Habari za Punde

KIST kuanza kusomesha mafunzo ya Huduma za Viwanja vya Ndege (Ground Handling)

Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karumé (KIST), Dk.Mahmoud Abdulwahab Alawi (kulia),  akitia saini MoU ya kuendesha mafunzo ya  Huduma za Viwanja vya Ndege (Ground Handling), (kushoto) ni Bw. Hassan S . Ngozi, Mtaalamu wa  mafunzo ya huduma ya Viwanja vya Ndege (Ground Handling, (katikati) ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Abdullah Said, akishuhudia hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Mbweni Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi na washiriki walioshuhudia hafla ya utiaji saini MoU ya kuendesha mafunzo ya huduma za Viwanja vya Ndege (Ground Handling), baina ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karumé (KIST) na Mtaalamu wa mafunzo hayo, Bw.Hassan S  Ngozi hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Bweni Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Abdullah Said (katikati) akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi mbali mbali wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karumé (KIST), Pamoja na waalikwa kutoka Taasisi mbali mbali baada ya hafla ya utiaji saini MoU ya kuendesha mafunzo ya huduma za Viwanja vya Ndege (Ground Handling), baina ya Taasisi ya Karume na Mtaalamu wa kutoa mafunzo hayo Bw. Hassan S . Ngozi.

Na Issa Mzee KIST.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema inaunga mkono mpango ulioandaliwa na Taasisi ya  Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) katika utowaji wa mafunzo ya huduma za Viwanja vya ndege .

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla Said, alisema hayo alipokuwa katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya utowaji wa mafunzo hayo kwa Taasisi ya Karume  na wataalamu wa huduma za ndege katika viwanja vya ndege, hafla ilifanyika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Bweni Zanzibar.

Alisema hatua hiyo inakwenda sambamba na dhamira ya Serikali juu ya kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.

Aidha alisema  kuwepo kwa mafunzo hayo itachochea kupatikana wafanyakazi wa kutosha wenye utaalamu wa kutoa huduma kwa kiwango kinachohitajika. 

Katibu huyo alifahamisha kuwa vijana wengi wanamaliza elimu zao na kubakia mitaani kufanya mambo yasiostahiki hivyo kutolea kwa mafunzo hayo itakuwa chachu ya kutimiza ndoto zao na kuipunguzia mzigo Serikali.

“Hakuna sababu kwa huduma hizo kufanywa na wageni ukizingatia hapa nchini kuna vijana wengi hawana ajira hivyo kupitia fursa hiyo itakuwa chachu ya kuwasaidia vijana kupata nafasi hizo na kujikwamua kiuchumi,”alisema.

Hata hivyo Alisema Zanzibar inaendelea kujenga miundombinu na kujenga viwanja vya ndege Unguja na Pemba hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi kubwa ya ndege kutoka nchi mbalimbali kufanya safari zake hapa nchini, hatua ambayo itatanua wigo na kuongeza fursa za ajira katika eneo hilo.

Vile vile alisema kutokana na hali hiyo KIST inajukumu la kuhakikisha wanaandaa wataalamu wataokuwa na uweledi ambao wataweza kufanya kazi hizo ndani na nje ya nchi. 

Hivyo kawataka vijana kutumia fursa ya mafunzo inayotolewa na Taasisi hiyo ili kupata taaluma na ujuzi katika soko la ajira katika Sekta hiyo.

Pia alitumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za ndege ziliyopo ndani na nje kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar na kuwapa fursa za ajira vijana watakaosoma katika kozi hizo ili kwenda kufanya kazi katika Sekta hizo.

Sambamba na hayo alitumia fursa hiyo kuishukuru mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania kwa kuruhusu masomo hayo kufundishwa katika Taasisi ya karume.

Mkuu wa Taasisi ya  Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST),  Dk Mahmoud Abdulwahab Alawi, alisema wamesaini makubaliano hayo kwaajili ya kuendesha kozi tofauti za utowaji wa huduma kwa kazi mbalimbali zinazofanyika katika viwanja vya ndege.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwajengea uwezo wazawa kufanya kazi hizo kutokana na kuwepo idadi kubwa ya viwanja vya ndege na makampuni mbalimbali kufanya safari zake hapa nchini.

Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo na Usafiri wa Anga kutoka Taasisi ya Karume Bw, Ali Hamad Mkali alisema lengo la makubaliano hayo ni kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ndani ya Taasisi hiyo kwa lengo la kuwaandaa vijana ili kuingia katika soko la ajira kupitia eneo hilo la utowaji wa huduma katika viwanja vya ndege.

Nae mtaalamu wa mafunzo hayo Bw. Hassan S. Ngozi alisema watowa huduma za ndege wanahitajika kuwa na taaluma na uelewa ili kuepusha athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Mafunzo hayo ya muda mfupi yatashirikisha kozi mbalimbali ikiwemo usafirishaji wa mizigo, abiria, uangalizi wa mashine za kusafirishia mizigo na mengineyo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.