Habari za Punde

Tanzania na Uganda Kudhibiti Magonjwa Yanayovuka Mpaka

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kwa upande wa Tanzania na Waziri wa Kilimo Mhe. Bright Rwamirama kutoka Uganda wakisaini makubaliano ya kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mipaka katika tukio lililofanyika Septemba 07, 2023 kwenye Ofisi za Wizara ya mambo ya nje jijini Dar-es-salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kwa upande wa Tanzania na Waziri wa Kilimo Mhe. Bright Rwamirama kutoka Uganda wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kusaini makubaliano ya kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mipaka katika tukio lililofanyika Septemba 07, 2023 kwenye Ofisi za Wizara ya mambo ya nje jijini Dar-es-salaam.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano na nchi ya Uganda yanayolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mpaka baina ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega kwa upande wa Tanzania na Waziri wa Kilimo Mhe. Bright Rwamirama kutoka Uganda, tukio lililofanyika Septemba 07, 2023 kwenye Ofisi za Wizara ya mambo ya nje jijini Dar-es-salaam.

Akizungumza kabla ya kusaini Makubaliano hayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa utafiti umeonesha uwepo wa magonjwa mbalimbali ya mifugo ni miongoni mwa sababu za kushuka kwa mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la Taifa.

“Ni lazima tufanye udhibiti wa pamoja na wenzetu wa Uganda ambao mifugo yao imekuwa ikiingiliana na ile iliyopo nchini, hivyo tumekubaliana kuwa na kalenda moja ya chanjo za kudhibiti magonjwa ya mifugo”Amesema Mhe. Ulega.

Aidha Mhe. Ulega amebainisha kuwa hatua hiyo ni matokeo ya mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambao waliafikiana kuchukua hatua ya pamoja katika udhibiti wa magonjwa yanayovuka mpaka.

“Tumeona tuwe na mpango wa miaka mitano ambao ni kampeni maalum ya uchanjaji wa mifugo utakaolenga magonjwa 5 tuliyoamua kuyapa kipaumbele na katika hilo tumeweka azimio la kuhakikisha ndani ya kipindi hicho tuwe tumeyapiga vita na ikiwezekana tuwe tumeyatokomeza kabisa” Aliongeza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa Uganda Mhe. Bright Rwamirama amesema kuwa amefurahishwa na hatua hiyo ambapo ameweka wazi itawasaidia kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini mwao ambayo mengi yametokana na tabia ya mifugo hiyo kutembea kutoka eneo moja kwenda jingine bila kujali mipaka iliyopo baina ya maeneo hayo.

Awali, akiwakaribisha viongozi hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa makubaliano hayo ni huru na upande wowote utakaokusudia kujitoa utapaswa kutoa notisi ya kipindi kisichopungua miezi sita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.