Habari za Punde

Zanzibar inahitaji ufumbuzi wa haraka kuongeza huduma za jamii vijijini - Dk Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji ufumbuzi wa haraka kuongeza huduma za jamii  vijijini.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa chakula barani Afrika, 2023 linaloendelea katika jengo la ukumbi wa mikutano ya kimataifa la Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Rais Dk. Mwinyi alisema ongezeko la vijana wanaokimbilia mijini linatokana na changamoto za kukosekana masoko kwa wazalishaji, vikwazo vya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi maeneo ya vijijini.

Pamoja na kueleza kuwepo  faida ndogo inayotokana na uwekezaji kinyume na matarajio ya vijana, upatikanaji mdogo wa mitaji na masoko, kukosekana kwa miundombinu ya uzalishaji na usarifu wa mazao pamoja nakukosekana mwa  teknolojia ya kisasa.

Rais Dk. Mwinyi alisema katika kutatua changamoto hizo barani Afrika kumekua na utashi wa kisiasa wa kuwahusisha vijana kwenye shughuli za kilimo-biashara kinachohusisha ujasiriamali kwa sekta za uvuvi na ufugaji wa viumbe wa majini na kuwashirikisha vijana na wanawake.

Alieleza bara la Afrika limechukua juhudi mbalimbali ikiwemo kupitisha Mkataba wa Vijana Afrika (African Youth Charter - AYC) na Umoja wa Afrika mwaka 2006, tamko la Mpango wa Utekelezaji wa Vijana wa Muongo mmoja, kuanzishwa dawati la vijana katika mpango mpya wa ushirikiano kwa Maendeleo ya Afrika (NEPAD) na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Kilimo Afrika(CAADP).

Rais Dk. Mwinyi alieleza pamoja na jitihada hizo, Tanzania kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeandaa mikakati shirikishi na tukitekeleza mipango mbalimbali ya kusaidia vijana na wanawake kujishughulisha na kilimo-biashara licha ya kuwepo ushiriki mdogo wa jamii hizo kutokana na upatikanaji mdogo wa rasilimali za uzalishaji, ujuzi mdogo wa kilimo,  vizuizi kwenye mgawanyo wa rasilimali na ugumu wakupata mitaji ya kuendeleza ujasiriamali wao.

Alieleza Zanzibar kupitia mipango ya utekelezaji wa miradi ya uchumi wa Buluu kumewainua vijana wengi na wanawake kutokana na msaada wa fedha za ahuweni ya Uviko 19 kwa kuwashirikisha vijana na wanawake kwenye  kilimo na uvuvi, kuzitumia fursa nyingi kwa kuendeleza uchumi unaotegemea kilimo vijijini

Alisema hatua hiyo imefungua milango zaidi ya ajira kwa maeneo ya uzalishaji wa chakula, uongezaji wa thamani na masoko ya mazao ya kilimo na uvuvi, kuweko kwa uhakika wa chakula na lishe na kupunguza umasikini.

Tumekusanyika hapa kwa kuwa tunajali mustakbali wa vijana na wanawake, ni lazima tushirikiane kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi yenye kusaidia kuwekeza katika kilimo, ufugaji wa viumbe wa majini na uvuvi.”

Naungamkono  jitihada zetu zinazoendelea za ‘Jenga Kesho iliyo bora(BBT)’ ambao ni mfano bora wa jitihada zilizobuniwa ili kufikia ndoto hii.

Akizungumzia Mpango wa maendeleo wa Jenga Kesho yako kwa maisha, (BBT) Rais Dk. Mwinyi alieleza unania ya kuongeza ajira zaidi kwa vijana na wanawake kwenye mifumo ya chakula inayojumuisha, uzalishaji wa mazao (kilimo)ya chakula,, mifugo, uvuvi na Uhifadhi wa chakula kwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, usafirishaji, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko.

Alieleza jukwaa la mwaka huu kuelekea 2030, lin nia ya kumaliza Umasikini na kufikia uzalishaji na matumizi endelevu.

Akizungumza kwenye mkutano huo Waziri wa kilimo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hussein Mohamed Bashe aliupongeza uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya kuwakomboa vijana na wanawake kwa kuwainua kiuchumi kupitia mpango wa Serikali wa “Jenga Kesho yako kwa maisha, (BBT)”.

Alisema kwa mda  refu vijana hawakupewa nafasi ya kujiajiri wala kuwezeshwa kwa lolote ili wajitegemee, sasa kupitia mpango huo utawakomboa vijana wengi Tanzania na kueleza kuwa kigezo kizuri kwa Afrika kujikita kwenye kilimo -biashara.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.