Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria uliofanyika tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023 jijini Algiers, Algeria. Pembeni yake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo.
Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudia na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na
Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria wakati wa Mkutano wa Tano wa Tume
ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Maafisa
Waandamizi uliofanyika tarehe 30 hadi 31 Julai 2023.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati
Madhumuni ya mkutano huo ni kutathmini hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye Mkutano
wa Nne uliofanyika mwaka 2010 jijini Dar es Salaam.
Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Tax ameleza
kuwa mkutano huu ni kielezo cha dhamira ya dhati kati ya Tanzania na Algeria
kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka mfumo rasmi wa kujitathimini
katika masuala mbalimbali yaliyokubalika.
‘’ Ni imani yangu kuwa wataalam wetu wamefanya kazi kubwa katika
majadiliano kwa kuangalia maeneo muhimu na ya kipaumbele ili kuendelea kukuza
ushirikiano kwa maslahi ya nchi zote mbili" alisema Dkt. Tax.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed
Attaf katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huo umetoa fursa ya
kujadili na kukubaliana maeneo ya kipaumbele kwa maslahi ya pande mbili.
Pia ameeleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano ni ishara ya wazi kuwa
nchi hizi zitaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo sanjari na kukuza
ushirikiano kwenye maeneo mapya yenye tija.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kushirikiana kwa karibu na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi pamoja ili kufikia
malengo tuliyojiwekea katika sekta mahsusi za ushirikiano,’’ alisema Mhe.
Attaf.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Attaf wamewashukuru Wakuu wa Nchi wa pande zote mbili kwa utayari na jitihada zao wanazozifanya katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarishwa zaidi kwa maslahi mapana ya nchi mbili.
Mkutano huo umejadili na kutathimini utekelezaji wa maeneo ya
ushirikiano katika Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi,
Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi na Afya, na Sanaa na Utamaduni.
Katika kuendelea kuhakikisha kwamba Tanzania na Algeria zinatekeleza maazimio ya mkutano husika, nchi hizi mbili zimekubaliana kuitisha mkutano wa sita utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment