa kuweka misingi imara zaidi ya uwajibikaji wa viongozi wanaoshika dhamana mbali mbali za kuwatumikia wananchi na pale wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo viongozi hao waweze kuwajibishwa na wananchi wenyewe.

Amesema kwamba siri ya mafanikio ya kimaendeleo katika taifa ,lolote duniani ni kuendesha na kusimamia masuala ya nchi  kwa misingi ya uwazi na  kuwepo viongozi wanaopewa dhamana wenye uwezo mkubwa waa kutekeleza na pia kusimamia vyema majukumu yao waliyopewa .

Aidha amesema kwamba kazi moja ya chama cha siasa ni kuhakikisha kwamba wanawasimamia ipasavyo viongozi na serikali kwa jumla na kuwasemea wananchi  hasa kwa vile chama na serikali ni vitu viwili tafauti katika kuisimamia serikali ili kujenga taifa imara lenye viongozi wenye nidhamu na uwajibikani na pia kuepuka kufanya ufisadi.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho  ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Mandeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban, amesema kwamba ahadi ya chama hicho  kwa wazanzibari ni kuwaletea wanchi pamoja katika Zanzibar yenye umoja katika jitihada za kuijenga nchi yao.

 Aidha amesema kwamba chama hicho  kitaendelea kuwa  cha kusimamia  haki,  umoja na mishakamano kwa  wanyonge na kujenga taifa lenye maadili ya wazanzibari  kwa kuwa hiyo ndio moja wapo ya kazi ya chama cha Siasa .

 

Mwisho

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

30, Julai, 2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.