Habari za Punde

Mhe Hemed aendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa Chama jimbo la Chambani na Kiwani

 

Wanachama wa CCM wakila kiapo cha utii mara baada ya zoezi la kukabidhiwa kadi wanachama wapya waliojiunga CCM wakati wa ziara ya kuimarisha Chama Jimbo la Chambani.                                             

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Kadi ya CCM Ndg. Said Zubeir Muhammed (wape Salam) alierejesha Kadi ya ACT Wazalendo na kuamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.                                                                              

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi na wanachama wa CCM kuongeza nguvu katika kukiimarisha Chama kwa kuweka mipango na mikakati sahihi itakayowavutia wananchi na wapenda Amani itakayowavutia wapinzani kujiunga na CCM.

 Akiendelea na ziara ya kuimarisha Chama katika Jimbo ya Chambani na Jimbo la Kiwani  Mhe. Hemed amewataka  Wananchi kujiunga na CCM ambayo inatekeleza ahadi zake kwa kasi kubwa na kuwaletea maendeleo ya haraka.

 Sambamba na hayo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewataka viongozi wa CCM kuendelea kuinadi na kuitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya kimkakati na maendeleo ambayo itawanufaisha wazanzibari wote inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

 Amewasisitiza Viongozi wa Kamati za Siasa za Jimbo, Wilaya na Mkoa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano uliopo ndani ya Chama kwa kufuata miongozo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

 Amesema CCM itaendelea kutekeleza ahadi zake kwa kuziondoa changamoto zilizopo na zitakazojitokeza ikiwa ni pamoja na kuajiri Walimu na Madaktari  walio na sifa katika fani hzio

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefafanua kuwa Serikali itazijenga barabara zote kwa kiwango cha Lami sambamba na kupeleka miundombinu ya maji katika vijiji ambavyo huduma hiyo haijafika kikiwemo kijiji cha Miamboni ambacho kimekosa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Mhe.Hemed ameeleza kuwa Jimbo la Kiwani ni miongoni mwa Majimbo yaliyobahatika kupata miradi mingi ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya Kendwa, ujenzi wa skuli Nne za Ghorofa pamoja na ujenzi waTangi la Maji safi na Salama lenye ujazo wa Lita Milioni moja.

Amesema kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussen Ali Mwinyi kuna kila sababu Wananchi kuwapa kura nyingi ifikapo 2025 ili waweze kuendelea kuwafanyia mambo  mazuri kwa wakati sahihi .

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndg Abdallah Muhamed Madishi amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa  maamuzi yake ya kuwajengea Soko kubwa la Kisasa la Mtambile ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara na wajasiriamali kufanya shughuli zao kwa ufanisi na Wananchi kupata huduma stahiki katika sehemu sahihi.

Ameeleza kuwa juhudi hiyo inadhihirisha azma ya Rais Dkt. Mwinyi ya kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika sehemu salama na kuacha na kufanya biashara sehemu zisizo rasmi

Nae Muwakilishi...... Mhe. Maryam Azzan na Mhe. Shadya Muhamed wameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kufikisha huduma mbali mbali kwa wananchi ikiwemo Afya, elimu, maji safi na Salama, umeme na barabara ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa masafa ya karibu na maeneo yao.

 Wameeleza kuwa ni wajibu wa Viongozi wa CCM kuanzia Shina hadi Taifa kufuata nyayo za Viongozi wakuu wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhubiri Amani na utulivu pamoja na kueleza mema yanayofanywa na Serikali zao.

Katika ziara hiyo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amepokea zaidi ya Wanachama 500 wakiwemo wanachama wapya na waliotoka vyama vya upinzani.

 Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao Ndg. Said Zubeir Muhamed (wape Salam) kutoka Chama Cha ACT Wazalendo ameeleza kuwa ameamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi kutokana na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na dhamira thabiti ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwaletea maendeleo wazanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.

Ziara hiyo ni muendelezo wa Ziara ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndg. Hemed Suleiman Abdulla kutembelea majimbo yote ya hamsini ya uchaguzi ambapo tayari ameshatembelea Majimbo arobaini na Tano kwa lengo la kuimarisha Chama.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

28 Agosti, 2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.